Kupoteza mechi za jana dhidi ya Ghana na Misri, kumeziweka Burkina Faso na Mali ambazo ni timu za taifa za nyota wawili wa Yanga, Djigui Diarra na Stephane Aziz Ki katika nafasi ngumu kwenye harakati za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Matokeo hayo yamefanya pengo la pointi kati yao na vinara wa makundi yao kuanza kuwa kubwa jambo linaloweka rehani ndoto za nyota hao wawili kushiriki Kombe la Dunia mwakani.
Kichapo cha mabao 2-1 ugenini mbele ya Misri, jijini Cairo jana, kiliifanya Burkina Faso ambayo anaichezea Aziz Ki kujikuta ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na pointi nne.
Burkina Faso ambayo jana haikumchezesha Aziz Ki kwenye mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa kimataifa wa Cairo, imezidiwa kwa pointi tano na kinara Misri huku kila timu ikicheza mechi tatu na nafasi ya pili ipo Guinea Bissau yenye pointi tano.
Kwenye Uwanja wa Machi 26 jijini Bamako, wenyeji Mali walijikuta wakiduwazwa nyumbani na Ghana wakifungwa mabao 2-1.
Katika mchezo huo, Diarra hakupata nafasi ya kucheza na badala yake alitumika kipa Mamadou Samassa.
Ni ushindi ambao umeipeleka Ghana hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi I ikifikisha pointi sita sawa na kinara, Comoro.
Mali iliyo inashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Afrika ya Kati iliyopo nafasi ya nne.