Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Copco yashinda, yasaka sare kubaki Championship

Hhahshahs Copco yashinda, yasaka sare kubaki Championship

Thu, 9 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Copco FC imeanza kwa ushindi nyumbani ili kubaki Ligi ya Championship kwa kuifunga Stand United ‘Chama la Wana’ mabao 2-0 huku ikihitaji sare katika mchezo wa marudiano ili kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.

Mchezo huo wa mtoano (playoff) kusaka nafasi ya kubaki Ligi ya Championship umechezwa leo Mei 8, 2024 katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni, huku mchezo wa marudiano ukipigwa Mei 12, uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambao umechezeshwa na mwamuzi, Mangile Hobu kutoka Geita kilikuwa wazi kwa timu zote mbili zikishambuliana na kwa zamu, lakini dakika 10 za mwisho za kabla ya kwenda mapumziko mambo yakabadilika ghafla.

Copco FC imepata penalti mbili dakika ya 32 na 40 baada ya mabeki wa Stand United kunawa mpira wakijaribu kuokoa hatari langoni mwao, mikwaju hiyo yote miwili imepachikwa nyavuni na mshambuliaji, Salum Ngadu na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.

Ngadu ameshindwa kuondoka na mpira (kwa kufunga hattrick) na kuiandikia timu yake bao la tatu, baada ya mkwaju wake wa penalti dakika ya 53 kuokolewa na kipa wa Stand United, Peter Mashinji. Penalti hiyo imepatikana baada ya nahodha wa Copco, Khalid Kibailo kuangushwa eneo la hatari na mwamuzi kutenga penalti.

Dakika ya 70, mshambuliaji wa Stand United, Warsha Machungwa ameifungia timu yake bao akiunganisha krosi ya upande wa kulia lakini bao hilo limekataliwa na mwamuzi kwa kuwa ameotea.

Ushindi huo ni muhimu kwa Copco FC ambayo inasaka kwa udi na uvumba nafasi ya kubaki Championship, hivyo inahitaji sare tu katika mchezo wa marudiano ili icheze michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo.

Mchezo huo ni wa tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu, ambapo Stand United imeshinda mechi mbili kwenye ligi ikiifunga Copco mabao 2-1 Kambarage na kushinda tena 2-0 Nyamagana, ambapo ushindi wa leo Copco FC imelipa kisasi.

Kocha wa Stand United, Seleman Kitunda, amesema adhabu za mikwaju ya penalti ambayo imeadhibiwa timu yake ni halali kwa sababu mabeki wake hawakuwa makini wakati wa kuokoa wakiwa hawajaweka mikono nyuma, huku akitamba kuwa bado wana nafasi ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano.

Naye Kocha wa Copco FC, Feisal Hau amesema lengo lilikuwa kuvuna ushindi mkubwa nyumbani, lakini mambo hayakwenda sawa huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kutoruhusu bao ambapo amewaahidi mashabiki kufanya vyema ugenini.

Chanzo: Mwanaspoti