Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corefa yafanya uchaguzi, Hasanoo ajitoa

Munisi Pic Robert Munisi

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Pwani (Corefa) kwa kauli moja wamemthibitisha Robert Munisi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho baada ya mgombea mwenzake Hassan Othuman 'Hasanoo' kutangaza kujitoa kabla ya uchaguzi huo.

Munisi amethibitishwa jana Agosti 13 baada ya mgombea mwenzake Hassan Othuman 'Hasanoo' kutangaza kujitoa kabla ya uchaguzi huo ambao awali ulitakiwa uwe ni wa uchaguzi wa kupiga kura ya kujaza nafasi hiyo ya Mwenyekiti.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kiomoni Kibamba amewaambia wajumbe kuwa kulitakiwa kuwe na uchaguzi wa nafasi moja tu ya Mwenyekiti wa Corefa ambao ungewashirikisha wagombea wawili Hassan almaarufu kwa jina la 'Hassanoo' na Munisi lakini mgombea Hasanoo amejitoa kwa barua aliyoiwasilisha katika Kamati hiyo.

"Kwa kuwa mgombea ni mmoja na kwa mujibu wa kanuni ya 19, kanuni ndogo ya 8 ya kanuni ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mnachotakiwa kufanya hapa ni kumthibitisha tu huyu mgombea aliyepo mbele yenu, Je mnamthibisha ndugu Robert Munisi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani Corefa?" Kibamba aliwauliza wajumbe wa mkutano huo na wote kwa pamoja wamemthibitisha.

Munisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilayani Kibaha (Kibafa) alipoulizwa kuhusu kushika nafasi mbili hizo amesema anazimudu na ataendelea kushikilia kofia zote mbili huku akisema Katiba haijambana japo kwa hapo baadaaye anaweza kuachia mojawapo ili aweze kutenda kazi kwa ufanisi zaidi.

"Namshukuru Mungu ndoto niliyokua naiota zaidi ya miaka saba ya kuwa kiongozi wa Corefa, imetimia leo hii nawaomba Kamati tendaji ya Corefa, wajumbe wake na wadau wote wa soka ndani ya mkoa wa Pwani tushirikiane ili soka la Mkoa wa Pwani ambalo lilikua limedorora liamke na kung'ara sasa" amesema Munisi

Mwenyeki huyo kwa mamlaka aliyonayo amemtangaza Mohammed Lacha kuwa Makamu Mwenyekiti Corefa, Katibu ikibaki kwa Mohammed Masenga ambaye alikua katika nafasi hiyo kweye kipindi kilichopita.

Pia Viongozi na wajumbe wa kamati mbalimbali ikiwemo wa soka la wanawake walitangazwa huku Kanda mbili za kimichezo ya kusini na kaskazini zikitangazwa.

Chanzo: Mwanaspoti