Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika 1170 za uamuzi wa mastaa Simba

GIP7WajXUAErTnb.jpeg Dakika 1170 za uamuzi wa mastaa Simba

Sun, 10 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kukabiliana na Coastal Union jana na kushinda mabao 2-1, nyota wa Simba wana mitihani miwili wanayopaswa kufaulu katika mechi 13 (dakika 1170) walizobakiza vinginevyo wataambulia patupu katika Ligi Kuu msimu huu.

Mtihani mgumu zaidi kati ya hiyo miwili ni ule wa kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kutokana na ushindani mkubwa uliopo baina yake na Yanga inayoongoza msimamo wa ligi na Azam inayoshika nafasi ya pili.

Kwa sasa Simba ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 39, ikizidiwa kwa pointi saba na kinara Yanga iliyo na pointi 46, huku ikiachwa kwa tofauti ya pointi tano na Azam FC ambayo imekusanya pointi 44.

Ili itwae ubingwa, inapaswa kuiombea mabaya Yanga angalau ipoteze michezo isiyopungua mitatu na yenyewe ipate ushindi karibia katika mechi zote 13 zilizobakia kwenye ligi lakini kinyume na hapo, inaweza kushuhudia kombe likienda Jangwani kwa mara ya tatu mfululizo kutokana na muendelezo wa matokeo mazuri ambao Yanga imekuwa nao katika ligi msimu huu.

Kibarua cha pili kwa wachezaji wa Simba ni kuboresha takwimu zao binafsi ili wajiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo binafsi za wachezaji wa nafasi tofauti mwishoni mwa msimu kutokana na wengi wao kuonekana kushindwa kufurukuta katika vita ya kuwania ushindi wa tuzo hizo mwishoni mwa msimu.

Hadi sasa, Simba imeonekana kuachwa mbali katika vita ya kuwania ufungaji bora huku nyota wa Azam na Yanga wakionekana kupigana vikumbo.

Chati ya kuwania zawadi ya mfungaji bora hadi sasa inaongozwa na Feisal Salum wa Azam mwenye mabao 12, akifuatiwa na Stephane Aziz Ki wa Yanga mwenye mabao 11 huku anayeshika nafasi ya tatu kwenye kinyang'anyiro hicho ni Maxi Nzengeli wa Yanga mwenye mabao nane sawa na Marouf Tchakei wa Ihefu na Waziri Junior wa KMC.

Kinyang'anyiro cha kipa bora ambacho mshindi wake hupatikana kwa kuwa na idadi kubwa ya mechi ambazo hajaruhusu bao (clean sheets), nacho bado Simba inajitafuta kutokana na makipa wake kuachwa mbali na vinara wanaoongoza orodha hiyo.

Baada ya mechi ya jana, Ley Matampi wa Coastal Union ni kinara akiwa amecheza mechi tisa bila kuruhusu bao akifuatiwa na John Noble wa Tabora United aliyecheza mechi saba bila nyavu zake kuguswa na wa tatu ni Djigui Diarra ambaye ana mechi sita bila kuruhusu bao.

Kipa wa Simba Ayoub Lakred ambaye hajaruhusu bao katika mechi nne kama ilivyo kwa Wilbol Maseke wa KMC na Ramadhan Chalamanda wa Kagera Sugar.

Kiungo wa zamani wa Simba, James Kotei alisema kuwa jambo la muhimu kwa Simba hivi sasa ni kuhakikisha inatwaa ubingwa badala ya kuzifikiria tuzo binafsi.

"Timu inapokuwa inapitia katika kipindi kigumu inahitaji kwanza ishinde taji ili ipate utulivu ambao utafanya hata mchezaji mmojammoja kufanya vizuri. Kwa sasa Simba inatakiwa kuangalia kwanza ushindi wa mechi zake badala ya kila mchezaji kutanguliza maslahi yake kwanza," alisema Kotei.

Chanzo: Mwanaspoti