Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DENZEL: Siyo Chama, Pacome tu mpaka Tshabalala

Denzel X Pacome DENZEL: Siyo Chama, Pacome tu mpaka Tshabalala

Wed, 28 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa wengi Ukisikia jina la Godfrey Mkinga itakuwa vigumu kujua ni nani anayezungumziwa, lakini ukitajiwa Denzel Trainer haraka utajua ni yule jamaa fundi wa kuwafua watu mbalimbali kwenye mazoezi ya kuimarisha miili.

Denzel amekuwa akiwapigisha tizi la nguvu la gym watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa kitaifa, wanamichezo, wanamuziki na hata watu wa kawaida ambao wamekuwa wakivutiwa na ufanisi wa mazoezi yake.

Baada ya kuwanoa na kuwapa mafanikio wanasoka mbalimbali wakiwemo John Bocco, Mohammad Hussein ‘Tshabalala’, Pacome Zouzoua na hata Clatous Chama, Mwanaspoti limetia timu na kusaka ili kujua undani wa kazi yake na siri ya mastaa kukimbilia kwake.

KABLA YA PACOME, CHAMA KUNA BOCCO

Denzel anasema kabla ya kuwanasa mastaa hao wa sasa wa Yanga huko nyuma alianza nahodha wa zamani wa Simba, John Bocco aliyekuwa akimpigisha tizi la maana tu na kuhakikisha kuwa anakuwa bora na fiti uwanjani.

“Watu wa michezo hasa soka mtu wa kwanza kabla ya kina Pacome nilikuwa nampa mazoezi John Bocco akiwa Simba, baadaye akafuata Chama wakati huo naye akiwa Simba,” anasema mtaalamu huyo mwenye taaluma ya mambo ya fiziki kutoka Uingereza na kuongeza:

“Chama alipoondoka Simba na kwenda Yanga aliendelea kuwa mwanafunzi wangu na sasa wakaongezeka Pacome na Tshabalala (Mohammed Hussein, nahodha wa sasa wa Simba).

“Kwa sasa nipo na hawa, lakini ndani ya muda mfupi ujao wataongezeka wengine nipo nao kwenye mazungumzo hivi karibuni nitaanza na mtawaona. Ninachoshukuru Mungu ni kwamba wote wanakuja kutokana na kuona mafanikio ya hawa nilionao.”

Denzel anasema hajakurupuka tu kuanza kutoa mafunzo kwani alipiga kitabu na hatimaye kufuzu kitaaluma na ndiyo maana anaifanya kazi yake kwa ubora.

“Hii taaluma nimeisomea Kenya, lakini hata hivi sasa nimemaliza mafunzo mengine ya taaluma hii kwa njia ya mtandao kule Uingereza kwa ngazi ya diploma, Juni mwaka, huu. Kwa hiyo nina elimu ya kutosha na sio kwamba nafanya kwa kubabaisha,” anasema.

MAZOEZI YA PACOME

Mtaalamu huyo wa mazoezi ya gym anasema, “kawaida kabla sijaanza kumpa mtu mazoezi hasa hawa wachezaji huwa nawaomba wanipe muda angalau siku tatu mpaka nne. (Huwa) hawaanzi mpaka niangalie mechi zao na kuangalia ubora wao uko wapi na upungufu uko wapi.

“Baada ya kujua hayo maeneo mawili, sitashughulika na mazuri yake nakwenda kuimarisha upungufu wake. Hizo mechi (wanazocheza) huwa naangalia zile kubwa.

“Kila mchezaji anayekuja kwangu najua udhaifu wake uko wapi. Kwa hiyo kwa Pacome nilikuja kugundua ni mchezaji mwenye kasi sana, lakini nilikuwa najaribu kuangalia alikuwa anakosa kidogo stamina. Siyo kwamba hakuwa kabisa (na stamina), anayo, lakini siyo kubwa sana. Mimi nikaanza kuhangaika na eneo hilo ili niiboreshe.”

Denzel anasema katika kipindi chote ambacho amekuwa akimuweka fiti mchezaji huyo wa kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast, kuna mambo mengi yameongezeka kwake.

“Stamina yake ndiyo hapo nilipoanzia kwamba mtu akimsukuma akiwa na mpira asiweze kumuachia (mpira) kirahisi, asiweze kwenda chini na ndiyo pale kwenye ile video (anaonyesha video) mnaona watu wanaizungusha alikuwa akisukumwa hakubali kirahisi kuachia mpira.

“Bado anaonekana yuko imara, ni kazi ambayo tuliifanya kwa kiwango kikubwa, lakini kama kusukumwa vile ingetokea kabla ya kupewa mazoezi niliyompa angeweza kuanguka kirahisi tu.”

Anazungumzia faida zaidi anazozipata Pacome kwa sasa baada ya kupigishwa tizi la nguvu, akisema: “Mazoezi ambayo nimekuwa nikimpa kiujumla yana faida nyingi sana. Kuimarisha kasi yake, stamina na kuupa mwili uwiano sawa sawa na hata nguvu za miguu. Ni mazoezi mazuri sana yanayomuimarisha mchezaji kwenye majukumu yake.”

WANAELEWANAJE?

Pacome siyo mchezaji anayejua sana kuzungumza Kiingereza wala Kiswahili, kwani anatumia Kifaransa muda mwingi kwa ajili ya mawasiliano na Denzel anaeleza namna wanavyoelewana.

“Huwa tunatumia Kiswanglish (yaani mchanganyiko wa Kiswahili na Kiingereza). Ni kweli hajui sana Kiingereza na mimi sifahamu Kifaransa, kwa hiyo tunatumia lugha hiyo huku pia tunazungumza kwa vitendo kama unavyojua haya ni mazoezi na mimi mbali ya kuwa mwalimu naanzisha safari kwa kuyafanya pia kwa vitendo,” anasema.

“Kuna maneno muhimu ya Kiswahili na Kiingereza anayajua mfano anaweza kusikia nahesabu moja, mbili, tatu au wakati mwingine nitahesabu kwa Kiingereza one, two, three anajua kwamba hapa mwalimu anahesabu ninachofanya na anafanya vizuri. Kwa hiyo hakuna shida kwenye maelewano kabisa.”

CHAMA NAYE IKO HIVI

Akimzungumzia Chama, Denzel anasema nyota huyo ambaye mashabiki wa Yanga wameanza kuchekelea makali yake ambayo amekuwa akiyaonyesha kwenye timu, ubora wake umeongezeka na mazoezi anayoyapata yamemuongea kasi na pia stamina.

“Chama ameimarika sana. Naona mengi ambayo tulifundishana yameongezeka kwake. Chama ni mchezaji mwenye nguvu ana stamina na ana akili kubwa ya kujua anachokifanya uwanjani, lakini alikuwa anakosa kasi,” anasema.

“Kwa hiyo nilipoanza kufanya naye kazi nikaanza na kasi yake, awe mwepesi (kitu) ambacho ndiyo alikuwa anakitaka.

Ukiangalia mechi iliyopita (dhidi ya Vital’O) mazoezi ambayo nilikuwa namfundisha ya wepesi na kasi ndivyo vitu alivyovionyesha pale.

“mchezaji akifanya vizuri mimi kama mwalimu wake nafurahia kitu ambacho amekifanya, mambo ya ufundi ni makocha wake wa klabu, lakini kwangu naona anaimarika kwenye maeneo ambayo nimekuwa napambana naye.

“Mara ya mwisho nilipofanya naye mazoezi nilimwambia nataka kuona anafunga bao au anatoa asisti kwa kuwa sasa yuko sawa. Nadhani mliona ile video (aliyokuwa akizungumza naye) na nilifurahia sana alipofanya kweli kwa kuwa mwili wake ulikuwa tayari.

CHAMA, MKEWE MAZOEZINI

Kuna video moja ilikuwa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii inayomuonyesha Chama akiwa anambeba mkewe mabegani kwenye mazoezi na Denzel anaeleza ilivyokuwa.

“Ile ilitokea kwenye mazoezi yetu na alitakiwa kuna zoezi alifanye ili kumalizia. Alishakuwa amefanya mazoezi ya kutosha na mke wake naye huwa anakuja naye mara moja moja naye huwa anajiweka sawa,” anasema.

“Sasa alipotakiwa kufanya mazoezi kama yale nikamwambia badala ya kunyanyua kitu chenye uzito ambebe mkewe kwa kuwa alikuwa na uzito wa kilo 62 ambazo ndizo alikuwa abebe uzito kama huo, kisha wafanye skwashi ndio pale mlipoona anafanya nadhani mkaona alikuwa anafanya kwa usahihi.”

WAKO FRESH

Akiwazungumzia Chama na pacome kwa pamoja, mtalaamu huyo anasema: “Chama na Pacome wako vizuri. Wanacheza timu moja wana mawasiliano mazuri, wanakutana hapa kwangu, wanacheka, wanapishana huyu anatoka, huyu anaingia kwa kuwa ratiba zao zinatofautiana ila wakikutana wanaongea kwa stori za kutosha.

“Mfano wiki ijayo wanaweza kukutana wote (Mohammed Hussein) Tshabalala, Pacome na Chama kulingana na ratiba ninayowapa hakuna shida wakikutana kwa sababu mfano Chama alikuwa anacheza pamoja na Tshabalala na unajua hawa ni wanamichezo wanakuwa tofauti uwanjani tu, ila huku nje ni watu wanaoshirikiana vizuri. Soka siyo uadui.”

TSHABALALA YUPO FITI

Denzel anasema kwa aina ya mazoezi ambayo anayapata Tshabalala na nidhamu yake sio rahisi beki huyo kupoteza nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba.

“Tshabalala ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Inawezekana wapo ambao wanajiuliza kwanini ameweza kudumu kucheza kwa muda mrefu na wala husikii ana majeraha au kucheza vibaya. Siri ni moja, Tshabalala ana juhudi kubwa ya mazoezi. Anaipenda kazi yake na kubwa kuliko yote ni mchezaji anayeishi kama mchezaji mkubwa wa Ulaya, ana nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja ndio maana wakati wote yuko fiti na anafanya vizuri,” anasema.

Pamoja na mastaa hao, lakini Denzel anasema wapo pia wengine wanaompigia hesabu za kwenda kupigishwa tizi ili kuboresha ubora wao uwanjani.

“Hapana, wachezaji ambao nafanya nao kazi ndio hawa mnaowaona kwa kuwa sioni kama kuna sababu ya kufanya usiri, lakini wapo wengine ambao nilisema awali kwamba watakuja muda si mrefu nao mtawaona. Ni wachezaji wakubwa na wengine wanachipukia. Tunamalizia mazungumzo na mtawaona hapa kwangu wanajiimarisha,” anasema.

“Namshukuru Mungu wachezaji wengi wanakuja kwangu. Najua kipi nakifanya na wenzao wanaifanya kazi na mimi, wanaimarika kwa kiwango gani. Unapoona kama haya unafarijika kwa kuwa kazi yako inaendelea kuwasaidia wengine.”

UKALI MAZOEZINI

Denzel anaweza wazi kuwa kwenye mazoezi yake kuna wakati analazimika kuwa mkali ili aweze kuona mafanikio kwa mtu anayemfanyisha mazoezi na mwisho yawe na majibu uwanjani.

“Mimi ni mkali, (lakini) sioy kila wakati. Ninapoona hapa nahitajika kuwa mkali kwa mwanafunzi wangu nafanya hivyo kwa kuwa ni mwalimu ambaye natamani kuona mwanafunzi wangu anafanikiwa kwa yale ambayo tumejipangia,” anasema.

Akizungumzia uzito sahihi anaopaswa kuwa nao mchezaji, anasema inashauriwa kwamba awe na kilo 80.

“Mchezaji wa soka haitakiwi azidi kilo 80, lakini anatakiwa awe kuanzia kilo 65 mpaka 78. Hapo anakuwa kwenye uzito sahihi utakaomfanya kutekeleza vizuri majukumu yake.”

MAWASILIANO NA MAKOCHA, WACHEZAJI

Mtaalamu huyo anasema katika ratiba yake na wachezaji ambao anawapigisha tizi na kuwafundisha mazoezi huwa haingiliani na ratiba ya mazoezi ya makocha wao kwenye klabu.

“Mimi ni kocha wa mazoezi ya ziada ya hawa wachezaji. Mchezaji ananifuata yeye binafsi na wala siyo kosa lazima mchezaji awe na ratiba binafsi ambayo kwa wachezaji hawa ndiyo hii ambayo naifanya kwao,” anasema na kuongeza:

“Wanapokuja kwangu sifuatwi na viongozi wala makocha wao, wanakuja wao kama wao. Kwa hiyo kwenye timu yake (mchezaJi) heshima ni kubwa, lakini wanapokuja hapa nawaimarisha kwa yale ambayo wanataka au tunakubaliana bila kuihusisha timu yake.”

Unajua gharama ya tizi lake, ratiba na mastaa wengine wanaopigishwa mazoezi ya nguvu? Usikose Mwanaspoti kesho!

Chanzo: Mwanaspoti