Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Declan Rice anukia Chelsea, Man Utd

Decline Rice Ee.jpeg Decline Rice

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Chelsea inatajwa kuwa katika nafasi kubwa ya kumnyakua kiungo wa West Ham, Declan Rice na kuzipiga bao Manchester United na Manchester City zinazomuwania.

Mkataba wa kiungo huyo na West Ham utafikia tamati Juni 2024 na inadaiwa kwamba klabu hiyo iko tayari kumuweka sokoni katika dirisha la usjaili la majira ya kiangazi kutokana na nyota huyo kuonekana anahitaji changamoto mpya.

Inaripotiwa kuwa mabosi wa West Ham tayari wameshajulishwa na Rice kuwa hana mpango wa kuongeza mkataba mpya pindi huu wa sasa utakapomalizika na amewataka wawe tayari kupokea ofa itakayokuja ikiwa ina maslahi kwake na klabu.

West Ham kwa muda wa mwezi mmoja imekuwa na mazungumzo ya kumshawishi Rice aendeleae kubakia katika klabu hiyo lakini kiungo huyo amegomea akidai anatamani kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. “Ninaona rafiki zangu hapa ambao wanacheza Ligi ya Mabingwa na mataji makubwa,” alinukuliwa Rice wakati alipokuwa akiitumikia England katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika huko Qatar.

Na kwa kutotaka kumpoteza bure au kumuuza kwa dau dogo siku za usoni, West Ham imeshawishika kumuuza kiungo huyo ambapo inaripotiwa kuwa hadi sasa, Chelsea ni vinara katika mbio za kumuwania Rice wakifuatiwa na Manchester United na Manchester City.

Kiwango bora cha nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, kimeonekana kuzikosha timu hizo hasa Chelsea ambayo imeanza kumfuatilia nyota huyo tangu mwaka 2020 ilipokuwa inanolewa na kocha Frank Lampard. Inaripotiwa kuwa West Ham iko tayari kumuuza nyota huyo katika dirisha la majira ya baridi litakalofunguliwa Januari mwakani lakini itaweka sharti la kubaki na kiungo huyo hadi msimu utakapomalizika.

Chelsea inatajwa kuongoza mbio za kumuwania Declan Rice na inadaiwa kuwa imekuwa ikitumia vilivyo urafiki mkubwa uliopo baina ya nyota wake Mason Mount na Rice ili kumshawishi kiungo huyo kujiunga nao. Na taarifa za Chelsea kumtolea udenda Rice zilizidi kupamba moto katika kipindi cha fainali za Kombe la Dunia pale mmiliki wa timu hiyo, Todd Boehly alipokwenda kutazama mchezo baina ya timu ya taifa ya England na Iran ambapo Rice alianza kikosini akicheza sambamba na Jude Bellingham.

Hii ni mara ya pili kwa Chelsea kumfukuzia Rice kwani mara ya kwanza ilikuwa ni ilipokuwa inanolewa na Frank Lampard mwaka 2020 na ilikaribia kumchukua lakini ikashindwa baada ya kuibuka mpasuko ndani ya bodi ya klabu hiyo.

Baada ya hapo, makocha wawili waliofuata, Thomas Tuchel na Graham Potter wameendelea kuvutiwa na uchezaji wa kiungo huyo anayetumia mguu wa kulia. Ikumbukwe mwezi Aprili, kocha wa West Ham, David Moyes alisema kuwa timu yoyote inayomhitaji Declan Rice itapaswa kulipa kitita cha Pauni 150 milioni (Sh 422 bilioni) ili kuishawishi timu yake imuuze nyota huyo Muingereza anayetajwa kuwa na kipaji kikubwa.

Chanzo: Mwanaspoti