Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dabo kuleta Double Impact Azam FC

Dabo Dabo kuleta Double Impact Azam FC

Sun, 16 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Double Impact ni filamu ya kibabe iliyotamba sana miaka ya 1990 iliyochezwa na Jean-Claude Van Damme aliyetumia jina la Chad, sambamba na Bolo Yeung, aliyecheza kama Alex Wagner.

Hii ilikuwa filamu ya pili kwa Van Damme kushirikiana na Bolo Yeung, baada ya ile nyingine ya Bloodsport ya miaka ya 1980.

Pia ilikuwa filamu ya tatu kwa Van Damme kushirikiana na muongozaji Sheldon Lettich, ambaye huko nyuma aliandika filamu ya Bloodsport na akaongoza filamu ya Lionheart.

Double Impact ilitoka Agosti 1991 na ni moja ya filamu zilizompa heshima kubwa sana Van Damme.

Mkasa wa filamu hii ni kwamba Chad (Van Damme) na Alex Wagner (Bolo Yeung) ni watoto mapacha ambao wazazi wao waliuawa katika shambulio la risasi la wahalifu. Mlinzi (bodyguard) wa familia aliyeitwa Frank, akatoroka na Chad, na dada wa kazi (house maid) akatoroka na Alex.

Frank akaenda na Chad nchini Ufaransa na dada wa kazi akampeleka Alex kwenye kituo cha Yatima mjini Hong Kong na kumuacha hapo akilelewa.

Mapacha hao hawakuonana tena hadi miaka 25 baadaye. Na ilikuwa baada ya Chad na Frank kufungua biashara ya dojo (sehemu ya kujifunzia sanaa ya mapigano), mjini New York Marekani.

Biashara yao ikanoga na wakataka kuitanua na kwenda kufungua ofisi nyingine mjini Hong Kong.

Kama zali, huko Hong Kong Alex na Chad wakakutana na baadaye wakakubaliana kuungana kulipa kisasi kwa wauaji wa wazazi wao na kufuatilia mirathi ya biashara za wazazi wao.

Katika harakati hizi, mapacha hawa wakafichua biashara kubwa haramu ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine wa kutisha.

Kwa hiyo harakati zao za kulipa kisasi na kupata mirathi zikaleta vishindo viwili, kutimiza dhamira yao na kufichua uhalifu...ndiyo maana ya Double Impact. Hiki ndicho kocha mpya wa Azam FC anakifanya ndani ya klabu hiyo ya Chamazi.

Baada ya kufichua mgawanyiko mkubwa kwenye benchi la ufundi na kusababisha Thank You, mwamba sasa kaungana na 'pacha wake', kukamilisha Double Impact. Djibil Sillah, kiungo wa ushambuliaji kutoka Raja Casablanca, alikuwa silaha kubwa ya Dabo kwenye klabu ya Tengueth FC ya Senegal.

Nyota huyo mwenye uwezo mkubwa, alimsaidia Dabo kushinda mara mbili mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2021.

Na sio tu kufika hatua ya makundi bali kwa kuitoa Raja Casablanca, iliyoangukia Kombe la Losers na kulibeba.

Wawili hawa, pamoja na Malickou Ndoye ambaye alitangulia tangu msimu uliopita ndiyo walioiangamiza Raja, na sasa wanaungana kama Van Damme, Bolo Yeung na Sheldon Lettich. Muungano wao umeashaanza kuleta double impact ndani ya Azam FC.

1. IMPACT Dabo amegundua kwamba tatizo namba moja la Azam ni nidhamu. Taarifa za ndani ya klabu zinasema kocha huyo amebadilisha kila kitu kuanzia mpangilio wa ukaaji wakati wa kula pale Canteen Chamazi, hadi kulala vyumbani. Zamani wachezaji walikuwa wanaenda kula kwa muda wanaoutaka wao na kukaa kwenye kitu chochote.

Utaratibu mpya ni kwamba wachezaji wote, lazima waende pamoja, na wafike dakika tano kabla ya muda wa kuanza kula.

Walifika wanakaa kusubiri muda ufike, na wanakaa sehemu yao maalumu...yaani kwenye meza zao.

Kuna meza kwa ajili ya wachezaji, kwa ajili ya benchi la ufundi na kwa ajili ya wafanyakazi wengine wanaokuwa na timu muda wote...kama.watu wa habari.

Atakayekaa kwenye meza tofauti atapigwa faini...itakayokatakwa kwenye mshahara wake.

Jambo hili limesaidia sana kuanza kurudisha nidhamu ndani ya timu.

2. MBINU

Dabo anasema wachezaji wa Azam ni mafundi kweli kweli lakini tatizo lao kubwa ni kuelewa mbinu.

Kwenye moja ya mahojiano aliyoyafanya na mtandao wa Instagram wa klabu, Dabo alisema wazi kwamba ana kazi kubwa ya kufanya kuwasaidia wachezaji hao kujua kucheza kimbinu.

Wachezaji wote wanatoka kwenye maeneo yao kufuata mipira bila kuwa na nidhamu ya maeneo.

Lakini akasema wachezaji wake siyo wazuri sana pale timu inapokuwa haina mpira...akasema ndiyo maana inaruhusu sana mabao kwa sababu inaacha mianya mingi kwa wapinzani kupenyeza mipira. Kuweza kuhimili hii, ni lazima timu iwe na utimamu wa mwili wa hali ya juu sana.

Na hiki ndicho anachifanyia kazi mjini Sousse nchini Tunisia. Azam inafanya mazoezi ya nguvu sana huko. Katika moja ya machapisho ya Instagram kutoka Tunisia, wachezaji wa Azam wanaonekana kuchoka vibaya na kuanguka mazoezini.

Abdul Sopu kwenye moja ya mahojiano, anasema yeye binafsi hajawahi kufanya maandalizi ya klabu ya misimu kwa misimu mitatu iliyopita na anachokutana nacho kwa sasa anaamini kitawasaidia sana msimu ujao.

Kauli hii ina maana kubwa sana, lakini picha ya jumla ni kwamba Dabo analeta Double Impact ndani ya Azam FC.

Chanzo: Mwanaspoti