Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dabo aipigia hesabu kali Simba

Rdg Kocha Dabo Dabo aipigia hesabu kali Simba

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema wala hawana presha ya kukabiliana na Simba ambayo inaonekana kufanya maboresho safu ya ushambuliaji akiisubiri kwa hamu ili kumalizana nayo siku tisa zijazo.

Simba na Azam zinatarajiwa kukutana Februari 9 katika mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Bara ambao awali ulipangwa kuchezwa mwishoni mwa mwaka jana kabla ya kusogezwa mbele baada ya mapumziko ya ligi kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi na ushiriki wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' kwenye fainali za Kombe la Mataifa (Afcon), zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Nyota wapya wa safu ya ushambuliaji wa Simba ni Freddy Michael Kouablan ambaye ni raia wa Ivory Coast aliyetokea Green Eagles ya Zambia na Mgambia Pa Omar Jobe ambaye amesajiliwa akiwa mchezaji huru.

Dabo ambaye anaendelea na dozi ya maandalizi kwa wachezaji akiwemo mshambuliaji mpya raia wa Colombia Franklin Navarro(24), alisema wanataka kuendelea walipoishia kabla ya Ligi Kuu Bara kusimama.

"Tunajua ubora wa Simba. Najua wanaweza kubadilika kwa sababu ya maingizo mapya, lakini hilo siyo tatizo kwetu. Tupo kwenye maandalizi na nina furaha kuona vijana wangu wakiwa na morali nzuri, huku kila mmoja akionyesha kuuhitaji mchezo. Tutaangalia nani ambaye atakuwa tayari zaidi kimchezo," alisema Dabo.

"Tumeupa uzito mchezo kama ilivyo michezo mingine. Najua kuwa hii ni dabi, lakini naamini wachezaji wangu watakuwa watulivu na wataonyesha kile ambacho tumekuwa tukikifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi. Popote tupo tayari kucheza maana bado uwanja haujatangazwa."

Wakati Azam ikijiandaa na mchezo huo, Dabo anaonekana kuwa na programu tofauti za mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex ambako wamekuwa wakifanya katika uwanja wa nyasi asili na bandia ili kuwa tayari na uamuzi wowote ambao utatolewa wa wapi ambapo mchezo huo utachezwa.

Kuhusu uwezekano wa wachezaji wapya Franklin Navarro na Yeison Fuentes kutoka Colombia pamoja na Mohammed Mustafa aliyesajiliwa kutoka El Merriekh ya Sudan kuwa sehemu ya mchezo, kocha huyo alisema hawatawapa presha na kwamba wataangalia nani ambaye atakuwa tayari zaidi kucheza.

Kwa upande wake, Mustafa ambaye anatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza kwenye ligi kutokana na machaguo ya kwanza eneo la kipa kupata majeraha, alisema: "Nina furaha kuwa hapa naamini kama mambo yakiwa vizuri nitasalia. Najua presha ya dabi ilivyo kwa sababu nimezicheza sana. Naamini kwenye ubora nilio nao hivyo nipo tayari kuanza kazi."

Rekodi zinaonyesha katika mechi nne zilizopita baina ya miamba hiyo kila upande umeshinda mara moja na sare mara mbili. Mara ya mwisho kukutana kwenye ligi ilikuwa Februari 21, mwaka jana zikitoka sare ya bao 1-1 ambapo Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Prince Dube katika dakika ya pili, lakini dakika ya 90 Kibu Denis aliizawazishia Simba.

Chanzo: Mwanaspoti