Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DR Congo ya Inonga na deni la miaka 50 AFCON

Congo Vs Inonga DR Congo ya Inonga na deni la miaka 50 AFCON

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Guinea juzi katika Uwanja wa Alassane Ouattara jijini Abidjan, Ivory Coast umeihakikishia timu ya taifa ya DR Congo tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu.

Mabao ya Yohanne Wissa, Chancel Mbemba na Arthur Masuaku yalitosha kufuta bao moja la Guine lililopachikwa na Mohamed Bayo na kuipeleka DR Congo katika hatua ya nusu fainali ambayo itakuwa ni mara ya tano kufanya hivyo tangu iliposhiriki Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1965.

Katika hatua hiyo ya fainali, DR Congo itakutana na mshindi wa mechi baina ya Ivory Coast na Mali zilizocheza jana usiku.

DR Congo kutinga hatua ya nusu fainali ya Afcon mwaka huu hapana shaka inajiweka katika nafasi nzuri ya kuhitimisha ukame wa miaka 50 wa kushindwa kutwaa taji la mashindano hayo kwani mara ya mwisho ilifanya hivyo mwaka 1974 ilipoibuka bingwa baada ya kuichapa Zambia kwa mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri.

Nusu karne ya unyonge

Kizazi cha DR Congo kilichotwaa ubingwa wa Afcon mwaka 1974 ni kama kiliacha nuksi kwa DR Congo kwenye Afcon kwani tangu hapo hadi sasa haikuwahi kunusa hatua ya fainali ingawa ilijitutumua nyakati kadhaa na kutinga nusu fainali.

Mafanikio makubwa ya DR Congo katika kipindi hicho cha miaka 50 tangu walipotwaa ubingwa wa mwisho kwenye Afcon yamekuwa ni kuingia nusu fainali wakifanya hivyo mara mbili tu ambazo ni 1998 na 2015 ambapo mara zote haikutoka patupu kwani iliambulia nafasi ya tatu.

Mwaka 1998 katika fainali zilizofanyika Burkina Faso, ilifungwa mabao 2-1 na Afrika Kusini na katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 4-4 katika muda wa kawaida na pia mwaka 2015 katika fainali zilizofanyika Guinea ya Ikweta ilifungwa mabao 3-1 na Ivory Coast kwenye nusu fainali huku yenyewe ikishinda kwa penalti 4-2 baada ya matokeo ya suluhu katika dakika za kawaida za mchezo.

Mwendo wa kinyonga

DR Congo haikuwa na mwanzo mzuri katika fainali za Afcon mwaka huu na hilo lilifanya wengi wasiipe nafasi angalau hata ya kufika hapo ilipo sasa hivi na hili linadhihirishwa na michezo iliyopita ya DR Congo kuanzia katika makundi hadi ule wa hatua ya 16 bora.

Ushindi wa juzi kwenye robo fainali ulikuwa ni wa kwanza kwa DR Congo kuupata ndani ya dakika 90 na kabla ya hapo haikushinda hata mechi moja katika muda wa kawaida wa mchezo.

Katika hatua ya makundi ambapo ilipangwa katika kundi F, DR Congo ilianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia, kisha ikalazimisha sare ya bao 1-1 na Morocco kisha ikatoka suluhu na Tanzania kwenye mechi ya mwisho ya makundi.

Mchezo wa hatua ya 16 bora ilikutana na Misri na kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 8-7 baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida wa mechi.

Namba zinazungumza

Katika mechi tano za mashindano hayo, DR Congo imefunga idadi ya mabao sita ikiwa ni wastani wa bao 1.2 kwa kila mechi na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne ikiwa ni wastani wa bao 0.8 kwa mechi.

DR Congo ni miongoni mwa timu zinazoonyesha nidhamu kubwa kwenye mashindano hayo na kuthibitisha hilo, timu hiyo katika mechi tano ilizocheza hadi sasa imekusanya idadi ya kadi saba zote zikiwa ni za njano, sawa na wastani wa kadi 1.4 kwa mechi.

Kikosi cha matumaini

Katika fainali hizo zinazoendelea huko Ivory Coast, wachezaji waliopo kwenye kikosi cha DR Congo ni Lionel Mpasi, Henoc Baka, Dimitry Bertaud, Baggio Siadi, Rock Bushiri, Gédeon Kalulu, Chancel Mbemba, Dylan Batubinsika na Arthur Masuaku, Kayembe na Brian Bayeye.

Wengine ni Meshack Elia, Théo Bongonda, Edo Kayembe, Gael Kakuta, Charles Pickel, Samuel Moutoussamy, Aaron Tshibola, Silas Katompa na Grady Diangana, Fiston Mayele, Cedric Bakambu, Yoane Wissa na Simon Banza.

Kocha wa timu hiyo ni Sebastien Desabre kutoka Ufaransa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live