Kikosi cha Yanga kesho kinatarajia kushuka uwanjani kuvaana na Simba katika mechi ya fainali ya michuano ya kuwania Ngao ya Jamii, lakini mmoja wa mabeki wa timu hiyo Dickson Job amepewa dili tamu litakalomrudisha kikosi cha kwanza.
Beki huyo wa kati kwa sasa ana kibarua cha kuhakikisha anapata namba katika kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa ushindani kwa mabeki wenzake chini ya kocha mpya Miguel Gamondi.
Misimu miwili iliyopita beki huyo alijihakikishia namba kikosini chini ya Nasreddine Nabi, kocha aliyeipa mafanikio timu hiyo katika misimu hiyo kabla ya kuondoka na kutua zake FAR Rabat ya Morocco akimtumia kama beki wa kati, kiungo na beki wa kulia.
Hata hivyo, ujio wa Gamondi uimefifisha nafasi yake licha ya kutumika kwenye mechi ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi alipoanza na Bakar Mwamnyeto katika beki ya kati, lakini juzi kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC aliishia benchi.
Katika mechi hiyo, Gamondi aliwatumia Mwamnyeto na Ibrahim Bacca na mabeki wa pembeni walicheza anayeomudu pia kuichezea ikitumika na Kouasssi Attohoula Yao na Joyce Lomalisa.
Bacca na Yao wote kwa wakati mmoja wakiwa wanatimiza majukumu yao walionyesha viwango vizuri kuituliza timu na kupeleka mashambulizi langoni mwa Azam.
Kiwango cha Bacca ni mwendelezo wake wa msimu uliopita na alishafanya vizuri akiwa na Job na hata Mwamnyeto, na mara nyingine alimfanya Job acheze kulia au wote watatu wakianza kwa pamoja kulingana na mfumo.
Upande wa Yao ni wazi kabisa mwenye namba yake amefika, hilo ni kutokana na namna ambavyo alikuwa mwepesi kupeleka mashambulizi langoni kwa Azam pamoja na kupiga krosi, hivyo kumpa wakati mgumu Job kuwa na kibarua cha kupambania namba.
Straika wa zamani wa Yanga, TZ Prisons na Moro United, Herry Morris ‘Ng’wenya’ alisema hana wasiwasi na nafasi ya Job kwani soka ni mchezo wa kupokezana, hivyo atapata nafasi ya kucheza, lakini ni lazima apambane kutokana na ushindani uliopo.
Morris alisema hilo sio kwa Job pekee bali hata wachezaji ambao msimu uliopita walikuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza, kwani mambo yameanza kubadilika wanatakiwa waendelee kuwa na utayari. “Wachezaji wote wanabidi wawe na utayari kwa sababu kocha atakuwa na uhakika wanaoanza na wale ambao wapo nje wote ni wazuri hivyo itamsaidia,” alisema Morris.
Akizungumzia tofauti ya Yao na Job ambao wote wana vimo vifupi, alisema upo na unatokana na mahitaji ya wakati husika ndani ya kikosi.
“Job ni mzuri sana kwenye kukaba akicheza kulia, Yao ni mzuri kwenye kushambulia zaidi, hivyo inategemea na mahitaji ya benchi kwa wakati huo.”
Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Bakari Kigodeko alisema ni wazi Job anatakiwa kuongeza juhudi kwa sababu ushindani wa namba umeongezeka.
“Job asikate tamaa kwa sababu kocha ataendelea kuangalia anayefanya vizuri mazoezini, ukweli ni kwamba ushindani umeongezeka kwenye eneo la beki wa kati na hata kule pembeni alipokuwa anacheza (kulia),” alisema. “Yule mgeni (Yao) kila mmoja ameona namna ambavyo amekuwa na spidi na uwezo wa kupeleka mashambulizi kwahiyo ni wazi Job upande ule ngumu kucheza kwa sasa.”