Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dani Olmo atajwa kuwa mbadala wa De Bruyne

Dani Olmo To City Dani Olmo

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuona kuna uwezekano mkubwa kiungo Kevin de Bruyne akaondoka katika dirisha hili au lijalo kutokana na ofa kubwa zilizowekwa mezani na timu za Saudi Arabia, Manchester City imeanza mazungumzo na RB Leipzig ili kuipata saini ya kiungo wa timu hiyo na Hispania, Dani Olmo, 26.

Staa huyo aliyekuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kilichochukua ubingwa wa Euro mwaka huu nchini Ujerumani ana kipengele kinachotaka timu inayomtaka kutoa Pauni 50 milioni ili kuvunja mkataba.

Kipengele hicho kilikuwa kinaisha mwisho wa wiki iliyopita, lakini kutokana na majukumu timu ya Hispania kiliongezwa muda na sasa kitafikia ukomo mwisho wa wiki hii na kuanzia hapo timu itakayomtaka itatakiwa kujadiliana bei na Leipzig.

Akiwa na Leipzig msimu uliopita Olmo alisumbuliwa sana na majeraha kiasi cha kucheza mechi 25 za michuano yote, akafunga mabao manane na kutoa asisti tano.

Man City itatakiwa kushinda vita kwanza dhidi ya majirani zao, Manchester United ili kumpata Olmo ambaye mkataba wake unamalizika 2027.

Wakati huo huo, Liverpool imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wa beki wa Crystal Palace, Marc Guehi kwa ajili ya kuipata saini yake katika dirisha hili baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha tangu msimu uliopita. Hata hivyo, Palace imeonyesha kutokuwa na nia ya kumuuza Guehi kwa sababu imeshamtoa Michael Olise na inaona akiondoka na timu itakuwa na wakati mgumu zaidi.

CHELSEA imefikia hatua nzuri katika mazungumzo yao na Borussia Dortmund kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo Karim Adeyemi, 22, katika dirisha hili. Adeyemi ambaye msimu uliopita alifunga mabao matano katika mechi 34 za michuano yote mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2025.

ARSENAL imefikia makubaliano na Ajax ili kumsajili kipa wa timu hiyo, Tommy Setford, 18, katika dirisha hili ili kuboresha eneo lao la ulinzi. Taarifa zinaeleza Arsenal imekubali kulipa kiasi kisichopungua Euro 400,000 ili kufanikisha dili la kumnasa staa huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.

WOLVES inaongoza katika mchakato wa kuwania saini ya beki wa Sheffield United, Anel Ahmedhodzic, 25, ili kuziba pengo lililoachwa na Max Kilman, 27, aliyejiunga na West Ham United. Taarifa zinaeleza Wolves ipo tayari kutoa Pauni 20 milioni kwa ajili ya kufanikisha dili hilo. Mkataba wa beki huyu unatarajiwa kumalizika 2026.

MIKEL Arteta ameendelea kuwasisitizia mabosi wa Arsenal kuwa anahitaji saini ya kipa wa Espanyol Joan Garcia, ambaye ana mkataba na timu yake hadi 2028. Inaelezwa kiasi cha Pauni 21 milioni ndio kinachoweza kutumika kumuondoa kipa huyo kutoka Hispania kwenda England. Katika msimu uliopita Garcia alicheza mechi 46 za michuano yote.

BEKI wa Atalanta United ya Marekani Caleb Wiley anatarajiwa kufanya vipimo vya afya nchini humo kabla ya kukamilisha dili la kujiunga na Chelsea katika dirisha katika dili ambalo litaigharimu timu hiyo Pauni 8.5 milioni. Chelsea haijapanga kumtumia Wiley msimu ujao na badala yake itamtoa kwa mkopo kwenda Strasbourg.

ARSENAL ina nafasi kubwa ya kuipiku Aston Villa katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa Real Sociedad na Hispania Mikel Merino, 28, ambaye amezivutia timu nyingi baada ya kiwango bora alichoonyesha katika Euro mwaka huu. Merino ambaye mkataba wake na Sociedad unamalizika 2025. katika Euro alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao manane.

Chanzo: Mwanaspoti