Kocha wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema katika mchezo uliobaki wa Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Geita Gold wataenda kuucheza kama fainali, kwani umeshikilia hatma ya timu hiyo kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku akibainisha hautakuwa mwepesi kutokana na hali mbaya ya Geita.
Dabo ameyasema hayo baada ya jana kuiongoza Azam kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ulioshuhudiwa kiungo mshambuliaji, Feisal Salum 'Fei Toto' akifunga mara mbili na kumfikia Stephane Aziz KI wa Yanga kila mmoja akiwa na mabao 18.
Ushindi huo umeifanya Azam kuendelea kushikilia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 66 sawa na Simba iliyoko nafasi ya tatu, tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufunga ambayo ni manane.
Keshokutwa Jumanne Azam itakuwa wageni wa Geita Gold katika mchezo wa mwisho kwa msimu huu wa Ligi ya Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita.
“Mipango yetu ni kuendelea kushikilia hapa tulipo kwa sababu mechi dhidi ya Geita itakuwa fainali na tunatakiwa kujiandaa vizuri kwa sababu haitakuwa rahisi kwani hata Geita watataka kushindani kutokana na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.
“Tunahitaji kupambana nao na kucheza mtindo wetu wa uchezaji na mwishowe tushinde ili kumaliza hapa tulipo,” amesema Dabo.
Katika mchezo huo wa mwisho, Geita Gold nayo inapiga hesabu za kushinda kwani inafahamu kwamba ikipoteza basi itashuka daraja moja kwa moja kwani hivi sasa ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 25. Juu yake kuna Tabora United yenye pointi 27.
Maombi ya Geita ni kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Azam ili kufikisha pointi 28, huku ikiiombea Tabora United ipoteze mbele ya Namungo ili icheze play off ya kupambana kubaki ligi kuu.
Azam inaisaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo waliipata mara moja tu mwaka 2014 walipokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara 2013-2014, tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kucheza Ligi Kuu 2008.