Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

De Gea anarudi Man United kufuata nyayo za mastaa kibao

De Gea Aondoka United De Gea anarudi Man United kufuata nyayo za mastaa kibao

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Manchester United imeripotiwa kuwa na mpango wa kumrudisha kipa wake wa zamani, David de Gea kwa dili la muda mfupi wakati dirisha la uhamisho wa majira ya baridi litakapofunguliwa mapema mwakani.

Miamba hiyo ya Old Trafford inafahamu wazi inaweza kuwa na upungufu wa makipa endapo kama namba moja wao, Andre Onana atakwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Cameroon kwenye fainali za Afcon 2023 zitakazofanyika kuanzia Januari mwakani.

Man United imekuwa kwenye sintofahamu hiyo baada ya kipa Onana kutangaza kurejea kuitumikia Cameroon baada ya awali kutangaza kustaafu. Afcon 2023 itaanza Januari 13 hadi Februari 11, hiyo ina maana, Onana aliyesajiliwa kwa Pauni 43.8 milioni atakosekana kwenye mechi nane za Man United atakapokuwa na Cameroon kwenye fainali hizo.

Hivyo, klabu sasa ipo tayari kumrudisha De Gea — ambaye ilimtupia virago vyake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya mkataba wake kufika tamati.

De Gea, 32, aliichezea Man United kwa miaka 12 kabla ya kuachana na timu yenye maskani yake Old Trafford. Tangu dirisha la majira ya kiangazi lipite, De Gea amekuwa hana timu.

De Gea alipewa ofa ya kutakiwa apunguze mshahara wake kutoka Pauni 375,000 kwa wiki hadi Pauni 200,000 kwa wiki, kitu ambacho alikigomea na hivyo kufunguliwa mlango wa kutokea.

Hata hivyo, Man United ilimtaka asijiunge na timu yoyote hadi hapo watakapokamilisha uhamisho wa Onana, kitu ambacho walikikamilisha - lakini De Gea bado hana timu na sasa huenda akarudi Old Trafford itakapofika Januari. Kwenye dirisha lililopita, Man United ilimsajili kipa Altay Bayindir kutoka Fenerbahce kwa ada ya Pauni 4.3 milioni, lakini Tom Heaton ndiye kipa ambaye angebaki mwenye uzoefu kidogo kwenye kikosi cha Man United michuano ya Afcon itakapoanza Januari.

Na sasa, wakati Man United ikifikiria kumrudisha De Gea kufanya mambo Old Trafford, hii hapa orodha ya mastaa kibao waliowahi kurudishwa kuzitumikia klabu zao za zamani, huku miamba hiyo inayonolewa na Mdachi Erik ten Hag ikiwa na mfano hai baada ya kuwarudisha kwenye vikosi vyao Paul Pogba, Cristiano Ronaldo na msimu huu, beki Jonny Evans.

Romelu Lukaku - Chelsea Awamu ya kwanza: 2011-2014 Awamu ya pili: 2021-hadi sasa

Straika Romelu Lukaku aliondoka Stamford Bridge mwaka 2014 akiwa hajapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ambapo alipelekwa kwa mkopo timu mbili tofauti, West Brom na Everton. Baada ya kujiunga jumla na Everton, ambapo alitamba sana na mwaka 2017, Chelsea ilitaka kumrudisha, lakini akachagua kwenda Man United. Miaka miwili baadaye, Lukaku aliondoka Man Unitd kwenda Inter Milan, mahali ambako alionyesha ubora mkubwa wa soka lake na kuwafanya Chelsea kumrudisha kwenye kikosi kwa uhamisho wa pesa nyingi, Pauni 97.5 milioni kwenye majira ya kiangazi 2021. Licha ya kufunga kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Arsenal, Lukaku akatibuana na Kocha Thomas Tuchel akakosa nafasi na matokeo yake akaamua kuondoka tena Chelsea, ambapo kwa sasa anacheza kwa mkopo AS Roma.

Didier Drogba - Chelsea Awamu ya kwanza: 2004-2012 Awamu ya pili: 2014-2015

Bila ubishi ni straika bora kabisa wa Chelsea kuwahi kutokea kwenye zama za Ligi Kuu England. Drogba alishinda mataji 10 katika awamu yake ya kwanza aliyokuwa na miamba hiyo ya Stamford Bridge. Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast alishinda Ligi Kuu England mara tatu na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja katika kipindi chake cha miaka minane aliyokuwa Chelsea katika awamu yake ya kwanza. Baada ya miaka miwili ya kuwa mbali na Chelsea, alipokwenda kucheza Shanghai Shenhua na Galatasaray - Drogba alirejea tena The Blues kwenda kucheza chini ya Jose Mourinho mwaka 2014 na kuisaidia timu hiyo kushinda tena ubingwa wa Ligi Kuu England huku akitengeneza jina lake na kuwa gwiji Stamford Bridge. Kwa awamu zote mbili za Drogba kwenye kikosi cha Chelsea, amekuwa mtu wa mafanikio.

Thierry Henry - Arsenal Awamu ya  wanza: 1999-2007 Awamu ya pili: 2012 (mkopo)

Staa mwingine aliyekuwa straika wa maana kwelikweli kwenye Ligi Kuu England ni Thierry Henry, aliyefanya makubwa Arsenal. Mkali huyo wa zamani wa Ufaransa baada ya kutamba kwa miaka minane kwenye kikosi cha Arsenal na kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, ikiwamo lila la msimu wa 2003-04, ambapo Arsenal ilicheza bila ya kupoteza mechi, naye aliondoka na kurudi tena. Henry alienda Barcelona mwaka 2007 kisha baada ya miaka michache akatimkia zake York Red Bulls, ambako iliaminika anakwenda kumalizia maisha yake ya soka. Lakini, mwaka 2012, Henry aliduwaza wengi baada ya kurudi kwa mkopo wa miezi miwili Arsenal, kuziba pengo la washambuliaji Marouane Chamackh na Gervinho waliokuwa majeruhi. Henry alifunga mabao kadhaa kwenye awamu yake ya pili na kuipa Arsenal ushindi.

Robbie Fowler - Liverpool Awamu ya kwanza: 1993-2001 Awamu ya pili: 2006-2007

Mashabiki wa Liverpool walimwabudu kama mungu wao, lakini hilo linatosha kusema kwamba supastaa Fowler alipendwa sana na mashabiki hao wa Merseyside. Lakini, alivunja mioyo ya mashabiki hao wakati alipoondoka kwenda Leeds United mwaka 2001, mahali ambako alitumika kwa miaka miwili kabla ya kwenda zake kujiunga na Manchester City. Baada ya kutemwa na Man City mwaka 2006 kutokana na kupata majeraha na kushuka kiwango, Fowler alirudi zake Anfield na kuonyesha makali makubwa ikiwamo kufunga mabao 12 akiwa na kikosi cha Liverpool, ikiwamo mabao manane aliyofunga kwenye Ligi Kuu England.

Gareth Bale - Tottenham Awamu ya kwanza: 2007-2013 Awamu ya pili: 2020-2021

Bale alijitambulisha vyema kwenye dunia ya soka wakati akiwa zake White Hart Lane kabla ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani aliponaswa na Real Madrid. Baada ya mafanikio makubwa akiwa na Los Blancos, mkali huyo wa kimataifa wa Wales alijikuta akiwa kwenye hali mbaya chini ya Kocha Zinedine Zidane na hivyo kujikuta akiwekwa tu benchi. Kutokana na hilo, Bale alirudi zake Tottenhma kwa mkopo, lakini nako alikumbana na wakati mgumu kwa kukosa nafasi za kutosha za kucheza chini ya Kocha Jose Mourinho. Alifanikiwa kufunga mabao 16 kwenye kikosi cha Spurs katika awamu yake hiyo ya pili kabla ya kurudi zake Hispania msimu ulipofika ukingoni.

Wayne Rooney - Everton Awamu ya kwanza: 2002-2004Awamu ya pili: 2017-2018

Rooney alitambulisha uwepo wake kwenye soka baada ya kufunga bao matata dhidi ya Arsenal mwaka 2002 wakati huo alipokuwa Everton na hapo Man United ilipomwona na kwenda kufukuzia saini yake. Baada ya hapo, mkali huyo alitua zake Man United na kuitumikia miamba hiyo ya Old Trafford kwa miaka 13, akishinda mataji matano ya Ligi Kuu Englad na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kurudi kujiunga na klabu yake ya zamani, Everton. Rooney alikwenda kuwa kinara wa mabao wa Everton kwa msimu wake mmoja aliorejea Goodison Park, baada ya hapo aliondoka kwenda kujiunga na DC United ya Marekani mwaka 2018, mahali ambako alikomesha maisha yake ya uchezaji na kutua zake Derby alikokwenda kuwa kocha.

Sol Campbell - Arsenal Awamu ya kwanza: 2001-2006 Awamu ya pili: 2010

Beki Sol Campbell alishtua wengi huko London mwaka 2001 alipoamua kujinga na Arsenal akitokea kwa mahasimu wao Tottenham. Baada ya miaka mitano ya kuwa kwenye klabu hiyo, beki huyo wa zamani wa England alikwenda Portsmouth na kuichezea kwa miaka mitatu na kisha akaenda Notts County - katika miaka yake ya mwisho ya soka. Lakini, Campbell alishtua tena watu baada ya kurudi kuitumikia Arsenal katika msimu wa 2009-10 na kuitumikia timu hiyo katika mechi 14 kabla ya kwenda Newcastle United, mahali ambako baadaye alistaafu soka lake.

Paul Pogba - Man United Awamu ya kwanza: 2009-2012 Awamu ya pili: 2016-2022

Pogba alicheza mechi saba tu katika kikosi cha kwanza katika awamu yake ya kwanza Man United ambapo aliibuka kutokea kwenye timu ya vijana. Akiwa na umri wa miaka 19, kiungo huyo Mfaransa aliondoka Man United na kwenda kujiunga na Juventus, mahali ambako alitengeneza jina lake na kuwa mmoja kati ya viungo matata kabisa wa kati waliowahi kutokea kwenye soka.

Mwaka 2016, Man United ilirudi kwa Pogba na kutoa pesa nyingi, Pauni 89 milioni, uhamisho uliovunja rekodi ya dunia kwa kipindi hicho ili kumrudisha Pogba Old Trafford. Pogba, alirudi Man United na baada ya miaka kadhaa kwenye kikosi hicho, staa huyo aliamua kurudi tena Juventus na tangu atue kwenye timu hiyo mambo yake yamekuwa ya hovyo sana.

Jermain Defoe - Tottenham Awamu ya kwanza: 2004-2008 Awamu ya pili: 2009-2014

Katika awamu yake ya kwanza Spurs - ikiwa imemsajili kutoka West Ham - Defoe alikuwa panga pangua chaguo la kwanza kwenye Timu ya Taifa ya England. Lakini, mwaka 2008, Tottenham iliamua kumuuza wakati Kocha Harry Redknapp alipohitaji huduma yake huko Portsmouth. Baada ya msimu mmoja, Redknapp akienda kuinoa Spurs - alilipa mara mbili ya kiasi ambacho Pompey ililipa miezi 12 iliyopita ili kunasa saini ya mchezaji huyo. Defoe alirudi White Hart Lane na kucheza kwa miaka mitano na kufunga mabao 79 na kumaliza maisha yake kwenye kikosi hicho akiwa mchezaji anayeshika namba sita kwa mabao katika kikosi cha Spurs kwenye orodha ya wafungaji wa muda wote.

Nemanja Matic - Chelsea Awamu ya kwanza: 2009-2011 Awamu ya pili: 2014-2017

Chelsea ilimsajili kiungo wa Serbia, Nemanja Matic kwa ada ya Pauni 1.5 milioni mwaka 2009. Lakini, staa huyo alicheza mechi tatu tu kwenye kikosi cha kwanza na kutolewa kwa mkopo Vitesse Arnhem  kisha akauzwa Benfica. Baada ya miaka mitatu mitamu huko Ureno, Chelsea ilivutiwa na huduma yake na kumrudisha Pauni 21 milioni. Matic aliisaidia Chelsea kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England kabla ya kuipa timu hiyo faida ya karibu Pauni 20 milioni alipojiunga na Man United mwaka 2017.

Wachezaji wengine

Mastaa wengine ni Mbrazili, Juninho, aliyechezea Middlesbrough kwa awamu mbili. Angel Di Maria (Benfica), Shinji Kagawa (Borussia Dortmund), Peter Crouch (Portsmouth), Carlos Tevez (Boca Juniors), Mathieu Flamini (Arsenal), Joe Cole (West Ham),  Claudio Pizarro (Werder Bremen), Kaka (AC Milan), Mario Gotze (Borussia Dortmund), Mats Hummels (Borussia Dortmund).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live