Ukitaka uone utekelezaji wa vitendo wa ile kauli ya ukipenda chongo huita kengeza, basi wewe fuatilia tu soka la Bongo.
Watanzania tukishapenda kitu huwa tunaweza kuongea chochote na tukakifananisha na chochote au yeyote hata kama tunaujua ukweli na uhalisia kuwa katika hali ya kawaida kinachofanyika sio sahihi ila ndio hivyo tumeshaamua kuwa na hiyo hulka.
Nakupa mfano mdogo tu wa kipindi fulani bwana mmoja alisema pale Uwanja wa Benjamin Mkapa timu yoyote ikicheza na Simba itafungwa hata ikiwa Barcelona, tena Barcelona ya kipindi hicho ambayo ilikuwa inatembeza dozi.
Na hili limeendelea kujidhihirisha katika fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea huko Ivory Coast ambapo ghafla Wabongo tumeibuka na ufananisho wa kipa wa Yanga, Djigui Diarra anayedakia Mali dhidi ya Andre Onana wa Manchester United ambaye alikuwa na timu ya taifa ya Cameroon kwenye fainali hizo.
Kwamba imeibuka hoja kuwa Diarra ni bora kuliko Onana kwa vile Mali imetinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo na pia amefungwa mabao machache kuliko kipa huyo wa Cameroon ambaye kwenye Afcon amedaka mechi moja.
Kiukweli hiki kinachofanyika ni kumkosea Onana. Kuruhusu mabao Afcon hakupaswi kushushe heshima na daraja la Onana hadi kufikia aonekane anazidiwa uwezo na Diarra.
Onana hachezi Ulaya tena Manchester United na Diarra hachezi Afrika tena Yanga kwa bahati mbaya. Kuna daraja kubwa ambalo lipo baina yao hadi kupelekea hilo litokee na sio kibahatibahati tu.
Kuna mengi ambayo Onana amemzidi Diarra ambayo hayawezi kushushwa kirahisi tu kwa kuangalia matokeo ya timu zao za taifa kwenye Afcon kama ambavyo sisi tunajaribu kufanya hivi sasa.
Tukumbuke Onana hajazaliwa Ulaya. Amezaliwa na kukulia hapahapa Afrika kama ilivyo kwa Diarra tena wote wametokea katika nchi ambazo zinafuatiliwa kwa ukaribu na maskauti wa Ulaya, hivyo kama Onana angekuwa hana uwezo, asingepata fursa ya kwenda Ulaya.