Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

De Jong avuruga hesabu Euro 2024

Franke De Jong Netherlandddd Kiungo wa Uholanzi, Frenkie de Jong

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo wa Uholanzi, Frenkie de Jong ametibua mipango ya kocha Ronald Koeman kwenye harakati zake za kwenda kunyakua ubingwa wa fainali za Euro 2024 huko Ujerumani baada ya kuondoka kikosini kutokana na kuwa mgonjwa.

De Jong, 27, anayekipiga kwenye kikosi cha Barcelona kwa siku za karibuni amekuwa akisumbuliwa sana na maumivu ya enka.

Mechi yake ya mwisho kucheza ilikuwa kwenye kichapo cha 3-2 na Real Madrid kwenye El Clasico, Aprili 21 na tangu hapo amekuwa akikimbizana na muda kupona haraka kwa ajili ya fainali hizo za kufukuzia ubingwa wa Ulaya.

Kocha wa Uholanzi, Ronald Koeman bado alimjumuisha kwenye kikosi chake cha Euro 2024 licha ya kuwa majeruhi.

De Jong wiki iliyopita alifanya mazoezi ya peke yake kabla ya kuungana na wenzake kwa mazoezi Jumapili. Lakini, baada ya uchunguzi wa madaktari uliofanyika juzi, vipimo vilionyesha kwamba mchezaji huyo bado hayupo tayari kwa ajili ya kuichezea nchi yake.

Uholanzi iliichapa Iceland 4-0 kwenye mchezo wao wa mwisho wa kirafiki kabla ya kwenda Ujerumani, ambao mabao yao kwenye mechi hiyo yalifungwa na Xavi Simons, Virgil van Dijk, Donyell Malen na Wout Weghorst.

Taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa X ilifichua: “Frenkie de Jong hatashiriki kwenye Euro 2024. Tupo pamoja Frenkie.”

De Jong baadaye alitumia ukurasa wake wa Instagram kuzungumzia masikitiko yake, alipoandika: “Nimehuzunika sana kwa kushindwa kucheza kwenye michuano hii ya ubingwa wa Ulaya. Tumefanya kazi kubwa sana kwa siki za karibuni, lakini enka yangu inahitaji muda zaidi kwa bahati mbaya. Ilikuwa ni ndoto na heshima kubwa kuitumikia nchi yangu kwenye fainali hizi.

“Kuvaa jezi za rangi ya machungwa, kuimba wimbo wa Wilhelmus na kupata ile raha ya mashabiki kukushabikia nchi nzima. Lakini, kwa sasa nitabaki kuwa mshangiliaji nikiwa jukwaani. Twende kazi vijana.”

Uholanzi itaanza kampeni yake ya kusaka ubingwa wa Euro 2024, Jumapili kwa kukipiga na Poland kwenye Kundi D, ambalo wamepangwa pia na timu za Ufaransa na Austria. Mchezaji, Ian Maatsen, ndiye aliyeitwa kuchukua nafasi ya De Jong.

Chanzo: Mwanaspoti