Mkalimani wa zamani wa timu ya Taifa ya Spain, Alex Pena katika michuano ya Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi, anadai kuwa mastaa kama David de Gea, Dani Carvajal na Nacho Monreal wote walikuwa wakitoka nje ya hoteli wakati wa Kombe la Dunia wakitafuta wanawake.
Pena amesema pia aliwahi kuingia kwenye chumba cha baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, akaona chupa za pombe na sigara zikiwa zimezagaa vyumbani mwao.
Pia Pena amemsifu kiungo Andres Iniesta, ambaye alikuwa mpole na mwenye nidhamu ya hali ya juu.
Carvajal amejibu madai hayo: “Taarifa zote zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari siku za hivi Karibuni zinazonihusu ni za uongo kabisa. Kuanzia ushiriki wangu katika vyama vya kisiasa hadi unyanyasaji wa kijinsia kwenye Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi.
"Vyombo vya habari vinajiona vina haki ya kuandika bila kuadhibiwa, wameutoa uaminifu wangu kwa watu kutokana na maneno yao. Wamechafua jina na heshima yangu. Wakae wakijua kuwa tayari nimeshachukua hatua za kisheria.”
Hadi sasa Carvajal ndiye mchezaji pekee aliyezungumzia sakata hilo. Kwa mujibu wa ripoti mbali mbali kutoka Spain zimeeleza kuwa, Carvajal ameanza kuzungumzwa baada ya kauli yake ya kusema hawezi kumhukumu aliyekuwa Rais wa RFEF Luis Rubiales ambaye alifanya makosa ya unyanyasaji wa kingono kwa mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Spain, Jenni Hermoso hadi atakapokutwa na hatia baada ya kufanyika kwa uchunguzi wenye uhakika.