Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika 360 za mtego kwa Yanga

Mitego Pic Data Kikosi cha yanga Kikiendelea na maandalizi

Sat, 2 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kama Yanga itazitumia vyema dakika 360 za mechi nne mfululizo jijini Dar es Salaam, ikiwamo leo dhidi ya Geita Gold, ambako wameibuka na ushindi wa bao 1-0 basi wapinzani wao watakuwa na kazi kubwa kuchuana nao katika Ligi Kuu msimu huu, lakini ikishindwa kutusua ijue tabu itakuwa ipo palepale.

Ipo hivi. Ratiba ya mechi nne zijazo za ligi hiyo zinakoleza vita ya kuwania kilele cha msimamo wa ligi msimu huu kwa Yanga, Simba na Azam. Timu hizo kila moja italazimika kuchanga vyema karata katika mechi hizo ili iweze kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi na ikiwa itashindwa kufanya hivyo huenda ikajikuta inajitengenezea mazingira magumu katika mbio za ubingwa na kuwapa nafasi wapinzani wao kutamba au kuongeza pengo la pointi.

Ila ukiiangalia ratiba hiyo ni wazi ni wao tu, kwani baada ya mchezo wake dhidi ya Geita Gold, itakuwa na mechi nne za kibabe dhidi ya KMC, Azam FC, Ruvu Shooting zitakazochezwa Dar es Salaam kabla ya kwenda Lindi kuwakabili Namungo. Mechi hizo nne ni sawa na dakika 360 zinazoweza kuonyesha dira kwa Yanga. Ingawa katika mechi hizo nne, tatu zitakuwa hapa Dar es Salaam, ni ratiba inayoonekana ni ya mtego kidogo kwa Yanga kutokana na historia ya timu hizo atakazokutana nazo katika mechi zinazofuata.

Mechi dhidi ya Ruvu ndio inayoonekana haitakuwa na presha kubwa tofauti na nyingine kwani Azam, KMC na Namungo zimekuwa na historia ya kuivimbia Yanga. Msimu uliopita KMC na Azam kila moja iliifunga Yanga katika duru la pili, japo zote zilifungwa katika mechi za kwanza, pia ikalazimishana sare na Namungo mechi mbili.

Akizungumzia ratiba iliyopo mbele yao, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa wanaamini mechi zote zitakuwa ngumu.

“Mechi zitakuwa ngumu kwa sababu sasa hivi kila mchezaji anapkutana na Yanga anacheza kwa kujituma na kujitolea zaidi akiamini anacheza dhidi ya timu kubwa hivyo sisi tunachukulia kila mchezo kama fainali na mkakati wetu ni kutopoteza mechi yoyote,” alisema.

Wakati ratiba ikiwa hivyo kwa Yanga, Simba nayo haina mchekea kwani itakuwa na mechi ambazo kama isipojipenga zinaweza kumharibia hesabu. Ingawa mechi hizo nne zote itacheza ikiwa hapa jijini Dar es Salaam, michezo dhidi ya Ruvu Shooting na Namungo inaweza kuwa kibarua kigumu kwake kwani timu hizo zimekuwa zikionyesha ushindani mkubwa pindi inapokabiliana na Simba.

Ikumbukwe Maafande wa Ruvu walikuwa ni miongoni mwa timu zilizoifunga Simba katika msimu uliopita.

Hata hivyo Simba inaonekana haitakuwa na kibarua kigumu mbele ya Polisi na Coastal Union ambazo zimekuwa hazifui dafu mara kwa mara.

Kocha wa Simba, Selemani Matola amesema kila mechi kwao ina umuhimu mkubwa na watajipanga kuhakikisha wanashinda. “Hakuna mechi rahisi na kila timu inajiandaa lakini mwisho wa siku tunafahamu malengo yetu ni kutwaa ubingwa hivyo kwa pamoja tutajitahidi kuhakikisha tunatimiza hilo Mwenyezi Mungu akipenda. Tunajua kiu ya mashabiki ni kuona tukifanya vizuri na sisi tunaamini tukipata sapoti yao tutafanya vyema,” alisema Matola.

Kwa upande wa Azam wao wana mtihani mkubwa zaidi katika mechi nne zinazofuata baada ya kumalizana na Polisi Tanzania kutokana na ugumu wa timu itakazocheza nazo pindi inapokabiliana nazo. Timu hizo ni Namungo, Yanga, KMC na Geita Gold. Msimu uliopita, Namungo FC ilivuna pointi mbili kwa Azam wakati Yanga ilichukua tatu kama ilivyokuwa kwa KMC.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz