Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DTB yafuta makosa Kirumba, yafungua mwaka kibabe Championship

DTB Kirumba DTB yauanza mwaka 2022 kwa ushindi

Sat, 1 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Timu ya DTB ya jijini Dar es Salaam imeuanza mwaka mpya wa 2022 kwa shangwe baada ya kuendeleza kasi yake ya ushindi kwenye Ligi ya Championship.

DTB imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Bao hilo limefungwa mnamo dakika ya 79 kwa mkwaju wa penalti na Nicolas Gyan baada ya Tafadzwa Kutinyu kuangushwa kwenye eneo la hatari akiwa anawania mpira na mabeki wa Pamba.

DTB ni kama imerekebisha makosa yake katika uwanja huo baada ya kufungwa na Mbao FC bao 1-0 katika mchezo wa Kombe la shirikisho (FA) huku Gyan akifikisha mabao nane msimu huu.

Katika dakika ya 81 mwamuzi msaidizi namba mbili Fatuma Mambo Kutoka Iringa aliondoka eneo lake na kutishia kuondoka uwanjani wakati mchezo ukiendelea baada ya kurushiwa maneno na mashabiki wakidai amepotezea nafasi ya kuotea wakati Tambwe akikaribia kufunga bao la pili, hata hivyo waamuzi wenzake walimzuia na kumbembeleza na kukubali kuendelea na majukumu yake.

Matokeo hayo yanaifanya DTB kuvuna alama zote sita za Championship katika mkoa wa Mwanza, wakianza kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Gwambina na 1-0 mbele ya Pamba.

DTB sasa wanaendelea kung'ang'ania kileleni mwa msimami wa Ligi ya Championship wakifikisha pointi 33 huku Pamba wakisalia na pointi zao 16 katika nafasi ya saba.

Mshambuliaji wa DTB, Nicolas Gyan amekabidhiwa hundi ya Sh 250,000 baada ya kuibuka mchezaji bora wa mwezi Desemba akionyesha kiwango kizuri yakiwemo mabao matatu aliyofunga kwenye ushindi wa 5-3 mbele ya Gwambina  na kufikisha mabao Saba msimu huu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz