Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diarra anavyoiweka Yanga tumbo joto

Djigui Diarra Maliii Diarra anavyoiweka Yanga tumbo joto

Fri, 26 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Djigui Diarra kimemnogea. Ameiteka namba kwenye kikosi cha Mali na sasa amefuzu 16 Bora. Atakiwasha na Burkina Fasso ya Azizi Ki wiki ijayo nchini Ivory Coast.

Lakini kiwango chake ambacho kimewatoa makipa wakubwa kwenye nafasi zao, kimeibua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa Yanga kwamba huenda wakampoteza dhidi ya timu zenye misuli ya fedha za Arabuni.

Mkataba wa Yanga na Djigui Diarra umebakiza mwaka mmoja na nusu kumalizika lakini mashabiki na hata uongozi wa timu hiyo una hofu.

Kipa huyo licha ya kucheza mechi tisa tu kati ya 11 za timu yake kwenye Ligi Kuu msimu huu, anashika nafasi ya pili katika chati ya makipa wanaoongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao (clean sheets) ambapo amefanya hivyo katika mechi tano huku anayeongoza akiwa amecheza mechi sita bila nyavu zake kutikiswa.

Kana kwamba haitoshi, Diarra katika miezi ya hivi karibuni amejihakikishia nafasi ya kwanza katika kikosi cha Mali mbele ya kipa mmoja ambaye alikuwa akipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele yake.

Makipa hao ni Ismail Diawara anayecheza AIK ya Sweden na Aboubacar Doumbia anayechezea Afrique Football Elite ya kwao Mali.

Kabla ya msimu huu, benchi la ufundi la Mali lilikuwa likimtumia Ibrahim Mounkoro kama chaguo la kwanza golini huku Ismail Diawara akiwa wa pili na Diarra akiwa wa tatu lakini upepo umeonekana kugeuka katika miezi ya hivi karibuni.

Diarra ndiye amekuwa kipa tegemeo wa Mali katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea mwezi huu hadi Februari 11 ambapo amedaka mechi mbili za mwanzo dhidi ya Afrika Kusini na Algeria akiruhusu bao moja. Dhidi ya Namibia pia alidaka dakika zote bila kuruhusu bao na timu yake ikafuzu kwenye 16 bora za Afcon.

Mbali na bao moja aliloruhusu, Diarra kwa mujibu wa mtandao wa Fotmob.com, anashika nafasi ya pili kwa kuondosha hatari nyingi kwenye mashindano hayo hadi sasa akiwa na asilimia 85.7 ambapo ameokoa idadi ya mashambulizi sita kabla ya mechi ya jana dhidi ya Namibia.

Hata hivyo tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti imebaini kuwa Yanga haipaswi kuwa na presha na Diarra kuondoka kutokana na sababu tatu za msingi.

Sababu ya kwanza ni uwezekano finyu wa timu zenye misuli ya fedha zinazoweza kuitingisha Yanga na Diarra mwenyewe hadi kufikia kumnyakua, kutokana na uwepo wa makipa ambao wazuri ambao wana mikataba mirefu katika timu hizo.

Mfano ni katika timu za kutoka Tunisia, Morocco, Afrika Kusini na Algeria ambazo nyingi zinaonekana kutokuwa na mahitaji ya mchezaji wa nafasi hiyo na zinaridhika na makipa ambazo zinao katika vikosi vyao.

Sababu ya pili ni kupanda kwa thamani ya Diarra kwa sasa ambako kunaweza kuzirudisha timu na kuzipa hofu ya kutaka kumnunua ambapo kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt, thamani ya kipa huyo sokoni kwa sasa ni Euro 200,000 (zaidi y Sh 548 milioni).

Na jambo la tatu ambalo linaonekana linaipa Yanga uhakika wa kumbakiza Diarra ni ukaribu na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya kipa huyo na uongozi wake pamoja na mashabiki.

Kocha wa makipa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’ alisema kuwa Yanga inapaswa kuhakikisha inambakiza Diarra kwa muda mrefu kwavile ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye vipaji.

“Diarra ni kipa mzuri na kwa muda ambao amecheza katika ligi yetu ameonyesha kitu cha utofauti na makipa wengine. Tangu Yanga imemsajili amekuwa akitoa mchango mkubwa kwao hivyo kipa kama huyu sio wa kumuacha aondoke kirahisi,” alisema

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: