Ndo hivyo. Dili la Declan Rice la kung’oka West Ham United na kutua Arsenal linachukua muda wa kukamilika baada ya timu hizo mbili kushindwa kuafikiana kwenye mtindo wa malipo.
West Ham wameshakubali kumpoteza kiungo huyo matata kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Arsenal wamejiweka pazuri kwenye mchakato wa kunasa saini yake baada ya kuweka mezani ofa ya Pauni 105 milioni, wakidai watatanguliza kulipa Pauni 100 milioni na Pauni 5 milioni zilizobaki zitalipwa baadaye kulingana na maendeleo ya uwanjani ya staa huyo.
Lakini, West Ham wanaweka ngumu wakitaka mkwanja wote uwe umemalizwa hadi kufikia mapema 2025, wakati Arsenal wanahitaji kulipa pesa hiyo katika kipindi cha miaka mitano.