Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dirisha dogo la usajili, linahitaji umakini mkubwa

Victorien Adebayor Deal.jpeg Dirisha dogo la usajili, linahitaji umakini mkubwa

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha la usajili kwa klabu za soka zilizo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linafunguliwa rsmi kesho Jumamosi. Kipindi hiki huitwa dirisha dogo au wengine huita dirisha la majira ya baridi.

Hiki ni kipindi ambacho Ligi nyingi huwa katikati hivyo klabu huwa na nafasi ya kuimarisha kikosi chao na pia wachezaji huwa na fursa ya kuangalia hatima yao ya kitaaluma.

Ni kipindi ambacho klabu zinaruhusiwa kufanya usajili wa kumalizia msimu huu. Hapa nyumbani tayari klabu zimeanza kuhaha kusaka saini za wachezaji wa ndani na wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.

Huko nyuma katika safu hii tuliwahi kuandika makala yenye kichwa cha habari ‘mkataba wa mchezaji ni kama mpira...’ namna unavyoupiga ndivyo unavyokwenda...’’ Maana ya andiko lile ni kwamba makosa yakifanyika kwenye makubaliano ya mchezaji na klabu hayawezi kurekebishika wakati wa utekelezaji.

Tuliongea juu ya umuhimu wa mchezaji kuwa na menejimenti inayoelewa vizuri ibara ya 17 ya kanuni za FIFA zihusuzo uhamisho wa wachezaji wa kulipwa. Uzoefu unaonyesha kwamba wakati wa kuingia mkataba pande zote huwa zina matumaini makubwa katika kile kitakachopatikana ndani ya mkataba. Inapokuja wakati wa utekelezaji au hata usitishwaji wa mkataba ndipo kizungumkuti huanza.

Kwa bahati mbaya wanamichezo wengi, hata mawakala na maofisa wa klabu za hasa katika nchi zetu za Kiafrika hudhani ya kuwa mikataba hufanana. Ni kawaida hapa kwetu Tanzania kusikia watu wakisema mkataba kamili ni ule wa shirikisho la TFF. Ni kweli, shirikisho la mpira hutoa mfano wa namna mkataba unavyotakiwa kuwa kwa kueleza kuwa ni muhimu au lazima vipengele fulani viwemo katika mkataba.

Mfano mkataba lazima uonyeshe muda wa ukomo, mshahara na marupurupu mengine. Hata hivyo, ni juu ya pande zinazoingia mkataba kuwasilisha maslahi yao mezani wakati wa kuingia mkataba. Kama nilivyosema katika safu hii juma lililopita, mkataba wa mwanamichezo unaweza kuwa na vipengele vingi hata vya kipuuzi ili mradi havivunji sharia ya mpira na sharia ya nchi.

Si ajabu kuona mwanamichezo analalamika kuhusu maslahi ya mwenzake kwenye timu moja kuwa bora kuliko yake wakati wanatumikia timu moja.Lisilojulikana ni jinsi kila mtu alivyoweka karata za maslahi yake wakati wa kuzungumza mkataba.Kama jinsi mpira unavyokwenda kutegemea nguvu na sehemu gani ya mwili imeupiga na mkataba vivyo hivyo hutegemea namna ulivyowekewa vipengele vya mslahi ya mchezaji au ya mwajiri.

Tatizo la kuelewa vifungu na maslahi yaliyojificha haliko kwa wachezaji bali pia hata kwa wanasheria wasomi wanaowakilisha wanamichezo.Katika uzoefu wangu wa utawala wa mpira hapa Tanzania nimeshuhudia wanasheria wengi wasomi wakipata wakati mgumu kuwakilisha vema wateja wao katika sekta ya michezo. Sina hakika sasa hali ikoje lakini kwa siku za nyuma waliokuwa na jicho la ziada ni kama mawakili maarufu wakati ule Damas Ndumbaro, Rutashobya na James Bwana.

Ni vizuri kwa klabu, mwanamichezo au hata wasimamizi wake kujitahidi kupata uzoefu wa mikataba ya wanamichezo wengine wa hapa nchini au nje ya nchi kama imeonekana kubeba vizuri maslahi ya upande husika.

Kuna mikataba imewahi kugonga vichwa vya habari kama ya ajabu lakini inaweza kutumika kuwasaidia wanamichezo, wawakilishi wao na hata taasisi kama shirikisho na klabu kujua namna ya kulinda maslahi kwenye mkataba. Hapa chini ni baadhi ya mikataba ya kushangaza ya wanamichezo:

Neymar na wageni

Mwaka 2013 mchezaji kutoka Brazil Neymar alijiunga na klabu ya Barcelona ya Hispania. Katika mkataba wake kiliwekwa kifungu kinachomruhusu kutembelewa na wageni kila baada ya wiki mbili. Klabu yake ya Barcelona ililipia gharama za ugeni huo bila kinyongo kwani ni kifungu cha mkataba ilichoridhia

Samuel Eto’o na ndege binafsi

Kuelekea mwisho wa uwezo wake kama mchezaji wa kulipwa, mchezaji kutoka Cameroon Samuel Eto’o alipata kandarasi katika klabu ya Anzhi Makhachkala. Kwa vile alipachukulia Makhachkala kama kijijini, Eto’o alihakikisha kuna kifungu cha kukodishiwa ndege binafsi kila mara alipotaka kwenda jijini Moscow ambako ndiko alitumia muda mwingi.Klabu ilitekeleza kama ilivyoingia mkataba.

Ronaldinho na ruhusa ya ‘kula bata’

Aliporudi nyumbani akitokea Ulaya, nyota Ronaldinho Gaucho alijiunga na klabu ya Flamengo. Katika mkataba wake aliweka kifungu cha kumruhusu kwenda kwenye kumbi za starehe mara mbili kwa juma. Hili halikuwa tatizo kwa klabu ya Flamengo iliyoamini kuwa Gaucho atafanya vizuri uwanjani anapokuwa na furaha kwenye kumbi za starehe.

Mifano hiyo hapo juu inatuonyesha kuwa maslahi ya mchezaji au ya klabu yanalindwa zaidi wakati wa ‘kuchumbiana’. Ni machache sana mapya yanayoweza kuingizwa kwenye mkataba wakati wa utekelezaji. Utaratibu huu hutumika pia kulinda maslahi ya wadhamini wa mchezaji na wa klabu.

Bahati mbaya sana kwetu Watanzania, maumivu yetu tangu enzi za Karl Peters hutokana na kuingia mkataba bila kujua kilichomo na madhara yake huku tukiishia kulaani kulaghaiwa au kupunjwa wakati wa utekelezaji. Ni wakati sasa kwa wanamichezo wetu na wadau wote kuwa waangalifu katika namna wanavyoendesha mambo yao ikiwa tunataka kuleta maendeleo na kupata faida kutoka kwenye vipaji na uwekezaji michezoni.

Katika msimu wa 2023/24 klabu kadhaa za Tanzania kwa vipindi tofauti, zimefungiwa kufanya usajili kwa sababu ya kutotimiza wajibu wao katika mikataba yao na wachezaji. Kwa haraka sana naweza kukumbuka klabu za Simba, Yanga, Tabora United na Singida Fountain Gate.

Bila kuzionea klabu nilizozitaja zimejikuta katika kadhia hiyo zaidi ya mara moja hivyo kuonyesha kutokuwepo umakini kwenye uandaaji wa mikataba, utekelezaji wa mikataba na hata utekelezaji wa maagizo ya shirikisho la mpira duniani yaani FIFA.

Lakini pia yawezekana klabu hizi zinazidiwa ujanja na menejimenti za wachezaji hasa pale zinapokuwa na haraka ya kunasa saini za wachezaji. Mara nyingine viongozi wa klabu wasiokuwa watendaji hufanya safari za kuwafuata wachezaji bila wasaidizi wenye uelewa na masuala ya mikataba hivyo kujikuta wanatoa ahadi wasizoweza kuzitimiza kama klabu. Hali inaweza kuwa hivyo hata upande wa wachezaji hasa wazawa.

Mara nyingi wachezaji wetu wazawa wanakuwa desperate (na tashwishwi) ya kuchezea klabu kubwa, kupata mshahara mkubwa au kupata gari la ndoto yake hivyo kilicho kwenye mkataba kwake ni ziada.Tunakumbuka huko nyuma picha zilipigwa za wachezaji wakiwekewa bunda la noti nyekundu mezani na kurushwa roho ili waweze kusaini mkataba ambao kwao lililo la muhimu ni tarakimu za mshahara basi.

Kuna maswali kadhaa ya kujiuliza kutokana na mifano ya hapo juu. Je ni kwa nini mara nyingi wachezaji wanaojikuta kwenye mikwaruzano na klabu ni wale wa kigeni? Je, wachezaji wa Kitanzania hutimiziwa matakwa yao kwa mujibu wa mikataba?

Chanzo: Mwanaspoti