Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dilunga arejea, ataka kufunga msimu

Hassan Dilunga HJD Dilunga arejea, ataka kufunga msimu

Tue, 2 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga JKT Tanzania, Hassan Dilunga ameanza mazoezi baada ya kukaa nje miezi sita huku akiweka wazi kuwa ni muda sahihi kwake kwani bado msimu haujamalizika.

Dilunga aliumia Oktoba 30, 2023 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na klabu yake ilithibitisha nyota huyo atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu na sasa rasmi amerejea.

Akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo amesema anamshukuru Mungu kurejea kwenye majukumu huku akiweka wazi kuwa endapo atapata nafasi ya kucheza kwenye mechi zilizobaki zitamsaidia kurudi haraka kwenye ushindani mwakani.

"Kazi yangu ni soka kukaa kwangu nje kwa muda huo nilikuwa sipo sawa kwani mambo mengi yalisimama. Nafurahi nimerudi kipindi hiki ambacho mechi za ligi bado hazijaisha naamini ni nafasi yangu kujiweka sawa kwa msimu ujao," amesema.

"Nikipata dakika chache za kucheza katika mechi kumi zilizobaki ili kumaliza msimu zitanisaidia kunirudisha utimamu wangu wa mwili na kunipa nafasi ya kujiweka kwenye ubora tayari kwa msimu ujao."

Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Simba na JKT Tanzania ambayo amerudi kuichezea kwa mara ya pili, amesema yupo fiti asilimia 100 na ana uhakika wa kucheza akipata nafasi.

"Soka ndio maisha yangu nilikuwa nje kwa muda mrefu nimehakikisha napona na kuwa timamu ndipo nirudi kwenye ushindani. Iliripotiwa nitakuwa nje miezi mitatu, lakini imekuwa zaidi hii ni kwa sababu nilikuwa nataka kurudi nikiwa timamu," amesema.

Dilunga pia amewashukuru viongozi wa JKT Tanzania kwa kuwa naye pamoja kipindi chote alichokuwa anauguza jeraha la mguu.

Mchezaji huyo alijiunga na JKT Tanzania kwa mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa msimu huu baada ya kutemwa na waajiri wake wa zamani, Simba.

Chanzo: Mwanaspoti