Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dalali atoa ujumbe mzito Simba, mastaa wamwaga machozi

Dalali Katiba Dalali atoa ujumbe mzito Simba, mastaa wamwaga machozi

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, ameuomba uongozi wa timu hiyo chini ya Murtaza Magungu (Mwenyekiti), kuyaweka pamoja makundi ambayo yalijitokeza wakati wa uchaguzi.

Hivi karibuni Simba walifanya uchaguzi uliomrudisha madarakani Magungu na inaelezwa kuwa baada ya uchaguzi huo kumekuwa na makundi mbalimbali ambayo kama hayatawekwa sawa, basi timu hiyo inaweza kuadhirika.

Dalali alijitolea mfano wakati anaingia madarakani kwamba yalijitokeza makundi saba ambayo yalikuwa yanampinga, lakini baada ya kupata dhamana ya uenyekiti aliitisha mkutano makao makuu ya klabu kwa lengo la kuyajenga.

Alitumia uzoefu wake kwamba kuwepo upinzani kwenye uchaguzi ni jambo la kawaida, lakini viongozi wanaopita ni jukumu lao kuwaweka watu pamoja ili kuhakikisha kila mmoja anajisikia ni sehemu ya timu.

“Binafsi baada ya uchaguzi kila kitu nilikiweka kando, naipenda Simba natamani ifanye makubwa, siwezi kuchochea makundi ndani ya klabu na kama wanaofanya hivyo wanafanya kwa faida ipi! Alihoji.

“Japokuwa baada ya uchaguzi Magungu alisema uchaguzi umepita sasa tujenge Simba moja, ila ni bora angeitisha mkutano ili kujadili mambo mbalimbali ya afya kwa klabu, kwani atapata picha nzima ya mitazamo ya watu anaowaongoza.”

Mbali na hilo, alisema Simba kufungwa na Horoya na Raja Casablanca hakumaanishi ndio mwisho wa safari, badala yake aliwataka wachezaji kutokukubali kukata tamaa.

“Naamini Simba inaweza ikafika robo fainali, isipokuwa ni wachezaji wenyewe waamke na wasikubali kushindwa kutokana na presha ya mashabiki, kufungwa ni jambo la kawaida ndio maana kuna matokeo matatu ingawa hilo la kufungwa ndilo linaloumiza zaidi,” alisema.

Wakati Dalali akisema hayo juzi baadhi ya mastaa walimwaga machozi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam wakionekana kujutia matokeo hayo.

Chanzo: Mwanaspoti