Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika 90 za utajiri na heshima Simba,Yanga, Mtani huko kwako vipi

Simba Yanga WA0007 Dakika 90 za utajiri na heshima Simba,Yanga, Mtani huko kwako vipi

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania nzima inamwomba Mungu azibariki klabu mbili zinazowakilisha nchi kimataifa usiku huu. Mkakati ni mmoja tu Simba, Yanga zivuke vigingi leo ugenini na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.

Yanga itaanza na Mamelodi Sundowns pale Afrika Kusini kuanzia saa 3:00 usiku, lakini baadae Simba itakiwasha na Al Ahly jijini Cairo kuanzia saa 5:00 usiku.

Pale Misri, watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly waliotwaa ubingwa huo mara 11, watakuwa wakisaka tiketi ya kucheza tena nusu fainali kwa kulinda ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba jijini Cairo ambako vigogo hao hufanya makosa kwa nadra sana.

Katika mechi nyingine inayohusisha wawakilishi wa Tanzania, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mabingwa wa michuano mipya ya Ligi ya Soka Afrika (AFL) na ambao wameshatwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja, watakuwa wakitafuta ushindi wowote ule jijini Pretoria dhidi ya Yanga baada ya kulazimisha suluhu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, matokeo ambayo hawakuyatarajia.

Katika mazingira hayo ni dhahiri nafasi za Simba na Yanga kusonga mbele zinaonekana finyu kirekodi na kiufundi, lakini mpira wa miguu una matokeo ya kushangaza kama timu zikijiandaa vizuri na ndio maana vigogo hao wa Kariakoo wameshafika Cairo na Pretoria kujaribu kufanya maajabu hayo ya soka.

Wakati Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo wa awali dhidi ya Al Ahly, lakini ikaruhusu bao mapema katika dakika ya tano lililodumu hadi mwisho, Yanga iliweka kambi langoni mwake dhidi ya Mamelodi waliotawala sehemu kubwa ya mchezo, kwani timu hiyo ya Jangwani ikapiga mashuti manne langoni dhidi ya mawili ya Wasauzi.

Jijini Cairo, hali inaonekana kuwa nyepesi kwa wenyeji watakapowakaribisha Simba majira ya saa 5:00 Ijumaa usiku, wakitarajia kuendeleza mpango wa kuimarisha rekodi ya idadi ya makombe kwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya 12 katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Alhadi Allaou Mahamat kutoka Chad.

Kocha Marcel Kohler alilazimika kuingiza kikosi chake Uwanja wa Benjamin Mkapa bila wachezaji watatu tegemeo, kipa Mohamed El-Shennawy, aliyeumia bega wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023), Emam Ashour, aliyefanyiwa upasuaji wa bega na Yasser Ibrahim, huku nyota wake kama Percy Tau wakiwa wametokea kuuguza majeraha.

Mjerumani huyo anatarajiwa na kikosi kamili Ijumaa atakapocheza mbele ya mashabiki wenye wendawazimu wa soka jijini Cairo. Mashabiki hao waliishuhudia Ahly ikichezewa nusu uwanja katika mechi ya kwanza, hivyo hawatakuwa na uvumilivu kuiona timu yao ikisumbuliwa tena nyumbani.

Ilionekana kama Ahly ilihitaji bao moja tu ili ijiweke katika mazingira mazuri ya mechi ya marudiano.

Kwa hiyo, muda mwingi ilikuwa golini ikifanya kazi moja tu ya kuharibu mipango ya Simba, kiasi Tau na winga hatari, Hussein El Shahat wakanekana hawana kazi uwanjani hadi walipotolewa katika kipindi cha pili.

Kuingia kwa Taher Mohamed, Reda Slim ambaye ana kasi, Kahraba na Afsha, kulitoa picha ya Ahly halisi itakayocheza mechi ya Cairo. Slim na Kahraba nusura wamalize mchezo Kwa Mkapa kama si ustadi wa kipa Lakred.

Jijini Cairo, hutegemei kuwaona mawinga Tau na El-Shahat wakizurura tena uwanjani kama ilivyokuwa Kwa Mkapa, huku makali ya Kahraba yakitarajiwa kuongezeka zaidi mbele ya mashabiki wao ambao hufurika uwanjani timu inapocheza mechi za kimataifa.

Mostafa Shobier, ambaye alifanya kazi kubwa ya kuizuia Simba kuandika bao muhimu nyumbani, anatarajiwa kumpisha kipa wa kwanza, Mohamed El-Shennawy.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ahly, kipa huyo mzoefu, aliyefanyiwa upasuaji wa bega, alikuwa ameanza mazoezi rasmi ya kumrejesha kikosini kwa ajili ya mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Mchezaji mwingine majeruhi anayetarajiwa kurejea kikosini ni Yasser Ibrahim, ambaye pia wiki hii alianza rasmi mazoezi ya uwanjani.

Hakuna maneno mazuri ya kuelezea ubora wa Al Ahly inapokuwa nyumbani, lakini Simba ina historia ya kufanya maajabu kimataifa. Mwaka 2003 ilipofuzu kucheza kwa mara ya kwanza hatua ya makundi, Simba iliivua ubingwa Zamalek baada ya timu zote kupata matokeo ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na hivyo mshindi kuamuliwa kwa penalti.

Lakini safari hii, Simba itatakiwa kufanya makubwa zaidi; ishinde ugenini kwa bao 1-0 ili mchezo uamuliwe kwa penalti, au ipate ushindi wa mabao 2-0 ili ivuke kirahisi.

Katika mechi saba zilizopita baina ya wawili hao, Ahly imeshinda mara tatu, huku Simba ikishinda mara mbili na timu hizo kutoka sare mara mbili. Kipigo cha bao 1-0 nyumbani wiki iliyopita kinaweza kutafsiri Simba imepiga hatua nyuma, lakini kiwango kilichoonyeshwa na vijana hao wa Mtaa wa Msimbazi kinatia moyo kuna jambo linaweza kufanyika Cairo.

Kipigo hicho kilikuja baada ya Simba kuiwekea ngumu Ahly kushinda kwenye mechi mbili za African Football League (AFL). Simba iliondolewa kwa sheria ya bao la ugenini baada ya timu hizo kufungana bao 2-2 Dar es Salaam na baadaye bao 1-1 Cairo.

“Haiishi hadi iishe,” alisema Kocha Abdelhak Benchikha akizungumzia mchezo huo wa marudiano.

“Tumecheza dakika tisini tu Tanzania. Bado tuna dakika 90 nyingine Cairo.

Tuna ubora wa kutosha wa kupindua meza, hakuna kisichowezekana katika ulimwengu wa soka. Kipigo kilituuma sana lakini tunakwenda Cairo na mpango wa kucheza na kushinda mechi.”

Makosa hayo ni pamoja na washambuliaji kutokuwa watulivu mbele ya lango, mabeki kutoelewana wakati wa shambulizi la kushtukiza na uwezo wa mabeki wa pembeni kudhibiti krosi, kitu ambacho Mohamed Hussein Tshabalala alikimudu mbele ya Tau katika mchezo wa kwanza.

Hata hivyo, bao pekee lilitokana na krosi ambayo nusura beki Inonga ajifunge kama si ubora wa kipa Ayoub Lakred.

Kipa huyo aliupangua mpira ulioelekezwa golini na beki huyo. Hata hivyo, mabeki wengine hawakuwa wamejipanga na hivyo mpira kutua kwa kiungo Ahmed Koka aliyeuzamisha wavuni.

Kosa jingine ni kutokuwa makini dakika za mwanzoni mwa mchezo ambazo Ahly walizitumia vizuri Kwa Mkapa, mwishoni mwa kipindi cha kwanza na dakika za mwisho ambazo vigogo hao wa Cairo walizitumia kusawazisha bao katika mechi ya marudiano ya African Football League (AFL), Misri baada ya kutangulia kufungwa katika dakika ya 67.

“Tumerekebisha makosa tuliyofanya katika mchezo wa kwanza,” alisema Benchikha. “Tunachoangalia sasa ni kushinda ugenini. Hatutaki kukata tamaa. Soka ni mchezo wenye matokeo ya ajabu. Haijalishi unacheza nyumbani au ugenini, kama umejiandaa vizuri na kucheza kama mlivyopanga, inawezekana kushinda ugenini.”

Simba bado haijapata mshambuliaji wa kati wa kuaminika tangu John Bocco aanze mapumziko ya kuelekea kustaafu.

Katika mechi iliyopita, Kibu Dennis alianza kama mshambuliaji lakini muda mwingi alionekana pembeni akisumbuana na mabeki na nafasi pekee aliyopata alipaisha, ingawa kibendera kilinyooshwa baadaye kuwa aliotea.

Sadio Kanoute, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza ni wachezaji wengine waliopata nafasi za kufunga, lakini walikosa utulivu na uzoefu wa kutosha kwenye mechi yenye upinzani mkali kumalizia pasi walizopewa.

Mechi ambayo imekuwa ikizungumzwa sana ni ile itakayofanyika kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld jijini Pretoria, ambako wenyeji Mamelodi watakuwa wakijaribu tena kwenda fainali watakapoikaribisha Yanga baada ya timu hizo mbili kutofungana.

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Dahane Beida kutoka Mauritania.

Kwa takwimu zote na uchambuzi wa kiufundi, Mamelodi anapewa nafasi kubwa ya kushinda na kutinga nusu fainali, nafasi ambayo wanaihitaji sana kukamilisha mpango wa kucheza Klabu Bingwa ya Dunia na kujivunia mabilioni mengine ya fedha baada yay ale ya AFL.

Zaidi ya nusu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Afrika Kusini wanatoka Mamelodi, klabu yenye utajiri wa kupindukia nchini humo na iliyowakodia wachezaji hao ndege kuwahi mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.

Sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni nzuri kwa mabingwa hao wa zamani wa Afrika, lakini katika miaka ya karibuni Yanga pia imeonyesha inaweza kupata matokeo mazuri popote.

Ilishinda mechi dhidi ya Club African, USM Alger, TP Mazembe, Marumo Gallants na Rivers United kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita. Ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Marumo Gallants uliwastua mashabiki wengi wa soka wa Afrika Kusini, hivyo mechi ya leo Ijumaa wanaiangalia kwa jicho tofauti licha ya kuwa na imani na Mamelodi.

Mamelodi wameibuka kuwa moja ya klabu bora barani Afrika ikipambana na vigogo kutoka Afrika Kaskazini, ingawa imetwaa kombe la mashindano hayo makubwa mara moja. Ushindi nyumbani na ugenini ndio moto wa vigogo hao wanaojulikana kama Wabrazili.

Wana uwezo mkubwa wa kugongeana pasi ndani ya eneo la hatari la mpinzani, lakini hawakuweza kufanya hivyo Kwa Mkapa, ambako kila mchezaji wa Masandawana aliyepenyezewa mpira ndani ya eneo la hatari, alijikuta amezongwa na kupokonywa mpira au kulazimika kurudisha kwa mabeki wake ambao hawakuwa wakivuka mstari wa kati.

Hata hivyo, kocha Rhulani Mokwena alimkosa nahodha na kiungo mshambuliaji hatari, Themba Zwane aliyekuwa na kadi.

Mshambuliaji huyo ameshafunga mabao manne msimu huu huku mengine mawili akiifungia timu ya taifa.

Uwepo wake utaongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji huku katika kiungo kukiwa na Teboho Mokoena, ambaye anasifika kwa mashuti ya mbali na alimjaribu kipa Djigui Diarra mara moja Kwa Mkapa.

“Yanga ni timu nzuri. Nadhani tulijilinda vizuri kwa sehemu kubwa ya mchezo kuwadhibiti (Kennedy) Musonda, (Clement) Mzize na (Stephane) Aziz Ki na kutowapa nafasi ni kitu kizuri, lakini tungeweza kufanya vizuri zaidi kutengeneza nafasi,” alisema kocha Mokwena.

“Tunaweza kucheza vizuri na kuutumia mpira vizuri. Hata kama tungeshinda, ningesema ni mapumziko tu. Hatuna budi kucheza vizuri zaidi mechi ya pili na kujaribu kushinda.”

Yanga itakuwa ikifurahia kurejea kwa Pacome Zouzoua, ambaye aliibeba timu mabegani mwake katika mechi za hatua ya makundi na kufunga mabao matatu, huku akiwa kinara wakati Yanga ilipoicharaza Belouizdad kwa mabao 4-0.

Zouzoua anatarajiwa kuiondoa timu kwenye nusu yake kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukokote mpira na kuchezesha wenzake.

Pia Yanga itamrejesha kiungo wake, Khalid Aucho ambaye ni muhimu katika kuiweka timu pemoja, kuitembeza pamoja na kuwa kinga kwa mabeki wake wa kati. Aucho na Zouzoua walikosa mechi ya kwanza kutokana na kuuguza majeraha.

Beki wa kulia, Yao Kouassi hatarajiwi sana kuwemo katika kikosi cha leo na huenda Shomary Kibwana akarejea katika nafasi hiyo baada ya kupona majeraha nafasi anayoweza pia kucheza Dickson Job kama ilivyokuwa katika mechi ya jijini Dar es Salaam, japo ni beki wa kati tegemeo wa timu hiyo.

Clement Mzize, ambaye amekuwa ndani na nje ya kikosi cha kwanza, alionyesha kiwango bora katika mechi ya kwanza na hakuna shaka Miguel Gamondi atamwanzisha katika mchezo huu kuwazuia mabeki wa Sundowns kupanda. Alikosa nafasi ya wazi katika mechi ya kwanza baada ya kukosa nguvu wakati akijiandaa kupiga shuti.

Mzize amekuwa msaada mkubwa kwa washambuliaji wenzake, akiwa na mikimbio inayosumbua mabeki na kasi inayomuwezesha kufikia mipira mingi mirefu na kupiga krosi ‘zenye macho’ kwa wenzake.

Stephane Aziz Ki ndiye ambaye mara kadhaa hupiga pasi hizo ndefu kumtangulizia Mzize na mara nyingi hutoa pasi muhimu zinazozalisha bao, huku Max Nzengeli akifanya kazi kubwa ya kupasua ngome, kusaidia kiungo na kurudi nyuma kutoa msaada kwa mabeki, mambo aliyoyafanya kwa ustadi katika mchezo wa kwanza.

“Niliwaambia wachezaji wangu kwa mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa si dakika tisini pekee, bali dakika 180,” alisema Gamondi baada ya mchezo wa kwanza kuisha bila kufungana.

“Tumefanikiwa kupata sare hapa nyumbani. Sasa tunarejea kwenye uwanja wa mazoezi kuchambua na kushughulikia kasoro. Kitu muhimu ni hatujafungwa nyumbani kwa sababu kama tungekuwa tumefungwa tungekuwa na kazi kubwa ugenini. Kwa hiyo tutaenda kupambana ugenini.”

Hata hivyo, uimara wa kiakili na kisaikolojia kwa wachezaji wa Simba na Yanga ndio utakuwa nguvu kwa timu hizo kupata matokeo mazuri ugenini dhidi ya timu zenye ubora kila eneo la uwanja.

Kikubwa zaidi ni kauli za makocha hao watatu, Benchikha, Gamondi na Mokwena kuwa mechi hizo hazijaisha na zitaisha tu pale filimbi ya dakika tisini zitakapopulizwa jijini Pretoria na Cairo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: