Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika za majeruhi dirisha la usajili Ulaya

Mechi Kali EPL Dakika za majeruhi dirisha la usajili Ulaya

Wed, 28 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Muda unakwenda kasi sana. Dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi huko Ulaya linafungwa wiki hii, Ijumaa saa 5:00 usiku kwa saa za Uingereza.

Klabu kadhaa za Ligi Kuu England bado zipo kwenye mazungumzo ya kunasa dili za mastaa wapya, huku nyingine zikipaswa kuuza wakali wake.

Miamba kama Arsenal, Manchester United na Chelsea inatarajia kuwa bize ndani ya wiki hii kuhakikisha kuna wachezaji wananaswa na wengine wanauzwa kabla ya dirisha hili halijafungwa.

Hii hapa orodha ya mastaa 11 ambao wanaweza kubadili timu muda wowote kabla ya dirisha halijafungwa keshokutwa, Ijumaa.

1. Mikel Merino; Bado hajatambulishwa rasmi kuwa staa mpya wa Arsenal. Miamba hiyo ya Emirates imekuwa kwenye mazungumzo na kiungo huyo wa Real Sociedad kwa wiki kadhaa sasa na kinachoelezwa, Arsenal imeshakubali kulipa Pauni 33 milioni kumsajili. Taarifa zilifichua, tayari Merino yupo London na muda wowote anaweza kutangazwa kuwa staa mpya wa Washika Mitutu hao wa London wanaonolewa na Mikel Arteta.

2. Kepa Arrizabalaga; Kipa huyo haonekani kuwa na nafasi kwenye kikosi cha Chelsea msimu huu. Ameshapoteza namba kwenye kikosi cha kwanza na kocha Enzo Maresca amekuwa wazi kabisa, mchezaji ambaye haoni kama atamtumia, amekuwa akifanya mazoezi kivyake. Kutokana na hilo, kuna uwezekano mkubwa Kepa akabadili timu kabla ya dirisha halijafungwa Ijumaa, huku Bournemouth ikiripotiwa kutaka huduma yake.

3. Raheem Sterling; Kocha mpya wa Chelsea, Enzo Maresca amemwambia wazi Sterling hatakuwa na nafasi ya kucheza msimu huu. Winga huyo alienguliwa kwenye kikosi na amekuwa akifanya mazoezi kivyake kama ilivyo kwa Kepa. Na mbaya zaidi, Sterling amevuliwa hadi namba yake ya jezi na kupewa mchezaji mpya wa kikosi hicho aliyenaswa kwenye dirisha hili, Pedro Neto. Kuna timu kibao zinamtaka Sterling.

4. Jadon Sancho; Ingawa ilionekana kama amejenga upya uhusiano wake na kocha Erik ten Hag baada ya kutibuana hadharani msimu uliopita, Sancho bado hajacheza mechi yoyote kati ya mbili ilizocheza timu yake ya Manchester United kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Na kinachoelezwa ni kwamba Sancho atakuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi, hilo linamweka kwenye nafasi kubwa ya kuhama wiki hii.

5. Ivan Toney; Kama ilivyo kwa Sancho na Sterling, straika Toney bado hajacheza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Wakati Brentford ilipokuwa ikijiandaa na mechi ya Crystal Palace, kocha Thomas Frank alifichua kukosekana kwa straika huyo kwenye kikosi kunatokana na ishu ya uwezekano wa kubadili timu kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa.

6. Victor Osimhen; Straika, Osimhen amejipambanua na kujiweka kwenye kundi la mastraika wa moto kabisa Ulaya kwa sasa. Klabu kadhaa zilionyesha dhamira ya kunasa saini yake ikiwamo Arsenal, Man United na Chelsea. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca aliweka wazi kwamba atafurahi kama atasajili straika mpya kabla ya dirisha kufungwa jambo linaloweka uwezekano wa Mnigeria huyo kutua Stamford Bridge.

7. Marc Guehi; Newcastle United imeripotiwa kufukuzia huduma ya beki wa kati wa Crystal Palace, Guehi kwa wiki kadhaa sasa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Ofa zao nne zimekataliwa, lakini bado wana matumaini ya kumnasa kabla ya dirisha halijafungwa Ijumaa. Lakini, Palace yenyewe inataka Pauni 70 milioni kwenye mauzo ya Guehi, ambaye alifanya vizuri sana kwenye Euro 2024 akiwa na England.

8. Jarrad Branthwaite; Beki huyo wa Everton amekuwa akihusishwa sana mpango wa kuachana na maisha ya Goodison Park kwa miezi ya karibuni. Man United ilipeleka ofa mbili na zote zilikataliwa na moja ya ofa hizo ilikuwa ya Pauni 35 milioni. Lakini, Liverpool na Newcastle zinaamini zinaweza kumnasa kabla ya dirisha kufungwa, huku Everton ikiwa tayari kumuuza mchezaji huyo ili kujiweka sawa kwenye bajeti yao.

9. Scott McTominay; Napoli imekubali kumsajili McTominay kwa ada ya Pauni 25 milioni na huenda dili hilo likakamilika kabla ya dirisha kufungwa. Kiungo huyo awali alihusishwa na klabu za Fulham, Galatasaray na West Ham, lakini timu zote hizo zilishindwa kulipa pesa inayotaka Man United.

10. Manuel Ugarte; Man United itakapokamilisha mauzo ya McTominay, itatua rasmi kwa kiungo Ugarte na kuhakikisha inapata saini yake kutoka Paris Saint-Germain kabla ya dirisha kufungwa. Ripoti zilifichua kwamba staa huyo alitarajia kutua Manchester jana Jumanne, huku ada yake inaweza kuigharimu Man United, Pauni 51 milioni.

11. Frenkie de Jong; Barcelona inakimbizana na muda juu ya kuwafungulia mlango wa kutokea baadhi ya mastaa wake kabla ya dirisha kufungwa ili kupata nafasi ya kumwandikisha kwenye kikosi nyota wao mpya, Dani Olmo. De Jong anaweza kuwa mmoja wa wachezaji watakaofunguliwa mlango wa kutokea na anaweza kunaswa na Man United endapo kama watakwama kwenye dili lao la kumchukua Ugarte.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live