Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Darasani Pacome, Chama nani mwalimu?

Pacome Zouzoua Nov.jpeg Darasani Pacome, Chama nani mwalimu?

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya vitu vya kujivunia kwenye ligi yetu, ni kuona wimbi la wachezaji wa kigeni wenye ubora wanazidi kumiminika. Kama wewe ni mtu wa burudani, bila shaka yoyote Pacôme Zouzoua wa Yanga atakuwa anaukosha sana moyo wako.

Jamaa ni fundi bwana! Jamaa ana mwendo bwana! Akili nyingi sana zinahitaji kumkaba. Kama wewe ni mpenzi wa akili ya mpira, Clatous Chota Chama atakuwa anakupa burudani ya kutosha. Miguu ya Chama inaweza kuwa na akili nyingi sana kuliko vichwa vya wachezaji wengi. Kwa miaka ya hivi karibuni, sijawahi kumwona mtu mwenye akili ya boli kama huyu jamaa.

Ni kama mpira unaufanya anachotaka. Ni kama mpira muda wote unasubiri amri yake! Mchezo wa soka ni mchezo wa wazi. Hawa ni wachezaji pekee kwenye ligi yetu wenye ufundi mwingi mguuni. Kila mtu kuna namna anavyoweza kuwalinganisha na kuwatofautisha.

Ni fahari sana kuwaona wachezaji wenye ubora huu wote wako kwenye Ligi ya NBC. Kilikuwa ni kilio cha miaka mingi kupata wachezaji wa nje wanaoleta tofauti uwanjani. Je, Pacome ni Mwanafunzi wa Chama au Chama ndiyo mwanafunzi wa Pacome?

Pengine ni kwa sababu nimemtazama Chama kwa miaka mingi. Pengine nimemuona Chama kwenye mechi nyingi dume akiziamua. Namuona Chama kwenye picha nyingi zaidi.

Pacome ndiyo kwanza mpya. Mbichi kabisa kwenye makaratasi yake. Msimu wa kwanza Tanzania, lakini tayari ameshawalaza watu wetu chali. Ana spidi ya hatari akiwa na mpira. Pasi maridadi sana akielekea kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji.

Ni Mwamba kweli kweli lakini nadhani bado tunahitaji muda kuburudika. Chama anaonekana spidi kidogo miguu iko chini lakini akili yake inakimbia balaa.

Utulivu wa hali ya juu sana anapokuwa na mpira na namba zinambeba. Nadhani moja kati ya eneo ambalo Pacome anapaswa kuimarika zaidi ni upande wa namba. Chama ni mchezaji anayekupa uhakika wa walau mabao 10 na pasi 10 za mabao kila msimu.

Amefanya hivyo mara nyingi tu. Amefunga mabao mengi sana yaliyoipeleka Simba mbele. Pacome bado eneo hili hajakuwa na takwimu nzuri sana. Pengine bado ni mapema. Pengine ndiko anakokwenda.

Hawa ndiyo aina ya wachezaji tunaowahitaji kwenye ligi yetu. Najua mpira ni mchezo wa wazi na hata wewe umewafuatilia vizuri wachezaji hawa. Natamani sana kupata maoni yako juu ya ubora wao.

Chama amekuwa mfalme pale Simba kwa miaka mingi sana na ameweka gepu kubwa sana baina yake na wachezaji wengine. Pacome ana kazı kubwa sana pale Yanga. Baada ya Fiston Mayele kuondoka, Yanga imebaki bila mfalme.

Wachezaji wengi wanaonekana kuwa kwenye daraja moja. Kinachoweza kumpambanua na wengine ni kuamua mechi kubwa na kutengeneza namba za kutosha. Ukitazama umri, unaona Pacome ana faida. Bado anaonekana ni mdogo kwa Chama.

Miaka 26 aliyonayo, inampa uhakika walau wa kucheza kwenye kiwango cha juu kwa miaka mitano yote ijayo. Chama simuoni akifika huko. Tayari anaelekea maji ya jioni. Akiwa na miaka 32, sioni tena Chama akiendelea kutamba kwa muda mrefu.

Wakati mwingine ni kazi sana kulinganisha wachezaji kama hawa lakini soka ni michezo wa maoni. Pacome ana mwendo sana kuliko Chama. Haina ubishi. Anapotaka kutengeneza nafasi, spidi yake huwa ni ya hatari sana.

Sidhani kama Mwamba wa Lusaka anaogelea kwenye maji haya. Lakini, haiondoi ukweli pia, linapokuja suala la maamuzi ndani ya 18, Chama ni habari nyingine kabisa.

Eneo ambalo wachezaji wengi huchanganyikiwa ndiyo mara zote Chama anakufurahisha. Ni fahari sana kuwaona hawa wachezaji wote uwanjani. Ni faraja zaidi kuwaona kwenye ligi yetu.

Je, Mwamba wa Lusaka ndiye mwalimu wa Pacome? Majibu ni ndiyo na Sio. Nadhani yote ni Majibu sahihi. Kwenye ulimwengu wa soka, mashabiki wanapenda sana washambuliaji. Hawa ndio huwapa furaha ya kudumu. Ukiona kiungo au mlinzi anakuwa mfalme wa timu, ujue huyo mtu ni balaa. Haitokei mara kwa mara.

Haitokei kwa kila mchezaji. Ukiona Chama anaimbwa kwa miaka mingi, haiji kwa bahati mbaya. Pale Simba katika miaka mitano ya hivi karibuni, wamepita washambuliaji kibao lakini hakuna aliyefunika jina la Chama.

Pacome amekuta Yanga hakuna mshambuliaji mbeba timu. Wote wanaomba Mungu tu. Walau Clement Mzize anaanza kujipata. Kuanza kuimbwa jina lake sio kwa bahati mbaya. Ni umaridadi wa miguu yake. Njia ya kwenye ufalme wa Jangwani ni ngumu. Inahitaji kazi kubwa sana aifanye.

Yule Max Nzengeli ni kama amepoa kidogo lakini ni mtu na nusu. Aziz Ki ndiyo habari nyingine pale Jangwani. Kwa umri wake Kiafrika, bado ana muda sana wa kufanya makubwa. Nafurahia kuwaona wachezaji wenye ubora huu kwenye ligi yetu.

Nafurahi kumwona Chama. Nafurahi kumwona Pacome. Nadhani ni kwa sababu nimemwona Chama kwa miaka mingi, akiamua mechi nyingi dume za Simba. Namwona kama yuko mbele kidogo ya Pacome. Labda tukimpa walau misimu miwili Pacome anaweza kutupa kitu cha tofuati.

Najua na wewe unawafuatilia hawa wachezaji. Najua unafurahia wanachofanya. Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya simu hapo juu.

Hawa ndiyo aina ya wachezaji wa Kigeni tunaowahitaji kwenye ligi yetu. Wanaongeza thamani ya ligi yetu na kuleta ushindani kwa wachezaji wetu wazawa. Je, Pacome ni mwanafunzi wa Chama au Chama ndiyo mwanafunzi wa Pacome?

Chanzo: Mwanaspoti