Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dili za usajili zilizobuma kwa sababu za ajabu!

Lewandosk Pic Data Dili za usajili zilizobuma kwa sababu za ajabu!

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Straika wa Paris Saint-Germain, Mauro Icardi ameripotiwa kukataa ofa ya kwenda kujiunga na Newcastle United kwa sababu tu mkewe, mrembo Wanda Nara anataka kubaki Paris.

Newcastle imekuwa ikihusishwa na mastaa kibao wenye majina makubwa baada ya timu hiyo kubebwa jumla na bilionea wa Kiarabu, Mohamed bin Salman kwa mkwanja wa Pauni 305 milioni. Kylian Mbappe na Raheem Sterling ni mastaa wengine waliohusishwa na klabu hiyo ya St James’ Park kabla ya ishu ya Icardi kuibuka.

Hata hivyo, fowadi huyo Muargentina - ambaye amekuwa hana uhakika wa namba huko PSG, hana mpango wa kuhama Paris katika kipindi cha karibuni.

Hizi hapa dili za uhamisho wa mastaa zilizokwama kwa sababu za kuchekesha kabisa.

Lewandowski (Blackburn)

Maisha ya straika wa kimataifa wa Poland, Robert Lewandowski yangekuwa tofauti sana kwenye soka kama volcano ya Eyjafjallajokull isingelipuka huko Iceland. Blackburn Rovers ilikuwa imeshakubaliana kila kitu kwenda kumsajili straika huyo anayekipiga Bayern Munich kwa sasa, miaka 11 iliyopita kipindi hicho alipokuwa Lech Poznan.“Nilipanga na mkuu wangu wa maskauti Martyn Glover kwenda Iceland,” alisema Sam Allardyce, aliyekuwa kocha wa Rovers wakati huo.

“Tulivutiwa na mchezaji na mwenyekiti alikuwa ameshakamilisha mambo kwenda kumsajili kwa Euro 8 milioni. Lakini, mlipuko wa volcano ulisababisha safari zote za Iceland kwa ndege kusitishwa. Tuliishia uwanja wa ndege wa Manchester na wiki moja au mbili baadaye, akasajiliwa na Borussia Dortmund. Sikumbuki kilichotokea hadi niliposoma mahali, Lewandowski ameshanunuliwa.”

Aubameyang (West Brom)

Straika wa Arsenal alifunga hat-trick dhidi ya West Brom, Agosti mwaka huu, lakini alikaribia kabisa kujiunga na timu hiyo maarufu kama The Baggies. Stuart White, skauti wa zamani wa klabu hiyo, alipendekeza jina la Aubameyang kwenye klabu hiyo mwaka 2011 baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa huko Saint-Etienne.

“Nilikwenda Dijon usiku mmoja wa Ijumaa kwenda kumtazama mchezaji mmoja, mshambuliaji ambaye hakunivutia kabisa,” alisema White.

“Lakini, nilikuwa na bonasi ya mechi moja kabla sijarudi nyumbani Jumapili, hivyo nilikwenda kutazama mechi ya Auxerre v Saint-Etienne usiku wa Jumamosi. Saint-Etienne ilitoka sare ya 2-2, lakini Aubameyang na Emmanuel Riviere walicheza vizuri sana. Nilirudi nikiimba jina la Aubameyang, na ilikuwa bahati wakala wake alinipigia wiki mmoja baadaye kwa sababu alijua nilikuwapo kwenye mechi ile. Ni wazi alizipigia timu nyingi, lakini Auba kipindi kile alikuwa akitokea kwa mkopo AC Milan na alikuwa tayari kuja England. Maskauti wetu wengine walikwenda kumtazama kwenye mechi dhidi ya Sochaux, alifunga bao kwenye kipigo cha 2-1, lakini hakucheza vizuri usiku huo na dili likafia hapohapo.”

Van Dijk (Crystal Palace)

Kocha, Neil Warnock alikaribia kabisa kumsajili beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk kabla ya Crystal Palace kusitisha dili hilo kwa madai kwamba Mdachi huyo hana kasi uwanjani. Dili hilo la kumtaka kumpeleka Van Dijk huko Selhurst Park lilipangwa mwaka 2014, kipindi hicho beki huyo alikuwa akikipiga Celtic ya Scotland.

Warnock alisema: “Van Dijk nimefurahi kwa kuendelea kucheza kama anavyocheza. Tulitaka kumsajili Palace kwa ada ya Pauni 6 milioni tu, lakini bosi wangu wa maskauti aliniambia jamaa yupo taratibu sana uwanjani. Nadhani yule skauti bado yupo kazini hajapoteza nafasi yake!”

Michael Essien (Burnley)

Gwiji wa Chelsea, kiungo Michael Essien alikwenda kufanya majaribio Burnley wakati yupo mdogo baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ghana kwenye Kombe la Dunia la wachezaji chini ya miaka 17. Lakini, klabu hiyo yenye maskani yake Lancashire iliachana na mpango wa kumsajili Essien kwa sababu tu ya kung’ang’ania sera yao ya kutolipa mshahara zaidi ya Pauni 60 kwa wiki kwa mchezaji anayejifunza.

Mwaka 2009, mwenyekiti wa zamani wa Burnley, Brendan Flood aliambia The People: “Niligundua Michael Essien alifanya majaribio hapa kwa siku chache. Mmoja wa wachezaji mahiri kabisa, lakini hatukumsajili. Sera ya klabu hailipi mshahara unaozidi Pauni 60 kwa wiki kwa mchezaji ambaye bado yupo kwenye mafunzo.”

Diego Maradona (Sheffield Utd)

Staa wa Kiargentina, Diego Maradona alikuwa kwenye ubora wake kwa timu ya taifa na klabu yake ya Napoli, ambapo aliibadilisha timu kutoka kuwa ya kawaida na kubeba mataji mawili ya Serie A. Lakini, wangekuwa Sheffield United ambao wangefaidi maajabu ya staa huyo, wakati ilipokaribia kumsajili mwaka 1978. Sheffield United kipindi hicho ilikuwa Daraja la Pili, ilituma mawakala wake kutoka Tottenham kwenda kumfuatia mchezaji huyo huko Amerika Kusini. Kocha wa Sheffield, Harry Haslam na mkurugenzi John Hassle walipanda ndege kwenda Buenos Aires. Lakini, kwa wakati huo Sheffield United tayari ilikuwa imeweka mahali pazuri dili la kumsajili Alejandro Sabella na Pedro Verde, lakini baada ya kumtazama Maradona mazoezini, Haslam alivutiwa na kusema: “Namchukua, shilingi ngapi?”

Haslam alikutana na wakati mgumu ambapo wahuni wa Argentina walimwambia watamruhusu Maradona aondoke kama tu watalipwa Pauni 150,000 zaidi ya kile kiwango walichokubaliana kuwalipa Argentinos Juniors. Kutokana na siasa hizo, Sheffield walisitisha usajili.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz