Mabosi wa Azam FC walikuwa wakikuna kichwa wakimpigia hesabu kocha wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge ili aje kukinoa kikosi hicho, lakini matajiri wa kiarabu wa timu hiyo wametibua dili baada ya kumwekea kocha huyo Mkongoman fedha za maana mezani ili kusalia Omdurman.
Iko hivi. Azam kwa sasa inatafuta kocha mpya ili aione kwa msimu ujao ikiamini ikimpata mapema atakisoma kikosi kabla ya ligi kumalizika na ataungana na makocha waliopo kuchambua na kutoa mapendekezo ya timu ikiwemo usajili kuhusu msimu ujao walioupania zaidi na katika mipango yao jina lililokuwa limepewa kipaumbele ni Ibenge.
Azam ilianza mazungumzo na Ibenge na kumpa ofa ya kutua Dar es Salaam kuchukua mikoba iliyoachwa na Mfaransa Denis Lavagne, lakini hakujibu ofa hiyo licha ya mawasiliano ya kawaida baina yake na mabosi wa klabu hiyo wanaoamini Ibenge anaweza kuibadili timu hiyo na kuipa mafanikio kama alivyofanya kwa Hilal.
Hata hivyo, huenda dili hilo likaota mbawa kama Ibenge atafanikiwa kuifikisha Hilal robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo anahitajika kushinda au kutoa sare mchezo wa mwisho dhidi ya Al Hilal ya Misri ugenini ambapo matajiri wa Hilal wamemuahidi kumuongezea maslahi mara mbili ya anachokipata sasa pesa ambayo ni nyingi sana kwa Azam.
Pamoja na sekeseke hilo, lakini chanzo chetu kutoka Azam kimeeleza bado hawajakata tamaa ya kumpata Ibenge lakini hata ikitokea wakamkosa bali watashusha kocha mwingine mwenye uzoefu na soka la Afrika kutoka mataifa ya Ulaya.
"Wale jamaa (Hilal) wamemuahidi Ibeng pesa nyingi kama atatinga robo fainali pia bado wana mpango naye wa muda mrefu," kilieleza chanzo na kuongeza;
"Lakini bado hatujaka tamaa, tunaendelea kuwasiliana naye na kumshawishi na kama tutaona haiwezekani kabisa tutaleta kocha mwingine ambaye yupo kwenye Top Four (nne bora) ya lisiti yetu na huyo atatoka ulaya ila analijua vyema soka la ukanda huu."
Azam iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na alama 47 baada ya mechi 25 imeendelea kujifua kipindi hiki cha kupisha mechi za timu za taifa chini ya kocha Dani Cadena na Jumatano iliyopita ilicheza mechi ya kirafiki na JKU ya Zanzibar ikashinda 2-0 na kesho Jumatatu itapimana nguvu na KMC uwanja wa Azam Complex kisha kuendelea na ratiba za mechi za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iliyofika robo fainali, na Ligi.