Haya kumekucha. Luis Diaz ametishia atang'atuka Liverpool mwishoni mwa msimu huu, wakati dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa kama tu miamba hiyo ya Anfield itampa mkataba mpya supastaa wa Misri, Mohamed Salah.
Klabu kadhaa za Hispania zimekuwa zikimtolea macho mshambuliaji Diaz.
Liverpool wenyewe wamefungua milango ya kupokea ofa ya kuuza washambuliaji wake kwa sababu inao wa kutosha kwenye kikosi hicho cha Merseyside.
Mpango mkubwa wa mrithi wa Jurgen Klopp huko Anfield ni kuona Mo Salah anapewa mkataba mpya, sambamba na wakali wengine, Trent Alexander-Arnold na Virgil van Dijk.
Hapo kwenye ishu ya Salah, kama atasainishwa mkataba mpya, basi jambo hilo litakuwa na athari kubwa kwenye maisha ya mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia, Diaz.
Amekuwa na wakati mgumu katika nusu ya kwanza ya msimu, hata kabla ya wazazi wake kutekwa huko kwao.
Lakini, siku za karibuni, Diaz ameonyesha kiwango kikubwa sana kwa mara ya kwanza tangu alipokamilisha uhamisho wake wa kutoka FC Porto kwa ada ya Pauni 37 milioni, Januari 2022.
Thiago Alcantara na Joel Matip nao wanajiandaa kuachana na maisha ya Anfield wakati mikataba yao itakapofika tamati mwishoni mwa msimu huu.
Mo Salah, Alexander-Arnold na Van Dijk wote watabakiza mwaka mmoja kwenye mikataba yao huko Anfield itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Klabu za Saudi Pro League na Paris Saint-Germain zinamtaka Mo Salah, wakati nahodha wa Anfield, Van Dijk alisema hana uhakika wa kama atabaki au la wakati Klopp atakapoondoka mwisho wa msimu.
Liverpool inaamini itaweza kufanya mazungumzo mazuri na mastaa wake mara tu mkurugenzi wao mpya wa michezo pamoja na mrithi wa Klopp watakapowasili kwenye kikosi.
Mkurugenzi wa Michezo, ambaye atatangazwa siku chache zijazo, atakuwa na jukumu la kutambua kocha mpya wa kuja kuinoa Liverpool kuanzia msimu ujao.
Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso — ambaye ni kiungo wa zamani wa Liverpool, amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kwenda kurithi mikoba ya Klopp.
Kocha Mjerumani, Julian Nagelsmann, yule wa Brighton, Roberto De Zerbi na mwingine wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim wote wamekuwa wakihusishwa na kibarua hicho cha kwenda kurithi mikoba ya Klopp.
Bado hakuna ofa rasmi, lakini kambi ya Alonso inaelezwa wanafahamu mpango wa Liverpool.
Liverpool hawajaweka wazi kama watakuwa bize kusajili kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi licha ya kwamba Bayern Munich wana mpango wa kuvamia Anfield kwenda kunasa huduma ya beki wa kushoto, Andy Robertson.
Liverpool pia imekuwa ikipokea ofa ya kuhusu kipa Caoimhin Kelleher, ambaye ameonyesha kiwango kikubwa golini kila wakati ambao Alisson amekuwa akikosekana.
MAVITU YA DIAZ
KWENYE LIGI 2023/24
-Amecheza: Mechi 25
-Ametengeneza: Nafasi 30
-Amefunga: Mabao 6
-Ametoa: Asisti 3
-Amelenga goli: Mashuti 22
-Amepiga: Pasi 603