Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dabo afuta bonasi ya wachezaji Azam FC

Dabo Azam 128.png Dabo afuta bonasi ya wachezaji Azam FC

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Raundi ya nne ya Ligi Kuu Bara iligubikwa na matukio yenye utata kwenye mechi kadhaa ikiwemo ya Azam FC dhidi ya Dodoma Jiji dimbani Jamhuri mjini Dodoma.

Mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bila kufungana ilizua mijadala mingi kwa wafuatiliaji wa soka kutokana na Azam FC kukataliwa bao lao safi.

Wakati wengi wakimlaani yule mwamuzi msaidizi aliyenyoosha kibendera kuashiria kuotea kwa mfungaji wa bao lile, wachezaji wa Azam FC walilia na kocha wao Yousouph Dabo.

Kwa kawaida, Azam FC hutoa bonasi kwa wachezaji wao pale wanaposhinda mechi ya mashindano.

Japo chanzo cha ndani hakikutaka kutaja kiasi kamili, lakini inakadiriwa kuwa kati ya Sh25 milioni hadi milioni 30 kwa mechi.

Lakini bonasi hiyo ni kwa ushindi tu. Matokeo zaidi ya hapo hayana bonasi.

Kwenye mchezo dhidi ya Dodoma, Azam FC wangeweza kushinda kama siyo kukataliwa bao lao halali.

Zaidi ya hivyo, walionyesha ari kubwa sana ya upambanaji uwanjani, kitu ambacho wamiliki wa timu hiyo hukipata kwa nadra sana hasa kwenye mechi za mikoani.

Kwenye mazingira kama haya, wamiliki huwa na utaratibu wa kuwapa bonasi wachezaji kuwapongeza kwa ufanisi wao hata kama hawakushinda.

Mfano ni mechi dhidi ya Yanga mwaka 2020 ambayo mwamuzi Elly Sasii alikataa mabao mawili na penalti za Azam FC na mchezo kumalizika kwa sare tasa.

Mabosi wa Azam FC waliwapa pesa wachezaji kwa sababu ushindi ulikosekana kwa mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wao.

Hata mechi ya sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar msimu uliopita, Desemba 2022 pale Kaitaba, mabosi walofurahishwa na ari ya wachezaji kupambana kutoka nyuma 2-2 na kusawazisha - wakatoa bonasi.

Yaani kama timu haikushinda lakini wachezaji walipambana, mabosi hutoa bonasi kama mechi ya ushindi.

Kwa hiyo hata mechi ya Dodoma, mabosi walikuwa tayari kutoa bonasi kwa wachezaji kuwapongeza kwa ‘pafomansi’ nzuri.

Lakini kocha Dabo akawakataza waajiri wake kwa kusema wachezaji hawatakiwi kupongezwa eti kwa ‘pafomansi’ bila kushinda.

Hoja yake ni kwamba ‘pafomansi’ nzuri ni wajibu wao kila mechi, hakuna haja ya kuwapongeza.

Wanatakiwa kupongezwa kwa kushinda mechi, hivyo akazuia bonasi.

Dabo anaamini kwamba wachezaji hawapaswi kudekezwa kwa kupongezwa kwa ‘pafomansi’ bila ushindi, akisema hilo ni moja ya makosa yaliyoichelewesha Azam FC.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, Dabo anataka wachezaji wake wazoee kucheza kwa kiwango cha juu kila mechi.

Hiki ni kitu ambacho hakikuwepo Azam FC na kimewachanganya sana wachezaji.

“Hata hivyo, yeye mwenyewe anajua namna ya kuwafanya waelewe wajibu wao wa kucheza vizuri kila mechi,” kilisema chanzo chetu.

Dabo anaamini kwamba wachezaji wa Azam FC wamekuwa wakiishi kwenye raha bila presha ya kutafuta matokeo na madhara yake kucheza vizuri kunakuwa kitu cha kupongezwa hadi na wamiliki.

“Kocha kabadilisha vitu vingi sana, na mara zote hata kwenye ‘interview’ zake utasikia anasema mentality yaani fikra,” kilisema chanzo chetu.

Baada ya mechi ya Dodoma Jiji, timu iliondoka usiku huohuo kwenda Tanga.

Wachezaji wengi walitaka walale Dodoma halafu waondoke siku iliyofuata, lakini Dabo akakataa na kuamuru safari ifanyike usiku uleule.

“Lengo lake ni kuwakumbusha wachezaji kwamba wapo hapa kucheza siyo kupumzika. Baada ya mchezo wa Dodoma, akili zao zilitakiwa kuiwaza mechi ya Coastal Union, siyo kulala,” kilisema chanzo chetu.

Haya siyo mambo ya kawaida kwa wachezaji wa Azam FC kwani siku zote wao ndiyo walikuwa wakichagua muda wa kuondoka baada ya mechi yoyote ya mkoani.

Makocha waliopita waliwapa huo uhuru, lakini Dabo amewanyang’anya.

Hata siku ya mechi ya Coastal Union asubuhi timu ilienda kufanya mazoezi uwanja wa TFF Mnyanjani - Tanga na jioni ikaenda kwenye mechi.

“Unajua timu ilisafiri usiku kucha wa tarehe tatu kuamkia nne, na kufikia Tanga asubuhi. Ikapumzika siku yote ya tarehe 4 bila mazoezi na kocha kupanga mazoezi asubuhi ya siku ya mechi kufidia Ile siku ya kupumzika,” chanzo kilisema.

Maneno hayo pia yalithibitishwa na kocha msaidizi, Bruno Ferr, kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Coastal Union.

Kama mabadiliko haya anayoyaleta Dabo yatafanikiwa, basi Azam FC itakuwa kwenye utamaduni mpya na kuanza zama mpya kabisa.

Yawezekana lile tatizo la homa za vipindi, leo kiwango juu kesho chini la Azam FC likawa limepata mwarobaini.

Lakini, hata hivyo, wachezaji wengi wa Azam FC ni kama wanamuona Dabo kocha mkali sana kwao, ila hawana namna.

Inasemekana wamiliki wa Azam FC sasa wameamua jambo moja, kumsikiliza kocha. Basi.

Miaka mingi wamekuwa wakiwasikiliza wachezaji na kuwafukuza makocha akiwemo Denis Lavagne msimu uliopita.

Kocha huyo alifukuzwa baada ya mchezo wa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa KMC katika mchezo wake wa nne tu wa ligi, na wa sita kwa ujumla.

Wachezaji wa Azam FC walilalamika kwa mabosi kwamba kocha huyo alikuwa mkali sana.

Lakini sasa mabosi hawataki kumsikiliza mchezaji yeyote, anachosema kocha ndicho wanachofanya. Ndiyo maana amesema hakuna bonasi nao wametii ila wachezaji wameumia sana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live