Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diarra kwenye simulizi ya mapito ya Ronwen

Diarra Vs Ronwen Diarra vs Ronwen.

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mji wa Port Elizabeth unapatikana huko Mashariki mwa Afrika Kusini, ni kati ya miji ambayo imebeba historia kubwa ya Afrika Kusini kuanzia enzi za ukoloni hadi sasa.

Ilikuwa ni sehemu ya kwanza kufikiwa na Wamishionari na walowezi kutoka Ulaya ambao walienda kuitawala Afrika Kusini kwa kipindi kirefu.

Kwa sasa hauitwi tena Port Elizabeth kwa kuwa ulibadilishwa jina kuanzia mwaka 2021 na kuitwa Gqeberha, jina la Port Elizabeth lilikuwa ni kumbukumbu ya mke wa aliyewahi kuwa gavana wa Jiji hili aliyeitwa Elizabeth Frances.

Mara nyingi hapa ndiyo yanapofanyika mashindano ya Cosafa ya Wanawake ambapo kwenye manispaa ya Nelson Mandela ndio mzigo wote hufanyika.

Nimewahi kusikia vitu vingi kuhusu mji huu kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania waliobahatika kuutembelea lakini kubwa ilikuwa vipaji vya soka vilivyopo.

Kila baada ya maili kadhaa ungekutana na uwanja wa soka na ungeona watoto wanacheza huku na kule.

Hapa ndipo alipozaliwa na William Ronwen, kipa wa Mamelod Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini ambaye alishika vichwa vya habari wakati wa Michuano ya Afcon 2023, kwa uwezo wake wa kuokoa penalti.

Baada ya kuonyesha uwezo huo media mbalimbali ziliandika historia ya maisha yake. Watu wengi walijiuliza kwanini kipa bora kama yeye bado anaendelea kucheza hapa Afrika na asiwe kwenye Ligi kubwa tano kubwa barani Ulaya ama akawa kwenye zile ligi nyingine ambazo hazina umaarufu mkubwa.

Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, katika makuzi yake staa huyu aliwahi kupata nafasi ya kuonekana na maskauti wa klabu ya Tottenham waliovutiwa na kiwango chake.

Baada ya kumuona walimpa nafasi ya kufanya majaribio kwenye akademi yao lakini hakufanikiwa kutoboa.

Inawezekana ikawa kawaida kwa wachezaji bora kukataliwa kwenye timu moja na wakakubaliwa kwenye timu nyingine lakini kwa Ronwen ilikuwa tofauti, alikataliwa na hakurudi tena Ulaya badala yake alirudi Afrika Kusini kuendelea na harakati zake pale Supersport United ambako alipandishwa hadi kikosi cha kwanza alikoendelea kuonyesha makali kisha akasajiliwa Mamelodi ambako yupo kwenye orodha ya mastaa wanaochukua pesa nyingi nchini humo na Afrika kwa ujumla.

Licha ya ubora wake kisha cha kwenda Ulaya kwa sasa kimebaki kuwa historia kwake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hata kwa kipa wa Yanga, Djigui Diarra.

Mwaka 2015 alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Mali cha vijana wa umri wa chini ya miaka 20, kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia kule nchini New Zealand. Mali ilimaliza mshindi wa tatu na Diarra alicheza mechi zote saba.

Ukijaribu kuwatazama wachezaji wenzake wote aliocheza nao kwenye mashindano haya karibia wote walienda zao Ulaya, wengine bado wapo huko na wengine wapo Afrika lakini wote walipata nafasi yakwenda kucheza soka Ulaya baada ya kumalizika kwa mashindano hayo. Diarra licha ya ubora wake langoni bado ilikuwa ngumu kutoboa.

Kwenye makuzi yake ya soka mara zote alikuwa akikatisha kwenye mitaa ya Bamako akiichezea Stade Malien. Kwanini?

Wanasema moja kati ya mambo magumu sana kwenye mpira wa miguu ni kufunga bao, na moja kati ya mambo rahisi ni kuzuia. Siku zote kuzuia ni kanuni kama ilivyo hesabu, lakini kufunga ni asili yaani mtu anazaliwa akiwa anafunga.

Lakini ukiondoa urahisi wa kuzuia, lazima mtu ambaye anazuia awe na sifa. Mfano, kwenye eneo la beki wa kati lazima awe na kimo cha kuanzia futi sita na kuendelea, huku upande wa kipa ni kuanzia futi 6.2 na kuendelea.

Kwa mujibu wa Google, Djigui Diarra ana urefu wa mita 1.75 ambazo ni sawa na futi 5.7. Ronwen ana futi 6.0.

Wote hawa hawajakidhi vigezo vya chini vya kuwa kipa, inawezekana ukawa na kipaji kikubwa lakini kwa nchi za Ulaya kitu cha kwanza wanachokiangalia kabla ya yote ni vigezo.

Kanuni ya 1+1 mara zote inasema ni mbili, hivyo kanuni ya kipa ni lazima ufikie urefu tajwa hapo juu zaidi ya hapo hakuna namna unaweza kutoboa.

Inawezekana kwa sasa tusingemuona Diarra maeneo ya Mbagala kwenye gari la Yanga akienda Azam Complex, inawezekana tusingepishana naye pale Mlimani City akitoka kufanya Shopping lakini Mungu ndio aliamua.

Kuna msemo wa waswahili unasema huwezi kumkataa mwanao kwa ugonjwa wa upele, licha ya kuonekana kuwa bidhaa zisizofaa kule Ulaya, hapa Afrika zinaonekana kuwa ni mkombozi na zinakidhi mahitaji yetu, Ronwen alikuwa mhimili muhimu wa Afrika Kusini kule Afcon wakati Diarra akiwa ndio kipa tegemeo wa Mali kwenye mashindano hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live