Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema hata akipata nafasi ya kucheza tena na Yanga kesho atawafunga tena kutokana na namna alivyowasoma na kutambua ubora wao na madhaifu yao.
Azam juzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, lakini Dabo amesema ameshagundua udhaifu wa wapinzani wao, ingawa kuna sehemu ameona wana ubora mkubwa, ila hawawezi kumsumbua.
Akizungumza na Mwanaspoti, Dabo raia wa Senegal, amesema ameifuatilia Yanga na kubaini ubora ni namna wanavyomtumia Stephane Aziz Ki kama mchezesha timu hivyo alitoa kazi kwa wachezaji wake kutompa nafasi.
"Yanga ndani ya 18 wana wachezaji zaidi ya sita ambao ukiwaacha wakachezea mpira lazima watakufunga nilichokifanya niliwaandaa wachezaji wangu kuhakikisha wanamlazimisha Aziz Ki kucheza nje ya 18," amesema na kuongeza:
"Kazi hiyo niliwapa Yahya Zayd na Adolf Bitegeko, ambao walifanya kazi nzuri kuondoa uhuru wa Aziz Ki, nilivyowaona hata kama nikirudiana nao kesho nina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi."
Amesema mtego alioutega ulikuwa unawalazimisha wachezaji wa Yanga kupita mbembeni na sio katikati kama ilivyozoeleka mbinu ambayo ilikuwa ngumu kwao kupenya.
Dabo amesema timu yoyote ambayo inategemea viungo kuwalisha washambuliaji au kufunga wao wenyewe wakidhibitiwa mtego wao unakuwa umekufa hicho ndio kiliwatokea Yanga na wao kunufaika kwa kupata matokeo.
Amesema Aziz Ki angepewa nafasi ya kucheza eneo lake mara kwa mara angewaadhibu kwani ni mzuri akiwa na mpira eneo hilo na wao walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanamdhibiti.