Straika wa Kagera Sugar, Anwary Jabir alibahatika kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya KAA Gent ya Ubelgiji, lakini dili hilo lipo fiftefifte (50/50) kwa sasa, huku akifichua somo kubwa alilolipata huko juu ya wenyeji wao kuchukulia kwa uzito mchezo tofauti na Tanzania.
Anwary alifichua hayo kwa mara ya kwanza wakati ametua Ubelgiji walimpokea watalamu wa kujua ufiti wake kabla ya kumpeleka kwenye timu husika, ili kwenda kuangaliwa kama anafaa kuendelea na majaribio au la.
"Kiukweli mazoezi ya kule kama haupo fiti unaweza ukafia uwanjani, wenzetu wapo mbali na hawana mchezo mchezo na kazi hiyo, baada ya kunipokea watalamu hao wakanipima kama nina fitinesi nzuri, kisha nikapelekwa kwenye timu.
Jabir alifanya majaribia hao chini ya wakala Mtanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) akaongeza; "Kiukweli hata kama sitafaulu, lakini niliyojifunza yananisaidia kwenye karia yangu, naamini kuna kitu kikubwa nimekiongeza."
Nje na hilo, alizungumzia uwepo wa fununu za kutaka kurejea Dodoma Jiji; "Nina mkataba wa mwaka mmoja na Kagera Sugar, siyo Dodoma pekee bali kuna Mtibwa Sugar na KMC, pamoja na hayo yote wanapaswa kuzungumza na waajiri wangu.
"Mchezaji unapokuwa na mkataba lazima uzingatie sheria zinataka nini ili kuepuka migongano ambayo haina sababu, kama zinahitaji huduma yangu zinapaswa kuzungumza na uongozi wa Kagera."