Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika tishio mechi ya watani

Simba Vs Yanga Mkwakwani Dakika tishio mechi ya watani

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Takwimu za mechi zilizopita za Ligi Kuu msimu huu, zinailazimisha safu ya ulinzi ya Simba kuwa makini zaidi katika kipindi cha pili na ile ya Yanga kuchukua tahdhari zaidi katika dakika 45 za kwanza wakati timu hizo zitakapoumana Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Timu hizo kila moja imeonyesha makali ya kufumania nyavu katika muda wake ambapo Yanga wameonekana kuwa mwiba kwa safu za ulinzi za timu pinzani katika kipindi cha pili wakati Simba ni hatari katika kipindi cha kwanza.

Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Simba imefunga mabao 16 ambapo katika kipindi cha kwanza imefumania nyavu mara 11 ikiwa sawa na asilimia 68.75 huku mengine matano sawa na asilimia 31.25 ikifunga katika dakika 45 za mwisho.

Muda huo ambao Simba imekuwa ikifunga mara kwa mara ndio ambao imekuwa dhaifu katika kujilinda kwani katika mabao matano iliyoruhusu hadi sasa, mabao manne sawa na asilimia 80 imefungwa katika kipindi cha kwanza na moja ambalo ni sawa na asilimia 20, imeruhusu katika kipindi cha pili.

Dakika 15 za kwanza na dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza ndio muda ambao Simba imekuwa ikifunga zaidi ambapo kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 15 imepachika mabao matano, idadi ambayo imeyafunga pia kuanzia dakika ya 31 hadi ya 45.

Katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, Yanga imefunga mabao 20 ambapo katika dakika 45 za pili imefunga mabao 12 sawa na asilimia 60 huku kipindi cha kwanza ikiwa imefumania nyavu mara nane sawa na asilimia 40.

Tofauti na watani wao wa jadi, safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa na uwiano sawa wa kuruhusu mabao katika kila kipindi ambapo kati ya mabao manne ambayo imeruhusu hadi sasa, mawili yamefungwa katika kila kipindi cha mchezo.

Dakika 15 za pili na dakika 15 za mwisho za kipindi cha pili ndio muda ambao Yanga imekuwa ikifunga zaidi ambapo kuanzia dakika ya kwanza hadi ya 31 hadi ya 60 imepachika mabao matano, idadi ambayo imeyafunga pia kuanzia dakika ya 76 hadi ya 90.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ramadhan Kampira alisema kuwa kilichotokea katika mechi zilizopita, kinaweza kuwa tofauti katika mechi hiyo ya watani wa jadi Jumapili.

"Hii mechi huwa na utofauti mkubwa na mechi nyingine za kawaida za ligi na kuna wakati hutokea mambo ambayo wengi wanakuwa hawayategemei. Timu ambayo inafunga sana mabao inaweza isifunge na ile ambayo haifungi ikafunga lakini pia ni mchezo unaohitaji umakini kwa dakika zote.

"Ukiangalia kwa sasa, timu hizo mbili zote zina wachezaji wazuri ambao wana uwezo mkubwa wa kuamua mchezo hivyo upande ambao utapoteza umakini utajikuta katika wakati mgumu," alisema Kampira.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Madaraka Selemani alisema kuwa timu hizo mbili zisiingie na matokeo ya mechi zilizopita.

"Huu ni mchezo ambao huwa hautabiriki na unachezwaga kama fainali. Maana kwanza huwa una nafasi kubwa ya kuamua mbio za ubingwa lakini pia hakuna upande ambao unakubali kuwa na unyonge dhidi ya mwingine.

"Hivyo timu hizi zinapokutana, huwa zinajiandaa vizuri kwa kila upande kuangalia vilivyo ubora na udhaifu wa mpinzani na kuufanyia kazi tofauti na inavyokuwa kwa mechi nyingine," alisema Madaraka.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: