Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Deschamp: Hakuna namna, Mbappe atapasuliwa

Mbappe Injury Deschamp: Hakuna namna, Mbappe atapasuliwa

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps amesema supastaa Kylian Mbappe atahitaji kufanyiwa upasuaji wa pua baada ya kuumia kwenye mchezo wao wa kwanza wa Euro 2024 dhidi ya Austria, Jumatatu iliyopita.

Katika dakika za mwisho cha mchezo huo ambao Les Bleus ilishinda 1-0, Mbappe aliruka juu kupiga mpira kichwa na hivyo kujigonga kwenye bega la Kevin Danso na hivyo kuvunjika pua.

Baada ya damu nyingi kutoka na kisha kupimwa na kuonekana amevunjika pua, staa huyo mwenye umri wa miaka 25 alitolewa uwanjani.

Saa kadhaa mbele baada ya tukio hilo, kocha Deschamps alisema staa wake huyo hayupo poa, wakati huo chama cha soka cha Ufaransa kikifichua kwamba kipo kwenye maandalizi ya kutengeneza maski kwa ajili ya kumsaidia mchezaji huyo kukinga pua yake.

Hata hivyo, bado kumekuwa na mashaka makubwa kuhusu Mbappe atarudi uwanjani muda gani na kuona kama atahitaji upasuaji kwenye hilo. Wasiwasi uliopo ni kama Mbappe ataweza kukipiga na Uholanzi, Ijumaa hii huku kocha Deschamps, akifichua mchezaji huyo atafanyiwa upasuaji mara baada ya kumalizana na michuano ya Euro 2024 huko Ujerumani, ikiaminika anaweza kufanyiwa upasuaji mwezi ujao.

Deschamps alisema: “Jumanne tulimfanyia vipimo zaidi. Ni kitu kilichoshtua. Timu ya madaktari ilifanya kila kitu inachokiweza baada ya vipimo. Hata kama hatafanyiwa upasuaji wa haraka, atafanyiwa hivyo baada ya michuano. Tutaendelea kumfanyia uchunguzi kila siku.”

Gazeti la L’Equipe linadai kwamba Mbappe bado ana matumaini ya kucheza dhidi ya Uholanzi kesho Ijumaa, lakini hilo bado lina mushkeli.

Mchezo wa mwisho wa Ufaransa kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo watakipiga na Poland, Juni 25.

Kama Les Bleus itamaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, haitacheza mechi yao ya mtoano kwenye hatua ya 16 bora hadi mwanzoni mwa Julai, hivyo jambo hilo litampa muda wa kutosha Mbappe kupata ahueni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live