Daktari wa Simba, Edwin Kagabo ameshusha presha kuwa wana matumaini makubwa Aishi Manula atarejea uwanjani mapema mara baada ya matibabu hayo.
Manula na Daktari huyo wapo Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, baada ya Uongozi wa Simba SC kufanya maamuzi hayo ya haraka kwa kuhakikisha Mlinda Lango huyo anakuwa sawa na kurejea katika majukumu yake kikosini.
Akiwa Afrika Kusini Manula atafanyiwa upasuaji kufuatia majeraha ya nyama za paja ambayo yamemuweka nje kwa zaidi ya miezi miwili sasa, akikosa michezo saba mfululizo iliyopita ya Simba SC.
Manula alipata majeraha hayo katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Ihefu FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Aprili 7, mwaka huu.
Akizungumzia utaratibu wa upasuaji huo Daktari Kagabo amesema: “Tumewasili Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya mlinda mlango wetu Aishi Manula ambaye alipata majeraha ya nyama za paja kwenye mchezo dhidi ya Ihefu na baada ya vipimo ilionekana anahitaji upasuaji.
“Kumekuwa na hofu juu ya muda gani ambao atakuwa nje ya uwanja, lakini niwatoe hofu kuwa tunatarajia atarejea uwanjani mapema baada ya matibabu licha ya kwamba hatuwezi kukadiria muda sahihi atakaokuwa nje ya uwanja mpaka pale upasuaji utakapomalizika.”