Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dah! msimu mmoja, makocha 31 Ligi Kuu

Nabi Robertinho Er Dah! msimu mmoja, makocha 31 Ligi Kuu

Wed, 17 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa Ligi Kuu Bara 2022/2023 upo ukingoni kila timu ikimalizia kuvuna ilichokipanda lakini msimu huu umekuwa wa aina yake kwani licha ya kuwa na timu 16 ila makocha wasiopungua 31 wameziongoza timu kwenye mechi.

Timu 12 kati ya 16 za Ligi Kuu, msimu huu zimebadili makocha huku nne pekee za Yanga, Singida Big Stars, Geita Gold na Mbeya City zikiwa ndizo zimedumu na makocha wakuu zilizoanza nao msimu bila kubadilisha.

Nassredine Nabi wa Yanga, Hans van der Pluijm wa Singida, Fred Felix 'Minziro' wa Geita na Abdallah Mubiru wa Mbeya ndio makocha pekee ambao hawajaachia kijiti hadi sasa ikiwa baadhi ya timu zimebakiza mechi mbili na nyingine tatu.

Kupitia makala haya, hizi hapa timu zote 16 na makocha waliozinoa msimu huu.

YANGA

Muda wowote Wananchi watatangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, na inakaribia kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na lile la TFF (ASFC), na mafanikio yote hayo inayapata ikiwa chini ya kocha mkuu mmoja tu, Nabi.

Kuna kipindi upepo ulimuendea ndivyo sivyo Nabi na Wanajangwani kutaka kumtimua lakini alibadili kila kitu alivyoifunga Monastir nchini kwao na imani kurejea ambapo amekuwa akiaminika hadi sasa.

SIMBA

Wababe hawa wa msimbazi msimu huu benchi lao limeongozwa na makocha wanne kwa nyakati tofauti hadi sasa. Msimu ulianza wakiwa chini ya Mserbia, Zoran Maki lakini ghafra akaondoka na timu kubaki kwa Selemani Matola na baadae wakampa mikoba Juma Mgunda akitokea Coastal Union.

Baada ya hapo Mgunda aliiongoza vyema Simba lakini baadae ilimuajiri Mbrazil Roberto Oliveira 'Robertinho' na Mgunda kuwa msaidizi wake huku Matola akirudi shule kuchukua ujuzi na hadi sasa inamaliza msimu bila taji lolote licha ya kupita kwa makocha hao wote. Lakini kuna mabadiliko makubwa yanakuja pale kwenye benchi na wawili huenda wakang'olewa.

AZAM FC

Matajiri hawa wa Chamazi msimu huu wamefundishwa na makocha watatu tofauti. Walianza kwa mbwembwe chini ya kocha Mkuu Mmarekani mwenye asili ya Sudan, Abdihimid Moallin ambaye baadae alifungashiwa virago na timu kubaki kwa Muingereza Kalimangonga Ongala 'Kally', lakini baadae ilimuajiri Mfaransa Denis Lavagne kukinoa kikosi hicho licha ya kwamba naye safari yake haikuwa ndefu na kuondoshwa kikosini hapo na mikoba kubaki kwa Kally anayesimamia Shoo hadi sasa.

Tayari Azam imepata kocha Mpya Msenegali Youssouph Dabo, na yupo viunga vya Chamazi akiandaa mipango ya msimu ujao lakini kwa mechi zilizobaki za ligi na fainali ya Kombe la TFF (ASFC), ataendelea kusimama Kally.

SINGIDA BIG STAR

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu, Singida Big Stars imeweza kutoboa na kocha mkuu mmoja, Pluijm tu.

Huenda uzoefu wake kwenye Ligi Kuu akiwa amewahi kuzinoa Yanga, Azam na Singida sambamba na usajili mkubwa aliofanya mwanzoni mwa msimu ndio vimemfanya akae 'Top Four' na kuendelea kuiongoza Singida bila kugasiwa.

GEITA GOLD

Wachimba dhahabu hawa wa Geita nao wameweza kumuheshimisha Minziro na kumuachia timu kwa msimu mzima.

Minziro ndiye aliwapandisha daraja kutoka Championship misimu miwili nyuma lakini baada ya hap walimfanya kuwa msaidizi na kumshusha Ettiene Ndayiragije ambaye baadae alifungashiwa virago na kikosi kubaki kwa Minzoro hadi sasa.

NAMUNGO

Wauaji wa kusini msimu huu wamefundishwa na makocha watatu tofauti.

Msimu ulianza wakiwa chini ya Mzambia, Honor Janza lakini baadae aliondoka na timu kubaki chini ya Jamuhuri Kihwelo 'Julio', ambaye baadae aliondoka na kikosi kukabidhiwa kwa Denis Kitambi aliyepo hadi sasa.

KAGERA SUGAR

Wakata miwa hawa wa Bukoba walianza msimu huu wamenolewa na makocha wawili ambapo walianza na Mkenya Francis Baraza na baadae kumfungashia virago na mikoba kupewa Mecky Mexime anayewanoa hadi sasa.

IHEFU

Walima Mpunga hawa wa Mbalali Mbeya kwa msimu huu wamefundishwa na makocha watatu tofauti.

Baada ya kuipandisha kutoka Championship, Zuberi Katwila aliendelea kuinoa Ihefu lakini baadae maji yalizidi unga na mikoba kupewa Juma Mwambusi aliyefundisha kwa muda kabla ya kuondoka na timu kurejea kwa Katwila na baadae wakamleta John Simkoko anayeifundisha hadi leo.

TANZANIA PRISONS

Maafande wa magereza hawa msimu huu wamenolewa na makocha wawili. Walianza na Mkenya Patrick Odhiambo aliyefundisha hadi katikati ya msimu na baada ya hapo alifukuzwa na mikoba kupewa Mohamed Abdallah 'Bares' anayekinoa kikosi hicho hadi sasa.

DODOMA JIJI

Walima zabibu hawa wa Dodoma nao msimu huu wamenolewa na makocha wawili. Shoo ilianza wakiwa chini ya Mrundi, Masoud Djuma lakini baada ya mechi kadhaa aliachishwa kazi na mikoba yake kuchukuliwa na Mmarekani Meris Medo anayepiga kazi hadi leo.

COASTAL UNION

Wagosi wa Kaya msimu huu wamenolewa na makocha wanne tofauti. Msimu ulianza wakiwa chini ya Mgunda lakini baadae alitimka ghafra hadi Simba baada ya kuwekewa mkwanja wa maana na timu kubaki chini ya Joseph Lazaro.

Hata hivyo, Lazaro baadae aliletewa Mkenya Yusauph Chipo kuwa bosi wa kikosi hicho ambaye naye hakudumu na kuondoshwa baada ya mechi kadhaa na mikoba kurejea kwa Lazaro aliyefundisha hadi pale walipomuajiri Fikiri Elias anawanoa hadi sasa.

MTIBWA SUGAR

Wakata miwa wa tuliani wamenolewa na makocha wawili kwa msimu huu kwani walianza na Salumu Mayanga lakini katika dakika za majeruhi walimfukuza na timu kubaki kwa Awadhi Juma ambaye atamalizia msimu kabla ya kumleta kocha mpya msimu ujao.

MBEYA CITY

Wajanja wa Mbeya hawa nao msimu huu wamekomaa na kocha mmoja Mubiru raia wa Uganda licha ya kuwa hawapo kwenye hali nzuri kwenye msimamo lakini bado wamemuachia yeye amalize kila kitu kwa msimu huu.

KMC

Wanakinondoni msimu huu wamefundishwa na makocha wawili tofauti. Walianza na Mnyarwanda Thierry Hitimana aliyeiongoza timu karibu robo tatu ya mechi zote msimu huu lakini matokeo mabaya yakafanya afukuzwe.

Kwa sasa timu imekabidhiwa kwa Julio ambaye ametinga KMC na wasaidizi wake, Kharid Adam na Boniphace Pawasa.

POLISI TANZANIA

Maafande wa Polisi hawa nao msimu huu wamepata maujuzi kutoka kwa makocha watatu tofauti kwani walianza msimu wakiwa na Mrundi Josline Bipfubusa aliyetimuliwa baadae na kikosi kubaki kwa John Tamba.

Hata hivyo baadae walimkabidhi mikoba ya kuwanoa maafande hao Mkongomani Mwinyi Zahera ambaye anahangaika kuhakikisha timu hiyo inabaki Ligi Kuu licha ya kuwa na nafasi finyu.

RUVU SHOOTING

Wazee wa kupapasa msimu huu wamenolewa na makocha wawili tofauti lakini mambo yao bado yanaenda ndivyo sivyo kwani wako mkiani.

Chama hili lilianza msimu likiwa chini ya Boniphace Mkwasa lakini baadae aliamua kuiacha timu hiyo kutokana na sababu mbalimbali na kuchukuliwa na Mbwana Makata anayeinoa hadi leo licha ya kwamba ipo kwenye hatari kubwa ya kushuka daraja.

Yanga- Nabi

Simba- Zoran, Matola, Mgunda, Robertinho.

Azam- Moalin, Lavagne, Kally

Singida- Plujm

Geita- Minziro

Namungo- Janza, Julio, Kitambi

Kagera- Baraza, Mexime

Ihefu-Katwila, Mwambusi, Simkoko

Tanzania Prisons- Odhiambo, Baresi

Dodoma Jiji- Djuma, Medo

Coastal Union- Mgunda, Chipo Lazaro, Fikiri

Mtibwa Sugar- Mayanga, Awadhi

Mbeya City- Mubiru

KMC- Hitimana, Julio

Polisi Tanzania- Bipfubusa, John Tamba zahera

Ruvu Shooting- Mkwasa, Makata.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: