Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diego Simeone anavyomtesa Guardiola kwa mshahara

IMG 4262.jpeg Diego Simeone na Pep Guardiola

Sun, 11 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni hivyo. Diego Simeone anayeinoa Atletico Madrid ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.

Kwa mujibu wa chapisho la L'Equipe la mwaka huu, Simeone kwa sasa analipwa mshahara Pauni 29,846,244 kwa mwaka, sawa na Pauni 573,966 kwa wiki.

Makocha wawili wanaomfuatia, wanafanya kazi kwenye Ligi Kuu England. Unajua? Je ni makocha gani wengine waliofanikiwa kuingia kwenye tano bora ya wale wanaovunja mkwanja mrefu kutokana na kazi yao hiyo ya ukocha.

Hii hapa orodha ya makocha watano wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye soka la dunia.

5. Thomas Tuchel (Pauni 202,815 kwa wiki)

Kocha huyo Mjerumani alifutwa kazi Chelsea, lakini mambo hayakuwa mabaya kwake, akaenda kupata kazi nyingine ya maana ya kuinoa Bayern Munich ya huko Ujerumani. Katika msimu wake wa kwanza, akiongoza timu hiyo kwa miezi michache tu, lakini aliweza kuipa taji la Bundesliga. Tuchel alisaini dili la maana, akilipwa mshahara wa Pauni 202,815 kwa wiki na mwaka anaweka mfukoni Pauni 10,547,580.

4. Max Allegri (Pauni 217,011 kwa wiki)

Juventus mambo yamekuwa si mambo kwa misimu ya karibuni huko kwenye Serie A. Imekuwa ikiyumba pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, jambo hilo haliifanyi mabosi wa miamba hiyo ya Italia kushindwa kutoa dili za maana kwa makocha wao na ndiyo maana inamfanya Max Allegri kuwa mmoja wa wanaolipwa pesa ndefu, ambapo Mtaliano analipwa Pauni 217,011 kwa wiki sawa na Pauni 11,284,620 kwa mwaka.

3. Jurgen Klopp (Pauni 302,194 kwa wiki)

Liverpool haikuwa kwenye ubora mkubwa kwa msimu wa 2022-23 kwenye Ligi Kuu England na kujikuta ikikosa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Hata hivyo, hilo halimfanya akaunti yake ya benki itetemeke kutokana na Mjerumani huyo kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa pochi nne, alipokea Pauni 302,194 kwa wiki, sawa na Pauni 15,714,096 kwa mwaka.

2. Pep Guardiola (Pauni 379,263 kwa wiki)

Manchester City imekuwa chini ya mikono salama chini ya kocha Pep Guardiola tangu alipojiunga na klabu hiyo yenye maskani yake Etihad. Chini yake, Man City imebeba mataji matano ya Ligi Kuu England ndani ya misimu sita iliyopita na jambo hilo limewafanya mabosi wa Etihad kumpa dili la kumpa mshahara mkubwa, akilipwa Pauni 379,263 kwa wiki, sawa na Pauni 19,721,724 kwa mwaka.

1. Diego Simeone (Pauni 573,966 kwa wiki)

Maisha yamekuwa matamu kwa Diego Simeone huko Atletico Madrid na ndiyo maana amekuwa akidumu kwenye kikosi hicho cha Wanda Metropolitano kutokana na kuvuna mkwanja wa kijanja, unaomfanya awe namba moja kwa makocha wanaolipwa mshahara mkubwa duniani. Muargentina huyo analipwa Pauni 573,966 kwa wiki, sawa na Pauni 29,846,244 anazolipwa kwa kipindi cha miezi 12.

Chanzo: Mwanaspoti