Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua kwa mara ya kwanza ameonekana akiwa mazoezini baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda, lakini daktari amesema alipaswa kuwa nje kwa siku 28.
Pacome mara ya mwisho kucheza akiwa na kikosi cha Yanga ni kwenye mchezo dhidi ya Azam FC timu yake ikikubali kichapo cha mabao 2-1 katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambao ulipigwa Machi 17, mwaka huu.
Kiungo huyo hakumaliza mchezo huo baada ya kuumia na ripoti yake ilitolewa kuwa ameumia kifundo cha mguu.
Mwanaspoti imefanya mahojiano na madaktari aliyeweka wazi kuwa kifundo cha mguu kinaweza kumuweka nje mchezaji kuanzia wiki moja hadi siku 28.
Daktari huyo wa Tabora United, Abel Shindika amesema kifundo cha mguu 'enka' kina shida mbili tofauti, hivyo inategemea Pacome alipata ya aina gani.
"Kifundo cha mguu kina maumivu mawili akiteguka eneo la kifundo cha mguu na pia kifundo kina mshipa unaweza ukachomoka na kwenda njia ambazo sio sahihi. Hili ndio jeraha la kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu," amesema.
"Mfano mchezaji akipata shida ya kifundo cha mguu kwa kuteguka anaweza kukaa nje wiki moja hadi mbili lakini mfupa ukitoka nje anaweza kukaa nje hadi siku 28 na zaidi kama atafuata masharti ya daktari."
Ameongeza kuwa, "mchezaji aliyeumia kifundo cha mguu anatakiwa kuzingatia utulivu ili kutouchezesha mguu mara kwa mara hasa akizingatia miundombinu ya nchi yetu anaweza kutonesha."
Shindika amesema mchezaji akizingatia kwa kuutuliza mguu wake eneo moja na kuufunga alilopata shida hawezi kuchukua muda mrefu kupona.
MECHI NNE KABLA YA JERAHA Pacome kabla ya kuumia kwenye mechi nne alizocheza Yanga imefunga mabao 10, huku kati ya mabao hayo amefunga moja kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Ihefu SC.
Pia alitoa pasi iliyozaa bao kwenye mchezo huo akimpasia Aziz Ki, mabao mengine yakifungwa na Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli na Augustin Okrah asisti zikitoka kwa Aziz Ki na moja alitoa Joseph Guede.
Mchezo dhidi ya Azam FC ambao walifungwa mabao 2-1 alifunga Clement Mzize bao la kufutia machozi akipokea pasi kutoka kwa Aziz Ki mabao ya Azam yalifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' na Kipre Jr.
Mechi nyingine aliyocheza kabla ya kuumia ni dhidi ya Namungo wakishinda mabao 3-1 yote walifunga Yanga baada ya Ibrahim Hamad 'Bacca' kujifunga na mengine yalifungwa na Aziz Ki, Mzize na Mudathir.
Na mchezo wa nne ulikuwa ni dhidi ya Geita Gold wakishinda bao 1-0 likifungwa na Aziz Ki akipokea pasi kutoka kwa Okrah.
NNE BAADA YA KUUMIA Pacome baada ya kuumia Yanga imecheza mechi nne mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns wakitolewa hatua ya robo fainali baada ya suluhu michezo yote miwili nyumbani na ugenini na kutolewa kwa penalti 3-2.
Baada ya hapo Yanga walicheza mchezo wa hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho 'FA' dhidi ya Dodoma Jiji wakishinda mabao 2-0 moja likifungwa na Mzize na jingine Dodoma walijifunga.
Pia walicheza mchezo wa ligi dhidi ya Singida Fountain Gate, Yanga wakishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na Guede akiingia kambani mara mbili na moja likifungwa na Aziz Ki.