Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dickson Job, Aziz Ki wasafisha njia ya Ubingwa Yanga

BCB480F2 9E1A 4000 BB42 74D6FCD94860.jpeg Fiston Mayele akimuhadaa mlinzi wa Namungo mchezo wa leo

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Namungo FC umemalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa wenyeji kuibuka kidedea na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao ya Yanga yamefungwa na beki, Dickson Job dakika ya 43 likiwa ni bao lake la kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho.

Bao la pili limefungwa na Stephane Aziz KI dakika ya 51 likiwa ni la tano kwake msimu huu akiwa na timu hiyo katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu.

Yanga imeendeleza rekodi nzuri inapocheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa bao 1-0 na Azam FC, Aprili 25, mwaka jana huu ni mchezo wa 30 mfululizo bila ya kupoteza ambapo kati ya hiyo imeshinda 25 na kutoka sare mitano.

Tangu mara ya mwisho Yanga ilipofungwa mabao 2-1 na Ihefu Novemba 29, mwaka jana kwenye Uwanja wa Highland Estate, huu ni ushindi wake wa tisa mfululizo katika Ligi Kuu Bara.

Mchezo wa mwisho uliopigwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi baina ya timu hizi Desemba 7, mwaka jana, Namungo ilipoteza pia mabao 2-0, yaliyofungwa na Yannick Bangala na Tuisila Kisinda.

Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara mbali na huu baina ya timu hizi uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Namungo FC ilifungwa mabao 2-1, Aprili 23, mwaka jana.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Fiston Mayele na Feisal Salum 'Fei Toto' wakati lile la kufutia machozi kwa upande wa Namungo FC lilifungwa na nyota wake, Shiza Kichuya.

Tangu Namungo FC imepanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20 haijawahi kuifunga Yanga kwani katika michezo nane waliyokutana imepoteza mara tatu na kutoa sare mara tano.

Katika michezo hiyo nane ambayo timu hizi zimekutana tangu msimu huo wa 2019/2020, Yanga imefunga mabao 11 huku Namungo FC ikifunga sita.

Tangu kocha, Denis Kitambi akabidhiwe kikosi cha Namungo Desemba 7, mwaka jana akichukua nafasi ya Mzambia, Hanour Janza amekiongoza katika michezo nane ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo ameshinda mitatu, sare miwili na kupoteza mitatu.

Katika michezo 22 ambayo Namungo imecheza katika Ligi Kuu Bara imeshinda nane, sare mitano na kupoteza tisa ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo na pointi zake 29.

Kwa upande wa Yanga katika michezo 22 iliyocheza imeshinda 19, sare miwili na kupoteza mmoja tu ikiendelea kujikita kileleni na pointi 59 nyuma ya Simba inayoshika nafasi ya pili na pointi 53.

Ushindi wa leo unaifanya Yanga kuhitaji pointi 21 katika michezo nane iliyosalia ili kutetea ubingwa wake iliouchukua kwa msimu uliopita kwani itafikisha jumla ya pointi 80 ambazo hakuna timu yoyote ambayo itakayozifikia.

Iko hivi, Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi 53 huku ikionekana ndiye mshindani pekee kwa Yanga kwenye mbio za ubingwa hata ikishinda mechi zake zote nane zilizobakia haitaweza kufika kwani itaishia tu na jumla ya pointi 77.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live