Kikosi cha Yanga Princess kimemuuza aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Cidalia Cuta kwenda kujiunga na FC Minsk inayoshiriki Ligi Kuu nchini Belarus.
Yanga imemuuza mchezaji huyo raia wa Msumbiji akiwa ni wa tatu kuuzwa nje msimu huu baada ya Blessing Nkor aliyetua Dogus Gold Asyapor ya Uturuki na Maimuna Hamis ‘Mynaco’ aliyejiunga na kikosi cha Zed FC kinachoshiriki Ligi Kuu ya Misri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo alisema mchezaji huyo wiki iliyopita alimalizia kufanya vipimo vya kiafya na kila kitu kwa sasa kipo sawa hivyo muda wowote kaunzia sasa watamtangaza kama mchezaji wao mpya.
“Watu wanaweza kujiuliza hatufanyi vizuri lakini tunauza wachezaji, ukweli ni klabu yetu imekuwa mstari wa mbele kuwasapoti wachezaji wa kike pindi wanapopata timu nje hivyo ikitokea fursa kwao tutafanya hivyo,” alisema na kuongeza;
“Soko la wachezaji wa kike ni dogo hivyo hatuna budi kuwaruhusu kwenda nje kutafuta changamoto nyingine ndio maana kuna wachezaji kama Blessing, Mynaco na Cuta ambao wote ni wazuri na tuliwahitaji zaidi msimu huu lakini tumeamua kuwauza.”