Supastaa, Cristiano Ronaldo amejipambanua duniani kama mwanasoka mahiri kuwahi kutokea kwenye mchezo huo na hilo linathibitika na wingi wa rekodi na medali alizowahi kubeba katika maisha yake ya mpira.
Ronaldo, 38, akiwa amefunga zaidi ya mabao 850 na kubeba mataji 32, staa huyo wa Ureno ameiweka juu sana grafu yake kwenye mchezo huo wa soka duniani na hilo linatokana na rekodi ambazo ameziweka na kuwafanya mashabiki kutania kwamba Ronaldo na rekodi ni kama vile amechanjia.
Hizi hapa rekodi zisizopungua 35 ambazo supastaa anazishikilia hadi sasa kwenye soka.
Ronaldo ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kimataifa, amefunga 123 katika mechi 201.
Ronaldo ndiye mchezaji aliyechezea Ureno mara nyingi zaidi kwenye mechi za kimataifa, 201.
Ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi za kimataifa kuliko yeyote, alipiku rekodi ya Al-Mutawa, Machi 2023.
Ronaldo ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao 100 kwenye michuano inayohusisha timu taifa.
Ronaldo ni mchezaji pekee aliyefunga mfululizo kwenye mechi 11 za kimataifa kati ya 2004 na 2022.
Ronaldo ni mchezaji wa kwanza na pekee kufunga bao katika fainali tano tofauti za Kombe la Dunia.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kinda wa Ureno (miaka 21 na siku 132) na mkongwe (miaka 37 na siku 292) kwa kufunga bao kwenye Kombe la Dunia.
Ronaldo ndiye mchezaji mwenye mabao mengi kwenye michuano ya ubingwa wa Ulaya, mabao 14.
Ronaldo ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi ya kimataifa ndani ya mwaka mmoja. 2017, mabao 32.
Ni mchezaji wa kwanza kufunga mabao 10 au zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na timu tatu tofauti.
Ronaldo ana mabao mengi kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya amefunga mabao 141, 12 zaidi aliyofunga Messi, 129.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mabao 17 katika msimu wa 2013-14.
Ronaldo ndiye mchezaji aliyefunga mara nyingi kwenye mechi za fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, fainali nne.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kufunga katika mechi zote sita za makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya msimu mmoja. Alifanya hivyo mara mbili 2017-18 na 2021-22.
Ronaldo ni mchezaji wa tatu kufunga dhidi ya timu moja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, yeye akiwa na klabu tatu tofauti. Timu hiyo ni Lyon ya Ufaransa.
Ronaldo alikuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu England na Kinda bora wa msimu ndani ya msimu huo huo, 2007-08.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyeifungia Manchester United mabao mengi kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu England, mabao 31.
Ni mchezaji pekee kwenye historia ya Man United aliyewahi kushinda Tuzo ya Puskas, kupitia bao lake aliloifunga FC Porto mwaka 2009.
Ronaldo ni mchezaji pekee kwenye historia ya Man United alishinda Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, 2008.
Ronaldo ni mchezaji pekee wa Man United aliyewahi kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka, 2008.
Ronaldo aliweka rekodi ya kufunga zaidi ya mabao 50 kwa misimu sita mfululizo kati ya 2011 na 2016.
Ronaldo ndiye kinara wa mabao wa muda wote Real Madrid, mabao 451 katika mechi 438.
Ronaldo ndiye kinara wa mabao wa muda wote wa Real Madrid kwenye La Liga, mabao 312.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao matatu au zaidi mara nyingi kwenye La Liga, amefanya hivyo mara 34.
Ronaldo ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi Real Madrid ndani ya msimu mmoja, mabao 61 katika msimu wa msimu 2014-15.
Ronaldo ndiye aliyefikisha kwa haraka mabao 200, 250 na 300 kwenye La Liga.
Ronaldo amevunja rekodi ya Juventus ya kufunga mara nyingi ndani ya msimu mmoja, mabao 37 katika michuano yote msimu wa 2019-20.
Ndiye mchezaji aliyefunga kwa haraka mabao 50 kwenye Serie A, akifikisha idadi hiyo ya mabao baada ya mechi 61 tu alizochezea Juventus.
Ronaldo ni mchezaji wa kwanza kufunga mabao 50 au zaidi kwenye Ligi Kuu England, La Liga na Serie A.
Ni mchezaji wa kwanza kufunga mabao 30 au zaidi ndani ya msimu mmoja katika Ligi Kuu tatu tofauti kati ya Ligi Kuu tano bora za Ulaya.
Baada ya kufunga tatu dhidi ya Cagliari, Januari 2020, Ronaldo akawa mchezaji wa kwanza wa Ureno kufunga hat-trick kwenye historia ya Serie A.
Ronaldo ni mmoja kati ya wachezaji wawili tu kufunga hat-trick kwenye Ligi Kuu England, La Liga na Serie A baada ya mkali wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic.
Ronaldo amempiku Rui Costa kwenye orodha ya wachezaji wa Ureno waliofunga mabao mengi kwenye Serie A baada ya kufikisha mabao 101 akiwa na kikosi cha Juventus.