Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dah! Chama ndio basi tena

Chama Clatous En Kiungo wa Simba Clatous Chotta Chama

Fri, 8 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Swali lililotawala kwenye vijiwe vya mashabiki wa Simba ni moja tu. Clatous Chama ataicheza robo fainali?.Jibu la kikanuni ni Hapana.

Kanuni za mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika zinaifanya Simba ishindwe kumtumia kiungo huyo msimu huu na maumivu yote hayo yametokana na dakika 102 tu.

Dakika hizo ndizo ambazo zimemponza Chama kwani ndizo alizocheza katika mashindano hayo akiwa na kikosi cha RS Berkane kabla ya kutimka na kujiunga Simba katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari.

Kwa mujibu wa kanuni ya nne ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, mchezaji aliyetumika ama kwa kuanza kikosi cha kwanza au kwa kuingia kutokea benchi katika mchezo wowote wa mashindano hayo, hatoruhusiwa kuchezea klabu nyingine jambo ambalo linamfanya Chama aikose Orlando Pirates kwenye robo fainali.

Si hapo tu hata hatua zinazofuata za mashindano hayo ikiwa Simba itasonga mbele hataruhusiwa kucheza msimu huu.

“Ndani ya mwaka mmoja,mchezaji kimsingi atakuwa halali kuchezea klabu moja hiyohiyo katika katika mashindano ya klabu ya Caf.Hata hivyo kwa mchezaji ambaye amesajiliwa katika orodha ya klabu ambaye hajapangwa katika mchezo wowote wa mashindano ya klabu ataruhusiwa kuchezea klabu nyingine inayoshiriki mashindano ya klabu Afrika ndani ya mwaka mmoja ilimradi iwe imetimiza matakwa ya kikanuni.

“Mchezaji aliyepangwa ni miongoni mwa 11 wanaoanza katika mechi au ambaye amepishana na mmoja kati ya wachezaji walioanza katika kikosi cha kwanza. Mchezaji wa akiba aliye katika orodha ambaye hajashiriki kama ilivyofafanuliwa hapo juu, hatohesabika kama alipangwa,” inafafanua kanuni hiyo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa akiwa na RS Berkane, Chama alicheza mechi mbili kwa jumla ya dakika 102 ambazo ni dhidi ya Ben Guardane ya Tunisia na ya nyumbani waliyocheza na APR ya Rwanda ambazo kama angeishia kukaa benchi tu, leo hii Simba ingekuwa inamtumia kwenye mashindano hayo.

Mchezo dhidi ya Ben Guardane ugenini ulikuwa ni wa raundi ya kwanza ambao Chama alianza kikosini na kucheza kwa dakika 65 kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Bakr El Helali ingawa katika mechi ya marudiano iliyochezwa Tunisia hakucheza.

Baada ya hapo, Chama hakucheza mechi ya raundi iliyofuata ugenini dhidi ya APR ambayo iliisha kwa sare tasa na waliporudiana huko Morocco na kushinda mabao 2-1, kiungo huyo aliingia kutokea benchi katika dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Sofian El Moudane.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema; “Chama ni mchezaji mzuri lakini ndio hivyo haruhusiwi kucheza. Hata katika hatua zilizopita hakucheza hivyo Simba ilishajiandaa kucheza bila yeye na naamini kama ikijiandaa vyema itafanya vizuri.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live