Kiungo wa Simba, Hassan Dilunga amewatuliza mashabiki wa klabu hiyo kuwa anaendelea vizuri na afya yake ipo freshi tangu alipofanyiwa upasuaji Afrika Kusini.
Dilunga akiwa Sauzi amesema kwamba alikuwa anapata shida kutembea kutokana na maumivu, ila baada ya matibabu aliyoyapata awali ila kwa sasa maendeleo ni mazuri na hatumii magongo kutembea.
Alisema alitakiwa kurudi Tanzania siku nyingi, lakini ameamua kubaki Sauzi ili kupunguza mawazo kama ambavyo ingekuwa wakati anaishi nchini.
“Unajua nikiwa nyumbani Tanzania napata mawazo na hamu ya kucheza mpira nikiona wenzangu uwanjani na nimeshauriwa ili nipone haraka, natakiwa kuwa katika mazingira mazuri,” alisema Dilunga.
“Nikiwa huku akili ni kufanya ambavyo natakiwa katika matibabu na kuachana na mengine ambayo yanaweza kunitoa katika maendeleo ya afya.” Dilunga ni miongoni mwa wachezaji mwisho wa msimu huu mkataba wake na Simba unamalizika ila uongozi umemhakikishia hautaachana naye. Aliumia goti kwenye mazoezi miezi mitatu iliyopita.