Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Desemba ya kibabe Kagera Sugar

Kagera Sugar Desemba Desemba ya kibabe Kagera Sugar

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Desemba hii ni ya kiume kwa timu ya Kagera Sugar kwani kabla ya mwaka kuisha itacheza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya vigogo watatu wa soka la Bongo kwa sasa, Simba, Yanga na Azam.

Kagera iliyotoka kupoteza mechi ya ligi dhidi ya Coastal Union ikifungwa 1-0 kule Tanga, leo Jumanne itakuwa Dar es Salam ikijiandaa na mechi ijayo dhidi ya Simba itakayopigwa Ijumaa hii, Desemba 15, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa ligi.

Kagera kwa sasa ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 13 baada ya mechi 11 ilizocheza na kushinda tatu, sare nne na kupoteza nne huku Simba ikiwa nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi nane, kushinda sita, sare moja na kupoteza moja.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Desemba 12, 2022 mechi iliyopigwa Kaitaba, Kagera na kumalizika wa sare ya mabao 1-1.

Wakata miwa hao wa Bukoba, wamepania kufanya vyema kwenye mechi hiyo ili kupata mwanga wa kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo ikiwamo ile ya Azam, Desemba 21 pia itakapokutana na Yanga Desemba 26 mwaka huu.

Kocha mkuu wa Kagera, Mecky Mexime alisema; “Tunajua ugumu tulionao kwenye ratiba lakini tunajipanga kufanya vizuri. Wote tunacheza ligi moja hivyo lazima tukutane na timu hizo hata kama isingekuwa sasa tungekutana tu.

“Kila mechi inakuwa na mpango wake, tunajua ukubwa wa Simba, tunajipanga kuwakabili na lengo ni kupata matokeo chanya yatakayorejesha morali kikosini.”

Chanzo: Mwanaspoti