Licha ya kuhamia Uwanja wa CCM Kirumba baada ya kutopata matokeo mazuri dimba la Nyamagana, mambo yameendelea kuwa magumu kwa Copco FC ya Mwanza kwenye Ligi ya Championship baada ya kupoteza mchezo mwingine wa nyumbani leo.
Timu hiyo imekubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Fountain Gate ya Dodoma kwenye mchezo wa raundi ya 17 ambao umepigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10 jioni.
Bao pekee katika mchezo huo limefungwa na Sadick Said mnamo dakika ya 18 na kudumu kwa dakika zote 90 za mchezo huo, huku Fountain Gate ikikosa nafasi nyingi za wazi.
Kipigo hicho ni cha pili mfululizo kwa Copco FC kupoteza nyumbani katika Uwanja wa Kirumba, ambapo mchezo uliopita ilichapwa 3-2 na JKT Tanzania huku ikibanwa mbavu na Mbeya Kwanza na kuambulia sare ya 2-2.
Copco FC imeshinda mchezo mmoja pekee nyumbani kwenye ligi hiyo, ilipoichapa Mashujaa FC 1-0, licha ya kusepa Nyamagana na kuhamia CCM Kirumba lakini mambo yamekuwa magumu kwao.
Ushindi huo umeipeleka Fountain Gate katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikifikisha pointi 33 huku Copco akisalia na pointi 13 katika nafasi ya 14.
Copco itakuwa na nafasi ya kujiuliza kwenye mchezo ujao wa ligi dhidi ya Pamba Februari 12 katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Licha ya matokeo hayo, Kocha wa Copco, Fulgence Novatus ameapa kuwa timu hiyo haitoshuka daraja huku Mwenyekiti, Simon Romli akisisitiza kuwa wanafanya juu chini timu ipate matokeo na mchezo dhidi ya Pamba watahakikisha ushindi unapatikana.