Winga Denis Nkane anakiri hadi sasa haamini zali lililomkuta la kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara, ASFC mara mbili mbili akiwa na Yanga, huku akisema kujifunza vitu vikubwa vya maisha yake ya soka vilivyombadilisha mtazamo na kumjengea kujiamini kuwa bora zaidi.
Uwepo wa mchanganyiko wa mastaa wazawa na wageni wenye uwezo na vipaji tofauti ndio umemfanya Nkane apate vitu vipya vya kiufundi, akisisitiza mtazamo wake umabadilika akiamini ndoto zake za kufika mbali zitatimia.
"Kila mchezaji anashindana ili apate namba, ndani ya kikosi cha Yanga kina vipaji vya aina yake, kuna funzo nimelipata la kuamini kwenye ndoto zangu kubwa kwamba zitatimia kwa sharti la kupambana bila kukata tamaa.
"Mfano nilikuwa natamani siku moja kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF na nimezivaa, nimepata nguvu za kuamini vitu vikubwa zaidi, jambo la msingi hakuna kinachoshindikana mbele ya bidii," alisema Nkane ambaye alikumbuana na majeraha ya muda mrefu na kushindwa kuitumikia kwa ufanisi tangu asajiliwe kutoka Biashara United msimu uliopita.
"Kupata nafasi ndani ya kikosi cha Yanga kumemisaidia kunijenga na kujiamini zaidi, kocha Nabi alikuwa na kawaida ya kumwamini kila mchezaji inakuwa kazi kwao kuonyesha anachokitarajia kutoka kwako, pia nimepata picha ya namna ya kujipanga zaidi msimu ujao," alisema.