Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari Yanga awapa Wananchi matumaini majeraha ya Aucho

Aucho Aanza Tizi Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho Jumatatu anaanza mazoezi mepesi tayari kwaajili ya kujiweka fiti kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini Machi 30.

Kwa mujibu wa daktari ya Yanga, Moses Etutu, mchezaji huyo anaendelea vizuri tofauti na matarajio yao huku akiweka wazi kuwa ni kutokana na namna ya kiungo huyo alivyo na fikra chanya kwenye mapokeo ya ugonjwa.

"Baada ya vipimo na kufanyiwa upasuaji huo mdogo tulitenga vipindi vitatu vya mazoezi, tumebaini anaimarika haraka sana tofauti na matarajio. Alianza na namna ya kufanya mazoezi ya miondoko, haijamchukua muda amekuwa imara eneo hilo," alisema na kuongeza;

"Hatua ya pili inayofuata ni wiki ijayo kuanzia Jumatatu anaanza mazoezi mepesi akiwa mwenyewe kabla ya kuungana na wenzake kuanzia wiki ijayo kwaajili ya mazoezi magumu tayari kwa mchezo."

Alisema kutokana na kasi aliyonayo ya kufanya vitu kwa uharaka anaweza akarudi uwanjani tofauti na wao walivyokuwa wanapanga kumuona akirudi.

Wakati huo huo, ameweka wazi taarifa ya beki Kibwana Shomari ambaye alipata shida kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold timu yake ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Alisema baada ya vipimo wamebaini beki huyo amepata shida ya enka kwenye mguu wake wa kulia tatizo ambalo linaweza kumuweka nje ya uwanja kwa wiki mbili na zaidi.

"Kibwana tumemfanyia vipimo na kubaini shida hiyo, lakini kutokana na utaratibu tulionao sasa naamini anaweza akarudi mapema zaidi kuendelea kuipambania timu, itategemea na mapokeo yake," alisema na kuongeza;

"Ugonjwa wowote unapona haraka kutokana na namna mgojwa anavyoupokea. Ukiangalia Aucho hakuna aliyetarajia kumuona anaimarika kwa kasi hivi, ni mchezaji ambaye anaipenda kazi yake kila alichoelekezwa kufanya anafanya kwa usahihi, ndio maana unaona anarudi kwa nguvu na uharaka."

Etutu alisema ili kuwaweka wachezaji hao katika hali nzuri na kutokurudi kwenye shida ya kupata majeraha kwa uharaka watalazimika kuwapeleka kwa kocha wa utimamu wa mwili (fitness coach) ili kuwarudisha taratibu kabla hawajacheza mechi za mashindano.

Aucho alifanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni na madaktari walimkadiria kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu lakini Jumatatu anaanza mazoezi mepesi hivyo kocha na mashabiki wa Yanga watarajie kumuona uwanjani kiungo huyo hivi karibuni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: