Zimebaki saa zisizopungua 72 kabla ya Simba na Yanga kuvaana katika Kariakoo Derby itakayopigwa Jumamosi ya Aprili 20 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, likiwa ni pambano la 112 kwa timu hizo tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965, huku familia ya beki wa kati ya Yanga, Ibrahim Bacca ikigawanyika.
Wakongwe hao wa soka la Tanzania wanakutana katika pambano la marudiano la msimu huu wa Ligi Kuu Bara iliyopo raundi ya 23, zikiwa na kumbukumbu ya mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 5, mwaka jana na Siomba ilipigwa mabao 5-1.
Hata hivyo, sasa kutoka hapa Zanzibar ni familia ya Bacca aliyekuwapo katika pambano hilo la kwanza lililomfukuzisha kazi Kocha Mbrazili Roberto Oliveira 'Robertinho' imegawanyika kutokana na wazazi wa staa huyo kila mmoja kushabikia timu tofauti na tayari tambo zimeanza mapema hata kabla ya mchezo huo.
Wakizungumza na Mwanaspoti wakiwa nyumbani kwao visiwani Zanzibar, wazazi wa mchezaji huyo kwa nyakati tofauti walisema kwa sasa kila mmoja ana omba dua kivyake katika mechi hiyo yenye presha kubwa.
Baba mzazi wa beki huyo kisiki, Abdallah Hamad amesema yeye ni shabiki damu wa Yanga na kuweka bayana kwa sasa anachokitamani ni kuona kikosi anachokishabikia kinaibuka kidedea kwa mara nyingine.
Huku akiungana na mtoto wa mwisho wa familia hiyo, Mudhir Abdallah, ambaye naye ni Mwananchi walisema furaha yao ni kupata pointi tatu za nguvu.
“Tunachotaka ni kuona Simba, inapigwa tena kama mchezo uliopita na sasa kiwe kipigo kikubwa zaidi. Hata kama wamekuja Zanzibar kujifungia, lakini bado tuna kikosi bora kuliko wao, hivyo kipigo kiko pale pale,” amesema baba wa Bacca.
Simba imeweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na pambano hilo na taarifa zilizopo, itaondoka kesho kurudi Dar es Salaam ili kumalizia maandalizi yao, ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha anayeikabili Yanga kwa mara ya kwanza tangu alipoajiriwa mwishoni mwa Novemba mwaka jana.
Kwa upande wa mama mzazi wa staa huyo, Mwajina Makame alisema kwa upande wake anajua Yanga ipo vizuri kwa sasa kuliko Simba, timu ambayo anaishabikia tangu ujana wake, lakini anaiombea ipate matokeo yenye unafuu kuliko yale ya mchezo wa kwanza ilipolipuliwa kwa mabao 5-1.
Mwajina amesema licha ya tambo zote kwake anachokitamani ni kitu kimoja tu ambacho si kingine, sare.
"Tutoke sare tu au tufungwe bao moja tu maana tukifunga msala wote utahamia kwa mwanangu kwa sababu yuko safu ya ulinzi," amesema Mama Bacca na kuongeza;
"Nawaombea Yanga sare au ushindi mdogo wa bao moja kwa ajili ya Bacca tu, sitaki wamseme vibaya kupitia mechi kubwa kama hii."
Bacca ameanza kuitumia Yanga misimu miwili iliyiopita aliposajiliwa katika dirisha dogo akitokea KMKM, lakini amekuwa moja ya nguzo imara ya tiimu hiyo katika safu ya ulinzi anayocheza sambamba na nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job na Gift Fred.
Kabla ya kukipiga KMKM, nyota huyo aliwahi kupita Jang'ombe Boys na Malindi pia akizitumikia timu za taifa za visiwani Zanzibar, Zanzibar Heroers na ile ya Tanzania, Taifa Stars akishiriki nayo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika Ivory Coast mapema mwaka huu.