Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika 1,260 za moto Championship

Champioship Moto Dakika 1,260 za moto Championship

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakat duru la kwanza la Ligi ya Championship likitarajia kumalizika Desemba 30 mwaka huu, imeshuhudiwa vita nzito katika kampeni za kila timu kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, zinatafutwa mbili za juu ambazo zitapanda moja kwa moja, huku mbili nyingine zikicheza mchujo ‘play off’ kuwania kupanda daraja.

Timu mbili za mkiani zitashuka moja kwa moja First League, ilhali zile za nafasi ya 13 na 14 zikicheza play off kuwani kubaki kwenye ligi msimu ujao au kushuka daraja iwapo zitakwama.

Hadi sasa Biashara United ya mkoani Mara ndio wamekamilisha michezo 15 ya mzunguko wa kwanza na kujikusanyia pointi 30 na kuwa nafasi ya pili nyuma ya vinara, Ken Gold wenye alama 32 na mchezo mmoja.

Makala haya yanakupitisha kwenye mtifuano ulivyokuwa katika mechi 14 wakati ligi ikisimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na namna raundi ya pili itakavyokuwa ya moto.

VITA YA POINTI

Mtihani mkubwa katika Championship upo kwenye kuwania pointi kusaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo na takribani timu sita kuonyesha upinzani wa kutaka nafasi hiyo.

Timu za Ken Gold, Mbeya Kwanza, Biashara United, Pamba Jiji, Mbuni na TMA zote zinao uwezo wa kuonyesha kitu kwenye harakati za kupanda Ligi Kuu msimu ujao kutokana na matokeo waliyonayo.

Ken Gold ndio wanaongoza kwa pointi 32, Biashara United (30), Mbeya Kwanza (29), Pamba Jiji (28) na Mbuni na TMA zikiwa na pointi 28 kila mmoja, huku Mbeya City ikivuna 21 na Polisi Tanzania 20.

UFUNGAJI MABAO

Wakati timu zenyewe zikipepetana kwenye vita ya pointi, ufungaji nao umekuwa mkali kwa mastaa kujibizana kibabe kwa kufumania nyavu na kufanya ligi kuendelea kuwa na ushindani na mvuto.

Katika vita hiyo imeshuhudiwa mastaa wa zamani waliowahi kutamba na timu kadhaa za Ligi Kuu wakitakata zaidi kwa kuonyesha uwezo wao kuzisaidia timu hizo kwenye ndoto za kupanda daraja.

Boban Zirintusa wa Biashara United na Willy Edgar (Ken Gold) ndio wanaongoza kwenye orodha ya wafungaji bora wakiwa wametupia mabao 11 kila mmoja.

Wengine ni Ramadhan Kapera wa Mbeya Kwanza mwenye mabao tisa sawa na Salimu Aiyee wa Mbuni FC, huku Abdulkarimu Segeja (Copco) na Kassim Shaibu wa Green Warriors wakiweka mabao nane kila mmoja.

TIMUA TIMUA MAKOCHA

Mechi 14 za mzunguko wa kwanza hazikuwa rafiki kwa baadhi ya makocha kukutana na rungu kutokana na matokeo kutoridhisha, huku wengine wakiamua kuingia mitini wenyewe.

Katika timuatimua hiyo, FGA Talents ndio wamekuwa vinara kwenye kutimua makocha wengi baada ya kuachana na watatu kutokana na kutoridhishwa na matokeo ya timu hiyo.

FGA Talents ilianza msimu ikiwa chini ya Novatus Fulgence ambaye alidumu kwa takribani mechi sita na kujikuta akionyeshwa mlango wa kutokea kutokana na kile alichofanya.

Baadaye timu hiyo ilimtambulisha Athuman Kairo ambaye naye hakudumu kwa kutimuliwa na nafasi yake kujazwa na Ngawina Ngawina aliyetangazwa juzi akitokea TMA.

Pan African nao wanaingia kwenye timu zilizotimua makocha kutokana na aliyekuwapo Mohamed Kijuso kuachana nao, huku Stand United nao wakipeana mkono wa kwaheri na Mahadi Fahadi kisha kumpa kazi Ally Kisaka aliyepo hadi sasa.

Ruvu Shooting ambao wanachechemea kwenye ligi hiyo wakiwa hawajapata ushindi wowote kwenye mechi 14 wakipata sare moja na kupoteza 13, aliyekuwa kocha mkuu, Khalid Adam aling’atuka mwenyewe kutokana na mazingira magumu.

VIPIGO VIZITO

Wakati kila timu ikiendelea kupiga hesabu za kumaliza vyema mzunguko wa kwanza, yapo matokeo yaliyoacha maumivu kwa baadhi ya timu kutokana na kuruhusu idadi kubwa ya mabao.

Katika mechi hizo, Mbuni ikicheza kwenye ubora wake iliikandika mabao 5-0 Ruvu Shooting, Mbeya Kwanza ikawalima 4-0 Mbeya City na Biashara United ikiilaza Pan 4-0.

Green Warriors nao walijikuta kwenye kipigo cha aibu walipolizwa mabao 5-2 dhidi ya Mbeya City, Ken Gold ikaichakaza 4-0 Pan African na Pamba Jiji ikaizima 4-0 Cosmopolitan.

MASTAA

WAFUNGUKA

Straika wa Biashara United, Boban Zirintusa anasema pamoja na matokeo waliyopata mzunguko wa kwanza, lakini bado kazi ni nzito akisema lazima wajipange vizuri na raundi ya pili ili kufikia malengo.

Kuhusu ufungaji bora msimu huu, nyota huyo anakiri ugumu akieleza anaendelea kupambana kuhakikisha kila mechi anayopata nafasi anatumia vyema uzoefu wake kufunga mabao.

“Lazima twende kujiuliza tena ili makosa yaliyoonekana kwa mechi za mzunguko wa kwanza tuyareebishe, lakini ninapopata nafasi ya kuanza uwanjani nitumie vyema madhaifu ya beki kufunga mabao,” anasema staa huyo.

Naye Ramadhan Kapera wa Mbeya Kwanza anasema msimu huu anayo mambo mawili akianza kuirejesha timu Ligi Kuu, kisha kugeukia ufungaji bora akichekelea kiwango walichonacho wachezaji kikosini.

“Kwa jumla naona nimebadilika binafsi kwa sababu nilipotea uwanjani kutokana na majeraha lakini kwa sasa nashukuru nimeimarika na kocha wetu ameniamini, hivyo napambana kufikia malengo,” anasema Kapera.

MAKOCHA NAO

Kocha mkuu wa Ken Gold, Jumanne Challe anasema msimu huu mkakati wao ni kupanda daraja baada ya kukosa nafasi hiyo misimu mitatu mfululizo na wanakuja kwa ‘surprise’.

Anaeleza kwa sasa wanajiandaa na mchezo dhidi ya Polisi Tanzania kuhitimisha kibabe raundi ya kwanza wakibaki kileleni akiwaomba nyota wake kutobweteka.

“Tunahitaji ushindi bila kujali nyumbani au ugenini, malengo yetu msimu huu tupande Ligi Kuu, tunakuja kwa surprise wengi hawaamini ila tutawashangaza, vijana lazima wapambane,” anasema Challe.

Kocha msaidizi wa Mbeya City, Mathias Wandiba anasema licha ya kupoteza mechi kadhaa kwa sasa wamejipata na wanahitaji ushindi mchezo wa kukamilisha mzunguko wa kwanza dhidi ya FGA Talents.

“Tutajipanga upya na mzunguko wa pili kuhakikisha lazima tutaboresha kikosi japokuwa tunao wachezaji wenye uwezo wa kutufikisha tunapotaka,” anasema Wandiba.

Chanzo: Mwanaspoti